
Rais Vladimir Putin wa Russia jana Jumanne, alitia saini amri ya kupanua uwezekano wa nchi yake kutumia silaha za nyuklia, na kusema kuwa Moscow huenda ikafikiria kutumia silaha za nyuklia iwapo itakabiliwa na shambulio la kombora kawaida linaloungwa mkono na nchi inayomiliki silaha za nyuklia.
Kwa mujibu wa mwongozo uliloboreshwa, ambao unabainisha vitisho ambavyo vinaweza kuufanya uongozi wa Russia kufikiria kufanya shambulio la nyuklia, shambulio lolote la makombora ya kawaida, ndege zisizo na rubani au ndege nyingine linaweza kutambuliwa kuwa linakidhi vigezo hivyo.
Mwongozo huo uiosasishwa pia unaeleza kwamba, uvamizi wowote utakaofanywa na nchi mwanachama katika muungano wa kijeshi wa NATO dhidi ya Russia utazingatiwa na Moscow kuwa ni uchokozi wa muungano huo mzima dhidi yake.
Mwongozo huo unasema kwamba, “mojawapo ya mambo yanayohalalisha utumiaji wa silaha za nyuklia ni kurusha makombora ya balestiki dhidi ya Russia.”
Mwongozi huo uliotiwa saini na Putin pia umeashiria hali nyingine ambayo inahalalisha matumizi ya silaha za nyuklia, ambayo ni “kutoa eneo na rasilimali kwa ajili ya kuanzisha mashambulizi dhidi ya Russia.”
Uidhinishaji wa Rais Putin wa kusasishwa Mwongozo wa Nyuklia wa nchi hiyo umesadifiana na kumbukumbu ya siku 1,000 tangu kuanza vita vya Ukraine, na umetolewa baada ya Marekani kutoa mwanga wa kijani kwa Kiev kutumia makombora ya masafa marefu kushambulia maeneo ya kijeshi ndani ya Russia.