Qalibaf atoa wito wa kuwekewa vikwazo vya kiuchumi, kukata mishipa ya uhai ya Israel

Spika wa Bunge la Iran amezitaka nchi za Kiislamu kuchukua hatua kwa uratibu na kufanya kazi kwa ajili ya kuweka “vikwazo vya kiuchumi na kukata njia muhimu za uhai wa utawala dhalimu wa Israel.”

Akizungumza mjini Tehran katika mkutano na mabalozi kutoka nchi za Kiislamu jana Jumanne, Mohammad Baqer Qalibaf aliyahimiza mataifa ya Kiislamu kutumia “njia za kimataifa” kulaani uhalifu wa Israel.

“Utawala huu haupaswi kuruhusiwa kutumia rasilimali za mataifa ya Kiislamu kufanya uhalifu dhidi ya ndugu na dada Waislamu”, amesisitiza Spika wa Bunge la Iran.

Amesema: “Nchi za Kiislamu zinapaswa kuchukua hatua kwa uratibu ili kutumia njia nzuri za kimataifa kulaani jinai za utawala wa Kizayuni na kutekeleza usitishaji vita.”

Maelfu ya watoto wa Gaza wameuawa katika mashambulizi ya kinyama ya Israel

Qalibaf ameongeza kuwa, “Tunahitaji kuweka vikwazo vya kiuchumi na kukata njia muhimu za uhai wa utawala ghasibu.”

Qalibaf amesisitiza jukumu la mabalozi hao wa nchi za Kiislamu, na kusema kwamba wanaweza kuzitaka serikali za nchi zao kuwasaidia na kuwaunga mkono watu wanaodhulumiwa huko Gaza na Lebanon.

“Katika wakati huu muhimu, Waislamu na mataifa ya Kiislamu yana jukumu kubwa la kutekeleza,” amesema Spika wa Bunge la Iran.

Vilevile ametahadharisha kuhusu “kunyamaza kimya na kutojali” mbele ya uhalifu unaoendelea kufanywa na utawala katili wa Israel.