Radiamali za kwanza za kimataifa katika kulaani hujuma za utawala wa Kizayuni dhidi ya Iran

Wizara za mashauri ya kigeni za Saudi Arabia, Malaysia, Pakistan na Oman zimetoa taarifa tofauti zikilaani hujuma za kijeshi za utawala wa Kizayuni dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Idara ya Mahusiano ya Umma ya Ulinzi wa Anga wa Iran imetoa taarifa ikisema kuwa leo Jumamosi alfajiri utawala wa Kizayuni wa Israel umeshambulia vituo vya kijeshi vya mikoa ya Tehran, Khuzestan na Ilam ikiwa ni katika kuzidisha hali ya mvutano katika eneo, ambapo mfumo wa ulinzi wa anga wa Jamhuri ya Kiislamu ya  Iran umeweza kukabiliana kwa mafanikio na kitendo hicho cha kichokozi cha utawala wa Kizayuni.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mashambulizi hayo yamesababisha uharibifu mdogo katika baadhi ya maeneo na uchunguzi unaendelea kufanywa kubaini uzito wa tukio hilo.

Kuhusu suala hili, nchi tofauti za dunia zimelaani kitendo hicho ambacho kinakiuka wazi sheria za kimataifa.

Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Malaysia imetoa taarifa kuhusu hujuma hiyo ya utawala wa Kizayuni dhidi ya Iran na kusema, Malaysia inalaani vikali mashambulizi ya utawala wa Kizayuni dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran yaliyotokea alfajiri ya leo (Jumamosi) na kuyaona kuwa ni ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa na tishio kubwa kwa uthabiti wa eneo. Taarifa hiyo imeendelea kusema, kuendelea kwa hatua za kichpkozi za utawala wa Israel kunaweza kuchochea mapigano katika eneo la Asia Magharibi na kuenenza migogoro mikubwa zaidi.

Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Saudi Arabia imetangaza katika taarifa kuwa: ‘Uchokozi wa kijeshi unaoilenga Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni ukiukaji wa kujitawala nchi na sheria za kimataifa na Saudi Arabia inalaani vikali kitendo hicho.’

Wizara ya Mambo ya Nje ya Saudia imeitaka jumuiya ya kimataifa na pande zenye ushawishi na amilifu kutekeleza majukumu na wajibu wao ili kupunguza mivutano na mapigano katika eneo.

Ofisi ya Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Pakistan pia imetoa taarifa ikisema kuwa, mashambulio ya kijeshi ya utawala wa  Israel dhidi ya mamlaka na ardhi ya Iran ni ukiukaji mkubwa wa Hati ya Umoja wa Mataifa na sheria za kimataifa.

Katika taarifa yake, Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Oman pia imelaani vikali kitendo cha kichokozi cha utawala wa Kizayuni dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kukiona kuwa ni ukiukaji wa wazi wa mamlaka ya kujitawala ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na ukiukaji wa sheria za kimataifa.