Raha na karaha za wasanii kwenye Lebo

Dar es Salaam. Ni wazi kuwa uwepo wa rekodi lebo nchini umeibua vipaji vya wasanii wengi wakali wenye kuiwakilisha nchi katika kiwanda cha burudani. Wanapotajwa wakali kama vile Rayvanny, Harmonize, Ibraah, Zuchu, D Voice, Lavalava, Mbosso, Anjella wote ni matunda ya lebo hizo.

Kutokana na maendeleo ya biashara ya muziki nchini uwepo wa rekodi lebo umekuwa ukiongezeka kila kukicha. Utakumbuka majina kama WCB ya kwake Diamond, Konde Gang ya Harmonize na hata King Music ya Alikiba ni kati ya lebo nyingi nchini ambazo zimeanzishwa.

Lebo iliyofungua macho ya wengi ni WCB  ya kwake Diamond Platnumz iliyoanzishwa mwaka 2015 na kumtambusha msanii wake wa kwanza Harmonize. Kisha baadaye kuongoza wengine kama vile  Rayvanny (2016), Queen Darleen (2016), Rich Mavoko (2016), Lava Lava (2017), Mbosso (2018), Zuchu (2020) na D Voice.

Hata hivyo, wasanii watatu walioachana na lebo  hiyo wamefungua zao.  Rich Mavoko – Billionea Kid, Harmonize – Konde Music Worldwide na Rayvanny – Next Level Music (NLM).  Kati yao Mbosso tu ndiyo bado kufanya hivyo.

Licha ya hayo wakati Harmonize akijitoa kwenye lebo hiyo kuliibuka mzozo ikiwemo wa kulipa Sh 600 milioni kwenda kwa lebo hiyo.

Utakumbuka alipotoka WCB, Harmonize alianzisha lebo yake ya Konde Gang, kisha akamsajili Ibraah na baadaye akaongeza wasanii wengine akiwemo Country Boy pamoja na kuwavuta wasanii waliokuwa wanafanya kazi Kings Record ya Alikiba, Cheedy na Killy. 
Mpaka dakika hii Konde Gang imebaki na Harmonize pekee baada ya Ibraah kuondoka kwa mzozo huku akidai lebo hiyo ilimtaka alipe Sh1 bilioni.

Siyo hizo tu mwaka 2020 Shilole alitangaza kuanzisha lebo ya muziki inayoitwa Shishi Gang. Siku anatangaza lebo hiyo kwa mara ya kwanza ilikuwa pia ni siku ambayo alimtangaza ‘msanii wake’ anayeitwa Renzo.

Mpaka hivi sasa Renzo siyo msanii wa Shishi Gang tena, lakini Shishi Gang bado ipo na 2023  ilitambulisha msanii mpya anayeitwa Nice ambaye hasikiki mwa chochote 
Mwaka 2016, Ommy Dimpoz alianzisha lebo yake ya muziki ya kuitwa PKP na alimtambulisha msanii anayeitwa Nedy Music. PKP hadi sasa watu wengi hawaifahamu.

Mwaka 2020 rapa Joh Makini alizindua lebo yake na kuipa jina la Makini Records. Wakati anazindua pia alimtambulisha ‘msanii wake’ anayeitwa Ottuc William, lakini kwa mujibu wa Instagram ya Ottuck haionyeshi kama bado ni msanii wa Joh Makini. 

Mwaka 2021, Rayvanny alizindua lebo yake inayoitwa Next Level Music na pia alimtambulisha MacVoice. Habari nzuri ni kwamba Macvoice bado yuko Next Level. Lakini kazi zake hazionekani mbali na hao wapo na wengine walioanzisha lebo lakini hadi sasa hatma zake hazifahamiki.

Licha ya uanzishwaji wa lebo hizo na kuwa na faida katika kiwanda cha burudani   bado kunaonekana kuwepo kwa  kirusi kinachochochea migogoro kwa wasanii na mabosi wao kila wanapotaka kujiengua katika lebo hizo, kama ilivyotokea kwa baadhi ya wasanii. Huku chanzo kikuu kikiwa ni mikataba wanayoingia.

Akizungumza na Mwananchi  Mkuu wa Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) Dk Herbert Makoye amesema wasanii wawe na tabia ya kusoma na kuielewa mikataba kabla ya kusaini ili kuepusha uadui wakati wanataka kujitoa kwenye lebo hizo.

“Kuna kitu kinaitwa mihemko, kama mtu kahangaika zaidi ya miaka mitano barabarani,  hamadi unapata kazi unasaini haraka asije akasaini mwingine. Baadaye ukijitambua unagundua ulisaini vitu ambavyo siyo.

“Inawezekana kuna wengine wanaingia kwenye lebo bila mikataba, alafu ndiyo inafuata baadaye. Pamoja na hayo lebo  nazo zisiwawekee wasanii masharti magumu. Zikimbuke hazipo tu kwa ajili ya biashara kutafuta hela  bali ni pamoja na kukuza tasnia ya muziki.Ili mtu akitaka kuondoka asiwe adui,”anasema.

Anasema  msanii akifikia hatua ya kuingia kwenye lebo aangalie mikataba  na siyo lazima aijue yeye  tu badala yake  atumie wanasheria pia.

“Wapeleke kwa wanasheria na hapa Tanzania tumesema hivi ukipata mkataba nenda  Basata kuna mwanasheria wa bure hana haja ya kufanya siri. Mwanasheria anatafsiri vyote maana mkataba unasaini baada ya  majadiliano unaweza kuomba hata kuondoka nao,”anasema. 

Aidha kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Sheria Baraza la Sanaa la Taifa (Basata), Christopher Kamugisha anasema janga hilo la migogoro limekuwa kubwa lakini ni kwa sababu wasanii wachache tu ndiyo wanaofika Basata kupewa msaada wa kisheria kabla ya kusaini mikataba.

“Kwa mujibu wa kanuni zetu zinasema  kabla mtu hajasaini mkataba  wowote, anaweza akaleta ukapitiwa na anashauriwa. Wasanii tunawashauri mara kwa mara wawasilishe  nakala ambayo wanaletewa na lebo, msanii au hata na meneja.

“Tunatapitia tunamshauri,  lakini mkataba ni makubaliano wa pande mbili kila mtu. Kinachofanyika ni wachache wanaleta wengine wanaleta wakiwa wamepata shida baada ya kusaini,”anasema.

Utakumbuka Mei 6 2025, Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) lilitangaza kuwa lipo mbioni kuanzisha muundo wa mikataba ya kazi za muziki, ambao unalenga kupunguza changamoto zinazoikumba sekta hiyo nchini.

Mikataba hiyo ya mfano itakuwa mwongozo kwa wasanii, mameneja wao na kampuni za kurekodi (record labels), kuhusu mambo muhimu ya kuzingatia ili kusaidia kupunguza matatizo ambayo yamekuwa yakijitokeza mara kwa mara katika tasnia ya muziki.

“Kumekuwa na changamoto kubwa sana linapokuja suala la mikataba. Sisi kama Baraza la Sanaa tumegundua kuwa mivutano mingi tunayopokea inatokana na mikataba isiyoeleweka vizuri.

“Kwa hiyo, tunakwenda sasa kama Baraza kuwa na model ya mikataba, ambayo hata kama haitakuwa kamili kwa asilimia mia moja, angalau itasaidia kupitia maeneo muhimu ili kuondoa changamoto ambazo tumeziona.,” alisema Afisa Sanaa Mwandamizi kutoka BASATA, Abel Ndaga.

Mbali na hayo akizungumzia kinachowaponza wasanii wengi kusaini mikataba bila kuielewa msanii wa muziki wa Singeli nchini, Menja Kunta anasema kuna umuhimu wa wasanii  kuelimishwa kabla ya kuingia kwenye lebo. 

“Binafsi nimekaa kwenye lebo zaidi ya moja nafikiri inabidi wasanii waandaliwe kisaikolojia.Kwa sababu wanapochukua msanii anakuwa hana chohote kila anacholetewa kwenye maisha yake kinakuwa kipya msanii hajawahi kuwa na gari anapewa, anakaa nyumba nzuri.

“Kila kitu anapewa kama mimi nilitolewa Temeke nikapangiwa Ununio mwaka 2018 kwa hiyo nikaanza kuishi maisha mazuri. Menejimenti zetu zinawekeza sana. Lakini kabla ya kuwachukue wasanii muwe mnawapa mwongozo kwamba ni biashara ili kupunguza hizi lawama za kila siku,”anasema

Naye msanii wa muziki wa Hip Hop, Musa Mabumo maarufu kama Bando, anasema kuwepo kwa muundo sawa ya mikataba kutoka Basata kutapunguza migogoro nchini kwenye sekta ya burudani.

“Nadhani model  zitazotolewa na Basata ziwe za pande mbili zimwangalie msanii na pia mwekezaji anayemuunga mkono. Ziwe na usawa ili isionekane msanii pekee ndiye anayestahili huruma, bali hata mwekezaji apewe haki yake. Hilo litaongeza imani na kuvutia wawekezaji zaidi kwa wasanii,” alisema Bando.
 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *