Radiamali ya Iran kwa azimio la nchi tatu za Ulaya kwa Bodi ya IAEA

Nchi tatu za Ulaya zimewasilisha mswada wa azimio kwa Bodi ya Magavana ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) ambapo zimeituhumu Iran kuwa haiweki wazi shughuli zake za nyuklia.

Seyyed Abbas Araghchi, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika mazungumzo ya simu na Mawaziri wa Mambo ya Nje wa baadhi ya nchi wanachama wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki zikiwemo Brazil, Afrika Kusini, Bangladesh, Algeria, Burkina Faso, Pakistan na Ufaransa, amesema kuwa harakati za baadhi ya nchi wanachama wa Magharibi wa wakala huo ni hatua isiyohalalishwa na ambayo inaweza kuvuruga majukumu ya kiufundi na kitasnia ya wakala huo.

Rasimu ya azimio la Wamagharibi dhidi ya Iran inaashiria maamuzi ya Bodi ya Magavana ya Juni 19, 2020, Juni 8, 2022 na vile vile Novemba 17, 2022, ambayo yanaiomba Iran ishirikiane kikamilifu na IAEA kwa ajili ya kuhakikisha kuwa mpango wake wa nyuklia haukengeuki malengo ya amani ya nishati ya nyuklia.

Baraza la Magavana liliitaka Iran ichukue hatua za haraka kwa ajili ya kutimiza wajibu wake wa kisheria na kuchukua hatua zote zinazohitajika ili kutatua masuala ya kiufundi yaliyosalia. Madai ya nchi za Magharibi kuhusu kukengeuka mpango wa amani wa nyuklia wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran yanatolewa katika hali ambayo wakala wa IAEA imekiri katika ripoti zake nyingi kwamba Iran imetekeleza ahadi zake zote za nyuklia.

Mnamo mwaka 2015, Iran ilikubali kusimamisha kwa muda mpango wake wa nyuklia ili iondolewe vikwazo haramu vya nchi za Magharibi, lakini kujiondoa kwa upande mmoja Marekani katika makubaliano hayo ya JCPOA mnamo 2018 na kuanza kutekeleza tena siasa zake za uhasama wa huko nyuma dhidi ya Tehran, na vile vile kushindwa nchi za Ulaya kutekeleza ahadi zao za nyuklia, kuliipelekea Iran, baada ya mwaka mmoja wa uvunjaji ahadi huo wa Wamagharibi, kuanzaa kupunguza hatua kwa hatua majukumu yake katika mapatano hayo.

Rafael Grossi, Mkurugenzi Mkuu wa IAEA akikagua maendeleo ya nishati ya nyuklia ya Iran, mjini Vienna Austria

Sasa Uingereza, Ufaransa na Ujerumani pamoja na Marekani zinadai kuwa Iran imekiuka makubaliano ya JCPOA na ahadi zake za nyuklia na hivyo kutaka kupitishwa azimio jipya dhidi ya Iran katika Baraza la Magavana.

Kazem Gharibabadi, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje anayeshughulikia Masuala ya Kisheria Kimataifa  ameashiria juhudi za baadhi ya nchi za Magharibi za kutaka kupitisha azimio hilo dhidi ya Iran katika kikao cha Bodi ya Magavana ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki na kusema: “Iran inafadhilisha kuendeleza ushirikiano na Wakala, lakini licha ya  Mkurugenzi Mkuu wa Wakala kusisitiza juu ya ulazima wa kutoharibiwa mazingira haya ya ushirikiano na kufanya mazungumzo mara kadhaa na nchi tatu za Ulaya ili kuzishawishi zijiepushe na suala hilo lakini nchi hizo zimechukua njia tofauti na kujiweka kwenye nafasi ya sekretarieti ya Wakala ambapo sasa zimechukua pozi za kujifanya kuwa wao ni wadai.”

Mwanadiplomasia huyu mwandamizi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameendelea kusema: “Tayari tumesema waziwazi kwamba iwapo azimio hilo litapitishwa, tutatoa jibu madhubuti na la haraka, ambapo Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran liko tayari kutekeleza uamuzi huo bila kupoteza wakati. Hatua hii ya Iran, kwa hakika, ni jibu kwa hatua haribifu za nchi hizi chache na ambazo hazizingatii nia njema ya Iran.”

Bila shaka, hatua isiyo ya kisheria ya nchi tatu za Ulaya dhidi ya Iran itavunjia heshima na kuuondolea itibari wakala huo wa kimataifa wla nishati ya atomiki. Kwa kuzingatia hayo, Seyyed Abbas Araghchi, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika mazungumzo yake ya simu na Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi kadhaa ambazo ni wajumbe wa Bodi ya Magavana ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki amelaani hatua hizo zisizo na tija na zisizokuwa na msingi za nchi tatu za Ulaya na kusema kuwa hatua hizo za kutaka kupitisha zimio dhidi ya Iran zitadhoofisha na kuvuruga tu michakato ya mashirikiano kati ya wakala huo na Iran.