
Dar es Salaam. Mwili wa aliyewahi kuwa waziri na mbunge wa Rorya, Profesa Philemon Sarungi (89) utazikwa Jumatatu ya Machi 10, 2025 katika makaburi ya Kondo Kunduchi wilayani Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Profesa Sarungi alifariki dunia jioni ya Jumatano, Machi 5, 2025 nyumbani kwake Oysterbay jijini Dar es Salaam kwa tatizo la moyo.
Akizungumza na waandishi wa habari, nyumbani kwa marehemu, msemaji wa familia, Martin Sarungi amesema ibada ya mazishi ya kumuaga mpendwa huyo itaanzia nyumbani kwa marehemu Oysterbay wilayani Kinondoni jijini hapa.
“Shughuli ya kuagwa mwili wa marehemu zitaanza saa nne asubuhi hapa nyumbani kwake. Uamuzi wa kuzikwa hapa umetokana na kikao cha familia pamoja na wosia wa Profesa Sarungi aliyependa azikwe Dar es Salaam,” amesema.
Martin amesema baada ya kumaliza kumzika Profesa Sarungi wataanza safari ya kwenda mkoani Mara kwa ajili ya mazishi ya ndugu yetu mwingine aliyefariki dunia.
Ndugu anayezungumzwa ni Emmanuel Sarungi (80) ambaye alifikwa na mauti Alhamisi ya Machi 6, 2025 nyumbani kwake jijini Mwanza, baada ya kupata taarifa ya kifo cha kaka yake, Profesa Sarungi.
Mawaziri wanavyomkumbuka
Akimzungumzia Profesa Sarungi, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda amesema kiongozi huyo alifundisha watu wengi na amefahamiana naye wakati akiwa kiongozi wa Serikali ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
“Wakati huo nikiwa kiongozi nilikuwa nakaa kwenye baraza la chuo, makamu mwenyekiti wakati huo akiwa Profesa Sarungi, sasa kulitokea tatizo la mahusiano ya wanafunzi wengine walikamatwa na tukapewa tuhuma za uongo,” amesema.
Kilichofanyika baada ya hapo Profesa Mkenda amesema iliundwa tume ya Profesa Sarungi kuchunguza kilichotokea na alifanya kazi yake na ripoti yake iliwasafisha wanafunzi wote.
Amesema barua walioandikiwa ziliwasafisha na kuitwa Ikulu akisisitiza Profesa Sarungi alikuwa mtu wa haki.
Profesa Mkenda amesema waliendelea kuwasiliana na Profesa Sarungi tangu wakati huo na mwaka 2020 alipogombea ubunge wa Rombo kulitokea msiba mmoja wilayani Rombo na kwenye msiba huo alikuwepo Waziri Mkuu mstaafu John Malecela.
“Katika timu ya Malecela alikuja mtu mmoja akaniambia Profesa Sarungi anaomba kuongea na wewe nikashangaa sana nikaenda nikaonana naye nikamsalimia akaniambia ananifuatilia sana na kunitakia kila la kheri.
“Nilifurahi sana na nikaweka azma nikishamaliza kugombea ningefika kumsalimia nasikitika sana hadi anafariki sikuja kumsalimia,” amesema.
Naye Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Stergomena Tax amesema Profesa Sarungi alikuwa mtu mwema na mcheshi.
Alikuwa mtu mwenye upendo hata alipokuwa nyadhifa mbalimbali aliweka pembeni udaktari wake na kuhudumia watu mbalimbali.
Kifo na historia ya Profesa Sarungi
Profesa Sarungi ambaye kwa mujibu wa familia alisumbuliwa na malaria na kupona amefariki dunia jijini Dar es Salaam Jumatano Machi 5, 2025 saa kumi jioni nyumbani kwake Oysterbay wilayani Kinondoni.
Katika historia yake Profesa Sarungi alikuwa mwalimu, daktari wa upasuaji na mtaalamu wa mifupa, waziri, mbunge na mwanamichezo.
Alizaliwa Machi 23, 1936 huko Tarime, mkoani Mara, wazazi wake ni Sarungi Igogo Yusufu na Amimo (Maria) Sarungi.
Mwaka 1966, Sarungi alipata shahada ya udaktari wa Tiba kutoka Chuo Kikuu cha Tiba, Szeged, Hungary.
Mwaka 1970, alihitimu shahada uzamivu ya upasuaji kutoka Chuo Kikuu cha Tiba, Szeged, Hungary. Sarungi alihitimu Diploma katika Orthopedics/trauma kutoka Chuo Kikuu cha Tiba, Vienna, mwaka 1973.
Pia, mwaka 1975 alihitimu Diploma katika upasuaji wa upandikizaji viungo kutoka Chuo Kikuu cha Shanghai.
Kuanzia mwaka 1971 hadi 1973, Sarungi alifanya kazi kama Mhadhiri wa upasuaji katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Aliwahi kushika nafasi ya Mhadhiri Mkuu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, mwaka 1973-1976.
Pia, Sarungi alifanya kazi kama Profesa Mshiriki katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, mwaka 1977-1979 na kuwa Profesa mwaka 1979, mkuu wa idara mwaka 1977-1984 katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Kuanzia mwaka 1984-1990, Sarungi alifanya kazi kama Mkurugenzi Mkuu katika Kituo cha Tiba cha Muhimbili na katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Pia alikuwa Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu, mwaka 1989-1991.
Kuanzia mwaka 1990-1992, Sarungi alifanya kazi kama Waziri wa Afya, Waziri wa Mawasiliano na Usafirishaji mwaka 1992-1993 na tangu mwaka 1993 amekuwa Waziri wa Elimu na Utamaduni na pia Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.
Pia, Sarungi mwanachama wa CCM tangu mwaka 1971, ni Mjumbe wa Chama cha Madaktari Tanzania na Chama cha Madaktari wa Upasuaji wa Afrika Mashariki.