
Pars Today- Mhadhiri mmoja wa Kiirani ameashiria mashambulizi ya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya raia wa Gaza na Lebanon na kusema kuwa, vyombo vya habari vya Magharibi ni washirika wa mauaji haya ya kimbari.
Kwa mujibu wa Pars Today, Seyed Mohammad Marandi, mhadhiri wa Chuo Kikuu na Mkuu Kitengo cha Lugha ya Kiingereza na Fasihi ya Kitivo cha Utafiti wa Ulimwengu cha Chuo Kikuu cha Tehran, amechapisha picha ya watoto wa Lebanon wakiwa mikononi mwa baba zao katika ujumbe kwenye mtandao wa kijamii wa X na kuandika: Haya ndiyo yale ambayo vyombo vya habari vya Magharibi hupenda kuyaita “shabaha dhidi ya Hizbullah” ili kuhalalisha mashambulizi ya utawala wa Kizayuni katika majengo ya makazi ya raia na minara ya ghorofa kote Lebanon.
Marandi ameongeza kuwa: Vyombo vya habari vya Magharibi ni washirika wa mauaji haya ya kimbari.
Jeshi la utawala haramu wa Israel lilianzisha mashambulizi makubwa katika maeneo ya raia wa Lebanon tangu Septemba 23, 2024, kwa kisingizio cha kukabiliana na Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon, ambayo bado yanaendelea. Hadi sasa, Walebanon wasiopungua 3,452 wameuawa shahidi na wengine karibu 15,000 wamejeruhiwa kufuatia mashambulio hayo.