Qatar: Hatutaruhusu ardhi, anga yetu zitumike kushambulia majirani

Waziri Mkuu ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar amesema nchi yake kamwe haitaruhusu Kambi ya Anga ya Al Udeid ambayo ina wanajeshi wa Marekani, Uingereza na Qatar kutumika kufanya mashambulizi dhidi ya nchi za eneo hili la Asia Magharibi.

Kwa mujibu wa mtandao habari wa Al-Jazeera, Mohammed bin Abdulrahman Al Thani, Waziri Mkuu wa Qatar hakutaja nchi yoyote lakini hapo awali, Doha pamoja na Kuwait zilitangaza kuwa hazitakubali Marekani itumie ardhi au anga za nchi hizo za Ghuba ya Uajemi dhidi ya Iran.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu wa Qatar pia amelaani jinai zinazoendelea kufanywa na utawala wa Kizayuni huko Gaza na Lebanon na kusema kuwa, Doha imesimama kidete kwenye msimamo wake kwamba vita dhidi ya Gaza vitamalizika, na umwagaji damu za watu wasio na hatia utakamokeshwa.

Kambi ya Jeshi la Anga ya Al Udeid ya US nchini Qatar

“Kipaumbele cha Qatar nchini Lebanon ni kusimamishwa vita na tumekuwa na mawasiliano ya kina na wanasiasa wa Lebanon katika suala hili,” amesema Abdulrahman Al Thani na kuongeza kuwa, utawala wa Kizayuni unatia vizingiti katika njia ya kukomesha vita.

Kauli ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar imekuja siku chache baada ya Lolwah Al-Khater, Waziri mshauri wa serikali ya Qatar katika masuala ya uhusiano wa kimataifa kuonya kuhusu hatari ya kuzuka vita vikubwa katika kanda nzima ya Asia Magharibi, na akataka mataifa ya Kiislamu yaungane kukomesha jinai za utawala wa Kizayuni unaofanya mauaji ya kizazi huko Palestina na Lebanon.