Rais Vladimir Pitin wa Russia ameelezea wasiwasi wake kuhusu kuzorota hali ya mambo katika eneo la Asia Magharibi, na kusema kuwa, sababu kuu ya mgogoro wa eneo hilo ni kutokuwepo taifa huru la Palestina.
Rais Putini alisema hayo jana Alkhamisi mwishoni mwa mkutano wa 16 wa BRICS na huku akieleza wasiwasi wake kuhusu kushadidi mizozo katika eneo la Asia Magharibi amesema kuwa Moscow inawasiliana mara kwa mara na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kutafuta njia za kupunguza mivutano katika eneo hilo. Amesisitiza kuwa, sababu kuu ya mgogoro wa Asia Magharibi ni kutokuwepo nchi huru ya Palestina.

Rais Putin amesema: Inawezekana kupunguza mvutano katika eneo la Asia Magharibi kwa kutekeleza maamuzi ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Wakati huo huo vyombo vya habari vya utawala wa Kizayuni vimetangaza kuwa, ujumbe wa ngazi za juu wa Russia umewasili katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na utawala wa Kizayuni ili kujadili uwezekano wa kufikiwa makubaliano ya usitishaji vita na kubadilishana mateka kati ya utawala wa Kizayuni na harakati ya Hamas.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, ujumbe wa Russia umebeba ujumbe kutoka kwa Rais Vladimir Putin kwenda kwa waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu wa kumtaka kumtaka akomeshe jinai zake huko Gaza na Lebanon haraka sana iwezekanavyo.
Ziara ya ujumbe wa Russia katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na utawala wa Kizayuni imefanyika katika hali ambayo ujumbe wa harakati ya Hamas pia umekutana na Mikhail Bogdanov, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia na mwakilishi maalumu wa rais wa nchi hiyo katika masuala ya Asia Magharibi mjini Moscow.