Urusi na Ukraine, zinalaumiana baada ya kushuhudiwa kwa mashambulio ya angaa, yaliyolenga miundo mbinu ya nishati, saa chache baada ya rais Donald Trump na Vladimir Putin kuzungumza kwa simu na kukubaliana, kusitisha mashambulio hayo.
Imechapishwa:
Dakika 1
Matangazo ya kibiashara
Rais Putin alikuwa amekubali kusitisha kwa muda, kushambulia miundo mbinu ya nishati nchini Ukraine, lakini akataa usitishwaji wa vita kwa siku 30 kama ilivyopendekezwa na rais wa Marekani Donald Trump.
Hata hivyo, siku ya Jumatano, Urusi, imeishtulu Ukraine kwa kujaribu kushambulia miundo mbinu yake ya nishati, licha ya makubaliano kati ya Putin na Trump.
Imeripotiwa kuwa, nchi hizo mbili zilishambuliana kwa ndege zisizokuwa na rubani, hata baada ya mazungumzo kati ya Trump na Putin.

Naye rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky ameitaka dunia, kuizuia Urusi kukwamisha jitihada za kumaliza vita, na kumshtumu rais Putin kwa kuagiza jeshi la nchi yake kuendelea kushambulia raia wake na miundo mbinu yake ya nishati.
Wakati hayo yakijiri, Ikulu ya Kremlin, imesema kuwa Urusi na Marekani, zitakubaliana ni lini maafisa wa nchi hizo mbili watakutana tena, kujadili tena namna ya kumaliza vita nchini Ukraine.