
Abby Kwesa, baba wa watoto watatu anayeishi jijini Dar es Salaam, anakumbuka namna mama mzazi wa mchumba wake alivyoharibu ndoto ya maisha yake.
Anasema alishajiandaa kuanza maisha ya ndoa na msichana aliyempenda.
Akapeleka posa nyumbani kwa wazazi wake, ambapo hata hivyo aligonga mwamba, kisa ni mama wa mchumba wake kutokuwa tayari binti yake aolewe bila ya kuwa na ajira.
Kwesa anasimulia: ” Mimi nilimaliza chuo mbele yake, tukapanga tuoane akimaliza masomo. Ulipofika wakati nikapeleka posa. Kwanza walitaka wanijue mimi ni mtu wa aina gani. Awali nilipoonana nao upande wa baba waliridhika kuwa nilikuwa na sifa ya kumuoa binti yao, hivyo nikatakiwa kupeleka posa.
“Sikufanya ajizi, nilizungumza na wazazi wangu posa ikapelekwa. Na kwa kuwa wahusika ni Waislam, posa ilipokelewa kwa baba ambaye aliafiki kama ‘ walii’ (mtoa idhini ya ndoa)
“Kumbe mama yake hakuwa tayari, akaweka mguu katika ile ndoa akidai mwanawe haolewi mpaka apate ajira. Nilikuja kugundua baba na mama yake walitengana siku nyingi na ilionekana mama alikuwa na nguvu zaidi, pengine kwa sababu ndiye aliyemlea.
“Kingine niligundua kuwa mama aliamini kuwa kwa kuwa amemsomesha mwanawe, alipaswa amsaidie kimaisha, hivyo kumruhusu aolewe pengine binti yake angegeuka mama wa nyumbani na hivyo yeye kukosa msaada wa maisha.
Alipokataa tukajipa muda mimi na mchumba wangu, tukisubiri apate kazi. Hakufanikiwa kuipata kwa haraka Muda ulivyoyoyoma,mie nikaamua kuachana naye.Mungu si Athumani miaka michache baadaye akafanikiwa kupata kazi ya maana, akajaribu kurudi tena kwangu lakini ilishindikana kwa sababu nami nilishapangan kuwa na maisha mengine. Kilichobaki kilikuwa historia, nakumbuka alizalishwa watoto wawili nje ya ndoa.”
Uhalisia ulivyo
Kisa cha Kwesa ni kielelezo tosha cha masaibu kadhaa wanayopitia baadhi ya watu kwenye uhusiano hasa pale wazazi wanapoamua kuingilia kati uhusiano huo kwa sababu mbalimbali
Ni sababu zinazoweza kuwa na mashiko lakini nyingine zinatajwa kama udhaifu wa wazazi ambao mara nyingi huharibu maisha ya watoto wao kama ilivyokuwa kwa mchumba wa Kwesa aliyelazimika kuzaa nje kinyume cha maadili ya dini yake na desturi za Kitanzania.
Nafasi ya wazazi
Swali muhimu, je, wazazi hawapaswi kuingilia uhusiano wa watoto wao?
Mwalimu mstaafu Bakari Heri anasema wazazi wanaweza kuingilia kati pale wanapohisi uhusiano huo unaweza kuwa na athari, japo anakiri kuwa mwenye uamuzi wa mwisho anabaki kuwa yule mwenyewe aliyependa.
” Mzazi yeyote makini hawezi kukubali kumpoteza mwanawe kuingia katika uhusiano ambao anadhani utamletea shida.Nikupe mfano, mzazi anayejua kwa mfano binti yake ana uhusiano na jambazi, muuza dawa za kulevya, amwache mtoto wake akaangamie kisa amempenda na ndio chaguo lake? ” anahoji Mwalimu Heri na kuongeza:
‘’Kumkataza mtoto kwa sababu zisizo na mashiko kama vile umasikini au uduni wa familia ya mpenzi wa mtoto wako, hizi hazina maana na sidhani kama zinaweza kumuathiri mtu. Unaweza ukawa na mwenza masikini leo, kesho akabadilika na kuwa tajiri. Umasikini hauwezi kuwa kikwazo cha kumzuia mtoto asioe au asiolewe. Lakini tabia mbovu inaweza kukupa uhalali mzazi kumkanya mwanao. Ipo mifano ya wasichana walioangamia kwenye janga la Ukimwi kwa sababu tu waliolewa na wanaume viwembe. “
Mwanasiasa maarufu nchini na Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, aliwahi kulieleza Mwananchi siku za nyuma kuwa, hawezi kungilia kati uchaguzi wa wachumba kwa watoto wake wawili wa kiume, akisema ana heshimu uamuzi wa mtoto.
“Siko hivyo kabisa, wewe utakayemleta ndiye huyo huyo si umemkubali wewe? si utaishi naye? Sasa mimi ni nani wa kuanza kukwambia aaahh, najua huwa mnafanyaje huko mkiwa peke yenu?, sijui umempendea nini? Sina presha kabisa kwenye hilo,” alisema Lissu katika mahojiano maalumu kuhusu maisha yake nje ya siasa.
Hoja ya Lissu inaungwa mkono na mama wa watoto watatu, mkazi wa Dar es Salaam, Lilian Timbuka, anayesema katika jamii nyingi, ndoa sio muunganiko wa watu wawili pekee, bali ni muunganiko wa familia mbili.
Kwa mtazamo wake huo, anasema wazazi wanaposhiriki katika kuchagua mwenza, wanaweza kuhakikisha kuwa familia zinapatana na zina uhusiano mzuri, jambo ambalo linapunguza migogoro ya kifamilia katika ndoa.
Anaeleza kuwa katika zama za sasa, vijana wengi wanaathiriwa na dhana za kimapenzi zinazoonyeshwa kwenye filamu, tamthilia na mitandao ya kijamii, ambazo si za uhalisia wa maisha halisi.
‘’Sasa wazazi wanapochagua mwenza, mara nyingi wanaangalia mambo ya msingi kama maadili, utulivu wa maisha na heshima badala ya mapenzi ya muda mfupi,’’ anasema.
Anaongeza: ;;Wazazi wanapochagua au kukubaliana na chaguo la mtoto wao, ni kwamba wanataka kuhakikisha ndoa hiyo inakwenda kudumishwa kwa kuzingatia mila na desturi za kifamilia, jambo ambalo linaweza kusaidia mshikamano nadnia ya familia.’’
Hata hivyo, anasema ingawa wazazi wanaweza kuzingatia vigezo muhimu, haimaanishi kuwa ndoa itakuwa yenye mafanikio kama wawili hao hawatakuwa na maelewano au haiba zao kutopatana.
‘’Katika baadhi ya matukio, wazazi wanaweza kuwa na matarajio makubwa kutoka kwa ndoa wanayoipanga kwa mtoto wao, lakini kama itakuwa na changamoto, inaweza kusababisha migogoro kati ya mtoto na wazazi wake, hasa ikiwa hakuwa na uhuru wa kuchagua mwenza wake mwenyewe,’’ anafafanua.
Wasemavyo wanasaikolojia
Mtaalamu wa Saikolojia, Dk Neema Mwankina anasema kwa sasa faida za kumchagulia mtoto mwenzi ni ndogo ukilinganisha na miaka ya nyuma.
“Wazazi walikua wakiwachagulia wenza watoto wao kutokana na mila na desturi za kipindi kile, na kwa kiasi kikubwa zilisaidia kupunguza magonjwa ya kurithi kwa kiasi kikubwa kama vile kifafa na kisukari,”anaeleza
Dk Mwankina anasema, kwa miaka ya sasa ni vigumu kumchagulia mtoto mwenza kutokana na mabadiliko ya kitabia anayoweza kukutana nayo mtoto aingiapo kwenye ndoa.
“Kwasasa hakuna faida ya kumchagulia mtoto mwenza; unapoona mwenza wa mtoto wako ana tabia fulani, chukua jukumu la kumkanya na kumuelekeza kuwa si hivi bali ni hivi ili waende sawa,”anasema.
Anasema kumchagulia mtoto kipindi hiki wanaweza wasipendane na wasielewane na kuwafanya watoto wasiiishi maisha sahihi katika ndoa.
Anaeleza kuwa wazazi wanachopaswa kufanya ni kuwasikiliza watoto wao na kuwapa ushauri wa kuchunguza familia za wenza wao kabla ya kuingia kwenye ndoa.
“Kama ni mwananume ajitahidi kuijua familia ya mwanamke wake na mtoto wa kike, vilevile ajitahidi kuwajua upande wa mwanaume,”anaeleza.
Anasema kuwa kufahamu familia ya upande wa mwenza wako, kutasaidia kujua unaingia kwenye familia ya aina gani na kama ina magonjwa ya kurithi.
“Kufahamu yote hayo, kutampa nafasi ya kufanya uamuzi sahihi kabla ya kuingia kwenye ndoa,”anasema.
Kwa upande wake, mwanasaikolojia, Charles Nduku anasema japo hasara ni nyingi za mzazi kumchagulia mtoto, lakini faida nazo zipo ikiwemo kumshauri mtoto kwa busara zaidi.
“Wengi tunapoingia kwenye uhusiano tunafanya uamuzi kwa hisia na si akili na busara kama watakazotumia wazazi kutoa ushauri kuhusu mwenza kabla ya kuingia kwenye ndoa,”anaeleza.
Hata hivyo, anasema hasara za mzazi kumchagulia mtoto mwenza, ni pamoja na kuwapa ugumu wenza hao kuwa na upendo kati yao.
Anasema tatizo hilo ndilo linalochangia wanandoa wengi kuishi nyumba moja bila upendo.
“Zinapotokea tofauti kwa wanandoa waliolazimishwa watashindwa kutatua tatizo na badala yake watamshukia aliyemtafutia mke na kumpa mashtaka,”anaeleza.
Hasara nyingine Nduku anasema ni kuathiriwa kihisia kwa mwanamke au mwanaume baada ya kuchaguliwa mwenza.