Putin aonya kujibu mapigo kwa nchi zinazotoa silaha za kushambulia ardhi ya Russia

Rais Vladimir Russia ameonya kuwa, Moscow inabaki nayo haki yake ya kushambulia vituo vya kijeshi vya nchi zinazoruhusu silaha zao kutumika dhidi ya ardhi ya nchi hiyo.

Putin ametoa onyo hilo katika hotuba ya hadhara aliyotoa jana Alkhamisi, akiahidi jibu madhubuti kwa uchokozi wowote utakaofanywa dhidi ya Russia.

Rais wa Russia amefafanua: “tutaamua sehemu za kulengwa wakati wa majaribio zaidi tutakayoifanyia mifumo yetu mipya ya makombora kulingana na vitisho dhidi ya usalama wa Shirikisho la Russia”.

Ameendelea kusema: “tunaamini kwamba tuna haki ya kutumia silaha zetu dhidi ya vituo vya kijeshi vya nchi hizo ambazo zinaruhusu silaha zao kutumika dhidi ya vituo vyetu.”

Kwa mujibu wa Putin, Marekani imeharibu mfumo wa usalama wa kimataifa na hivyo kuongeza hatari ya mzozo wa kimataifa.

Rais wa Russia amesisitiza kuwa Moscow imekuwa ikipendelea suluhisho la amani na iko tayari kutatua maswala yote yanayozozaniwa, hata hivyo ametoa indhari kwa kusema: “lakini pia tuko tayari kwa matukio yoyote. Msiwe na shaka yoyote, kutakuwa na majibu kila wakati”.

Kwa mujibu wa Putin, jeshi la Ukraine limerusha makombora aina ya Kivuli cha Kimbunga (Storm Shadow) yaliyotengenezwa na Uingereza na HIMARS yaliyotengenezwa Marekani katika maeneo yaliyoko katika mikoa ya Bryansk na Kursk nchini Russia…/