Profesa Shivji, wasomi wataja kinachokwaza maendeleo Afrika

Dar es Salaam. Mwanazuoni mkongwe, Profesa Issa Shivji, amesema miongoni mwa sababu zinazokwamisha maendeleo ya haraka katika mataifa ya Afrika ni kuminywa kwa uhuru wa mijadala ya wanataaluma.

Amesema kuminywa kwa mijadala ya wanazuoni kunazikosesha nchi uelewa wa wapi zinakosea, fikra mbadala na suluhu ya matatizo yake, ndiyo maana zinakosea kwa kujirudia.

Mkwamo wa mijadala ya kitaaluma unathibitishwa na ripoti ya Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (Unesco) ya mwaka 2021, inayoeleza kati ya nchi 17 za Afrika zilizoangaliwa, asilimia 65 hazikuwa na sera zinazoilinda mijadala huru ya kitaaluma.

Sambamba na hiyo, ripoti ya Umoja wa Afrika ya mwaka 2022, ilibaini ukosefu wa uhuru wa kitaaluma unasababisha wahadhiri na watafiti kuhama nchi. Katika kipindi cha 2018–2022, zaidi ya wataalamu 10,000 wa Afrika walihamia Ulaya na Amerika Kaskazini kutokana na mazingira duni ya uhuru wa kisomi.

Utafiti wa Mwenendo wa Uchumi wa Kisiasa Kusaini mwa Afrika mwaka 2023 (SAPES Trust) ulionyesha katika nchi ambazo mijadala ya kisomi inadhibitiwa, uamuzi wa kisera huchukuliwa bila ushahidi wa kisayansi, jambo linaloathiri miradi ya maendeleo.

Kama hiyo haitoshi, Ripoti ya Benki ya Dunia ya mwaka 2023, ilionyesha mazingira ya ukandamizaji wa wasomi yanakatisha tamaa sekta binafsi kushirikiana na vyuo vikuu kwenye tafiti au uvumbuzi. Katika nchi zilizoathirika, uwekezaji wa sekta binafsi katika elimu ya juu ulishuka kwa asilimia 38 kati ya 2018–2022.

Ukiacha hilo, wanazuoni wengine wanasema vipato finyu vya wanazuoni vinawaminya baadhi yao uhuru wa kujadili, wakiishi kwa kutarajia uteuzi au kuingia kwenye siasa kwa sababu ndiko kwenye kipato zaidi, kama anavyoeleza Mtaalamu wa Sheria, Profesa Chris Maina.

Wakati wanazuoni wakiyasema hayo, Spika wa Bunge Dkt. Tulia Ackson amesema Serikali ya Tanzania inaunga mkono uhuru wa kitaaluma na kwamba iko tayari kurekebisha sheria, sera au mazingira yoyote ya kimfumo yanayowazuia wasomi kuwa huru kutoa maoni katika maswala mbalimbali ya kijamii.

Profesa Shivji na wanazuoni wengine wamesema hayo leo, Jumatano, Aprili 30, 2025 walipozungumza na Mwananchi Digital nje ya Ukumbi wa Mkutano wa wanataaluma na wanazuoni unaojadili uhuru wa kitaaluma Afrika ulioandaliwa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Kanseli ya Maendeleo ya Utafiti katika Sayansi za Jamii (Codestro).

“Maendeleo yanaongozwa na dira, itikadi, ufahamu wa hali ilivyo na hali unayotaka. Sasa hayo yote chanzo chake ni mijadala na nafasi nzuri ya kuwa na mijadala huru ni vyuo vikuu, ndiyo kazi yao hasa,” amesema.

Profesa Shivji amesema mwaka 2000 nchini ulianzishwa utaratibu uliowatambua wanazuoni kuwa sehemu ya watumishi wa umma na utaratibu huo umesababisha Serikali iingilie kila hatua ya uendeshaji wa vyuo.

“Sasa kama Serikali inaingilia utapata watu watakaokuwa na ujasiri wa kuzungumza? Na uongozi wa chuo utatakiwa kulinda uhuru wa chuo husika,” amesema.

Amesema kunahitajika kuwepo kamisheni itakayokuwa mwamvuli wa wanataaluma na wawe huru na wasitambuliwe kuwa watumishi wa Serikali.

“Kuwe na kamisheni na wanataaluma wawe na nafasi ya pekee katika jamii, sio wawe watumishi wa Serikali. Wawe na kamisheni yao kabisa iwe katika ngazi ya vyuo,” amesema.

Amesema uhuru wa kitaaluma unahusisha utafiti pia, hivyo kama wanakosea uhuru wa kujadili hata wa kutafiti wataukosa.

Amesisitiza zamani walikuwa wanafanya utafiti baada ya kuhitimu elimu ya juu kisha wanakwenda kujadili kwa pamoja, lakini sasa haifanyiki hivyo.

Hata hivyo, Profesa Shivji amesema mijadala ya wanazuoni kwa sasa nchini inazimwa ingawa sio moja kwa moja, lakini mbinu mbalimbali zinatumika.

“Kuzimwa inazimwa, japo sio moja kwa moja mbinu mbalimbali zinatumika. Kwanini inazimwa waulize wenyewe kwanini mnazima na kwanini hampendi mijadala?” amesema.

Hoja ya kukwama kwa maendeleo ya nchi za Afrika inapigiwa msumari na Profesa Maina aliyesema maendeleo ya nchi hutegemea ukweli unaozungumzwa.

“Kama unazungumza kile ambacho mamlaka inataka, maana yake hapawezi kuwa na mawazo mapya na kwa hiyo hapawezi kuwa na maendeleo,” amesema.

Wanazuoni na uteuzi

Katika maelezo yake, Profesa Maina amesema isivyo bahati baadhi ya wanataaluma wanatarajia uteuzi hivyo inawanyima uhuru wa kuwaambia ukweli wanaohusika na mamlaka za kuteuwa.

Hali iko hivyo, kutokana na kile alichoeleza, kuna manufaa zaidi katika uteuzi kuliko yaliyopo kwenye kuwa mwanataaluma vyuoni.

“Kwa hiyo ndiyo maana unakuta wanataaluma wanakuwa wapole ili wateuliwe na wakati mwingine wanakwenda kugombea ubunge kabisa,” amesema.

Amesema kuna umuhimu wa vyuo kupewa nafasi yake na wanataaluma wawe huru kifedha kama wanataka kufanya tafiti na hata mishahara iwe mizuri.

“Isiwe Profesa unakimbilia ubunge au siasa pengine hata hupendi siasa, lakini unafuata fedha, kuna maslahi huko. Nadhani vyuo vikiwezeshwa, mishahara ikaongezwa na vitendea kazi vikawepo nadhani wanataaluma watakuwa huru,” amesema.

Changamoto ya uhuru wa kitaaluma, amesema inagubika hata masuala ya utafiti kwa kuwa nchi haziwekezi vya kutosha katika utafiti.

Kwa sababu ya hilo, Ofisa kutoka Taasisi ya Utafiti nchini Kenya, George Omondi, amesema watafiti wengi katika Bara la Afrika hutegemea ufadhili kutoka taasisi mbalimbali za nje ambazo wakati mwingine huja na masharti mbalimbali.

Amesema wakati mwingine masharti hayo yanaweza kuwa na athari katika tafiti na kuingilia uhuru wa kitaaluma.

“Inawezekana umeshapata fedha za utafiti ukafanya na kupata matokeo, lakini changamoto ikaja katika kupata fedha kwa ajili ya kuchapisha tafiti hiyo.

“Pia kama chuo hakina fedha kwa ajili ya kuchapisha itakulazimu kurudi kwa wafadhili ili kukupatia wanaweza kuhitaji kuupitia utafiti huo,” amesema.

Katika kuupitia, amesema ndipo wanapofanya marekebisho kwa kuondoa yale wasiyoyataka na kuingiza mambo wenye maslahi nayo.

Kutokana na hilo, amesema tafiti nyingi zinazochapishwa hukosa uhalisia wa mazingira ya nchi husika, badala yake unagusa maslahi ya wafadhili.

“Ili Afrika iendelee ni muhimu kwa tafiti kufanyika, tafiti hizo ziwe huru bila ya kuingiliwa,” amesema.

Amesema tafiti zikifanyika bila ya kuingiliwa kwa uhuru wa kitaaluma itasaidia kupatikana kwa ukweli na hali halisi ilivyo katika masuala mbalimbali ya kijamii.

Ameeleza mikakati itakayowekwa itaendana na uhalisia uliopo na hatimaye kupelekea maendeleo katika nyanja mbalimbali za kijamii.

Msimamo wa Serikali

Awali, akizungumza katika ufunguzi wa mkutano huo jana, Dk Tulia amesema Tanzania inathamini mchango wa wanataaluma na wanazuoni katika maendeleo ya jamii na iko tayari kulinda uhuru wao wa mawazo.

“Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limejipanga kusaidia Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na vyuo vikuu vingine nchini endapo kutakuwa na uhitaji wa mabadiliko ya sera kwa lengo la kuboresha uhuru wao wa mawazo ya kisayansi katika kuchangia uimara wa jamii,” alisema.

“Ikiwa mnahitaji mabadiliko yoyote ya sheria inayokwamisha mawazo yenu au mawasilisho ya mawazo yenu au utafiti wenu, basi tutakuwa tayari kusaidia,” aliahidi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *