
Kigoma. Uamuzi wa raia wa Burundi, Isaka Erick (20) kukiri kosa la kuua bila kukusudia, umemuokoa na adhabu ya kifo iwapo ingethibitishwa alilitenda kwa kukusudia na akatiwa hatiani.
Kwa mujibu wa kifungu cha 196 cha Kanuni ya Adhabu kama kilivyofanyiwa marejeo mwaka 2022, mtu yeyote ambaye kwa dhamira ya uovu anasababisha kifo cha mtu mwingine kwa kitendo kisicho halali ana hatia ya kuua kwa kukusudia.
Adhabu ya kuua kwa makusudi inapatikana katika kifungu cha 197 cha Kanuni ya Adhabu iliyorejewa Mwaka 2022, kinachoeleza mtu ambaye amepatikana na hatia ya kosa la kuua kwa kukusudia adhabu yake ni kunyongwa hadi kufa.
Hukumu ya kifungo cha miaka mitano na miezi sita jela kwa Erick imetolewa leo Februari 26, 2025 na Jaji John Nkwabi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma.
Jaji amesema kukiri kwake kosa mapema kumeokoa muda wa mahakama na gharama za Jamhuri.
Amesema katika hatua za awali, Erick alishtakiwa kwa kosa la mauaji ya kukusudia ya Kizito Ramadhan yaliyotokea Julai 30, 2023 eneo la Kibirizi, wilayani Kigoma.
Amesema leo Februari 26, upande wa Jamhuri umebadili hati ya mashitaka kutoka mauaji ya kukusudia na kuwa ya bila kukusudia ambayo kulingana na kifungu cha 198 cha Kanuni ya Adhabu, adhabu ya juu huwa kifungo cha maisha.
Baada ya kubadilishwa hati hiyo na mshtakiwa kukiri kosa, alisomewa maelezo ya namna kosa lilivyotendeka na kuyakubali. Mahakama imemtia hatiani kwa kosa hilo, huku upande wa Jamhuri ukiomba apewe adhabu kali.
Wakili wa Serikali aliyeendesha shauri hilo aliyetajwa kwa jina moja la Mpozemenya alipendekeza adhabu ya kifungo cha miaka 15 akitoa sababu tatu, moja ikiwa kosa lilifanyika kwa kutumia silaha hatari ambayo ni kisu.
Sababu ya pili ni kuwa Ramadhan (marehemu) alimsihi mshtakiwa aondoke nyumbani kwake alikokuwa akimtukana na tatu ni kuwa, mshtakiwa alisababisha jeraha kubwa kwa marehemu kisha alitoroka.
Alisema iwapo mshtakiwa angemsaidia Ramadhan aliyemjeruhi kwa kisu, ingekuwa sahihi na wazi kwake kuomba apewe adhabu ndogo.
Wakili wa mshtakiwa
Wakili wa mshtakiwa aliyetajwa kwa jina moja la Rwegoshora aliiomba mahakama itoe adhabu ndogo ya miaka minne kutokana na ukweli kuwa ni mkosaji wa kwanza, ni kijana mdogo mwenye miaka 20 na amekiri kosa, kuokoa muda wa mahakama na wa Jamhuri.
Alisema kiini cha tukio hilo ni ugomvi baina ya mshtakiwa na Ramadhan kwa hiyo naye alichangia kusababisha kifo chake, akieleza ni raia wa Burundi, hivyo adhabu hiyo itamfanya awe balozi mzuri nchini kwake.
Hukumu ya Jaji
Katika hukumu, Jaji Nkwabi amesema amezingatia maombolezo kuwa mshtakiwa ni mkosaji wa mara ya kwanza na kwamba, mauaji yalitokana na ugomvi na mshtakiwa alikuwa juu ya kilevi (kwa maana kuwa alikuwa mlevi).
“Upande wa mashitaka unaomba itolewe adhabu kali kwa sababu kosa la kuua bila kukusudia ni moja ya makosa makubwa hasa kutokana na mshtakiwa kutumia kisu, lakini utetezi nao wanaomba apewe adhabu ndogo,” amesema na kuongeza:
“Moja ya sababu ya kuomba adhabu ndogo ni kwamba, mshtakiwa alikiri kosa hivyo kuokoa muda wa mahakama na gharama kwa upande wa mashitaka, aliisaidia Polisi katika upelelezi na amekaa mahabusu mwaka na miezi mitano. Ni dhahiri mshtakiwa anajutia kosa la kumuua (marehemu) pasipo kukusudia,” amesema.
“Katika mazingira ya kawaida, kosa la mauaji ya bila kukusudia linakaribisha adhabu ya kati ya miaka 20 na kifungo cha maisha jela, hoja zilizotolewa na pande mbili zinapaswa kuzingatiwa wakati wa kupima adhabu kwa mazingira ya kosa,” amesema.
Jaji amesema: “Kwa sababu ya aina ya kosa lilivyotendeka, eneo la kuanzia ni miaka 20 jela. Lakini kwa sababu ni mkosaji wa mara ya kwanza, 1/3 (theluthi) inaondolewa katika miaka 20 na kukishusha kifungo hadi miaka 14.
“Kwa kuwa mshtakiwa amekiri kosa, hakuisumbua mahakama na hivyo kuokoa muda na gharama za upande wa Jamhuri, basi moja ya tatu inaondolewa katika miaka 20, kwa hiyo ukiondoa hiyo moja ya tatu, tunabakiwa na miaka minane,” amesema na kuongeza:
“Mshtakiwa amekaa mahabusu gerezani kwa mwaka mmoja na miezi sita ambayo ninaipunguza katika miaka minane na kubakiwa na miaka sita na miezi sita. Kwa vile aitoa ushirikiano kwa vyombo vya upelelezi nampunguzia mwaka mmoja.”
Kutokana na ukokotoaji huo wa hesabu, Jaji amesema mshtakiwa atatumikia kifungo cha miaka mitano na miezi sita ambayo kwa maoni yake inatosha kwa kosa alilolifanya na itakuwa fundisho kwa wengine wenye nia ya kutenda kosa hilo.