Dar es Salaam. Shuhuda za huduma za matibabu, hasa za kuwaunganisha mifupa Watanzania mbalimbali, zinamfanya Profesa Philemon Sarungi aendelee kuishi mioyoni mwa watu, wakati leo Jumatatu, Machi 10, 2025, atazikwa katika makazi yake ya milele.
Sambamba na hilo, maono yake yaliyochochea kuanzishwa kwa Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI), imeibua shinikizo la wadau na baadhi ya viongozi kutaka taasisi hiyo ipewe jina lake kumuenzi.
Shinikizo la waombolezaji hao linatokana na salamu mbalimbali walizozitoa wakati wa kuomboleza kifo cha Profesa Sarungi katika Uwanja wa Karimjee, Dar es Salaam.

Veronica Sarungi ambaye ni mjane wa Profesa Philemon Sarungi akiweka shada la maua katika kaburi la mume wake wakati wa maziko yake yaliyofanyika leo Jumatatu Machi, 10, 2025 katika makaburi ya Kinondoni, Dar es Salaam. Picha na Sunday George
Profesa Sarungi alifariki dunia Machi 5, 2025, kwa maradhi ya moyo akiwa na umri wa miaka 89 nyumbani kwake Oysterbay jijini Dar es Salaam.
Mbali na utaalamu wake katika tiba ya mifupa na majeruhi, Profesa Sarungi pia amewahi kuwa Waziri wa Afya, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Waziri wa Elimu, na Mbunge wa Rorya.
Hayo yamejiri leo, Jumatatu Machi 10, 2025, katika viwanja vya Karimjee, Dar es Salaam, zilipotolewa salamu za mwisho kwa mwili wa Profesa Sarungi kabla ya baadaye kuzikwa katika makaburi ya Kondo Kunduchi, Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam.
Miongoni mwa waliotoa shuhuda zinazomkumbuka Profesa Sarungi milele ni Waziri wa zamani wa Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka.
Katika maneno yake, amesema akiwa jeshini kwa mujibu wa sheria baada ya kidato cha sita alipata tatizo katika misuli ya shingo na alilazimika kupelekwa Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Baada ya kufika hospitalini, amesema kwenye chumba cha matibabu aliwakuta madaktari wawili, mmoja akiwa Profesa Sarungi.
Amesema walipomchunguza, Profesa Sarungi akamwambia hajavunjika mfupa wa shingo, bali ana tatizo la msuli ambalo kimsingi limesababishwa muda mrefu.
“Nikakumbuka kwamba kweli niliwahi kuanguka kutoka kwenye mti kwa nguvu kumbe nimeleta shida kwenye misuli,” amesema.
Mara ya pili, amesema alikutana naye baada ya kujifungua mtoto wake wa tatu, akisema alipata shida ya mgongo na marehemu mumewe alikwenda kumtafuta Profesa Sarungi.
“Alimwambia mume wangu kwa utani kwamba huyu mke ameshapooza, huna mke tena hapa, lakini alinitibu na leo hii mnaniona nimesimama hapa,” amesema.
Katika siasa, amesema baada ya kuhitimu elimu ya juu walianzisha baraza huru la wanawake, wakati ambapo Profesa Sarungi akiwa Waziri wa Elimu aliandika barua akiruhusu walimu wa shule za msingi wapewe semina ya haki za wanawake.
“Kwa maisha yangu ya misukosuko ninajua watu original, kwa hiyo huyu ni mtu original, unapopata shida hakimbii anakuja kuuliza imekuwaje.”
“Wakati yamenikuta ya Escrow, watu wananitukana, yeye alikuwa ananifuata ananiuliza, Anna, imekuwaje, usiogope kama hujafanya usiogope,” amesema.
Kumbukumbu alizonazo Profesa Anna zinafanana na za mfanyabiashara Azim Dewji, aliyesema baada ya kuvunjika kwa ajali ya gari akitoka Uwanja wa Ndege, alilazimika kwenda Muhimbili alikokutana na Profesa Sarungi.
Akizungumza kuiwakilisha Klabu ya Simba, ambayo Profesa Sarungi alikuwa shabiki wake, amesema alitibiwa naye baada ya miezi mitatu, na baadaye alipoingia Simba wakakutana tena.
Ameeleza anamkumbuka Profesa Sarungi akiwa mkweli na anayeishi kwa kanuni na alimwambia, pamoja na utaalamu wake, pia yeye ni mpenzi wa Simba.
“Sio viongozi wa sasa wanafichaficha lakini chinichini huku wanakwenda kuvuruga mpira wetu,” amesema, na kusababisha vicheko kutoka kwa waombolezaji.
Dewji amesema anakumbuka kulipotokea ajali ya treni Ihumwa mkoani Dodoma, Profesa Sarungi alikwenda kuweka kambi na kuwatibu majeruhi mbali na kuwa mbunge.
“Sisi ambao tunaomwakilisha Taifa letu kwenye mashindano ya kimataifa Simba, tunajivunia kwamba wabobezi karibu wote ni wanachama wa Simba au mashabiki wa Simba,” amesema.
Amesema sasa hivi majina mengi yanavuma, zamani ilikuwa Profesa Sarungi na sasa ni Profesa Mohamed Janabi (Mkurugenzi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili).
Alichokisema Kimiti
Akizungumza kwa niaba ya wakuu wa mikoa wastaafu, Paul Kimiti amesema Profesa Sarungi amemsaidia katika upasuaji wa mkewe na binti yake aliyevunjika mfupa.

Baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa wakiwa katika viwanja vya Karimjee, Dar es Salaam kwa ajili ya kuaga mwili wa Profesa Philemon Sarungi. Picha na Sunday George
Kuhusu upasuaji wa mkewe, amesema alikuwa na shida kwenye uti wa mgongo na alimwambia ukweli kwamba hangeweza kufanya, na alimpa rufaa ya kwenda India.
“Aliporudi akanambia umeona vifaa walivyomwekea, sisi hatuna, ningemuua mke wako bure,” amesema.
Amesema Profesa Sarungi alimsaidia pia kumfanyia upasuaji binti yake aliyepata tatizo la mifupa miguuni.
Wataka MOI ipewe jina lake
Baada ya simulizi za juhudi zake za kuanzisha MOI kutoka kwa madaktari wenzake, akiwemo Profesa Lawrence Maseru, wadau wamesema ni vema taasisi hiyo ipewe jina lake kumuenzi.
Hilo lilianza kuibuliwa na Mbunge wa Musoma Vijijini, Profesa Sospeter Muhongo, aliyetaka kumuenzi Profesa Sarungi kwa njia hiyo.
Amesema anaacha jukumu la kumuenzi Profesa Sarungi kwa Hospitali ya Muhimbili kuhusu jina lake kutumika MOI.
Amesema iwapo hospitali hiyo itachelewa kufanya hivyo, wakazi wa Mkoa wa Mara, ambako ni asili ya Profesa Sarungi, watafanya namna kuhakikisha wanalienzi jina lake katika moja ya mradi wa hospitali ambao unataka kuwa chuo.
“Tumemsifia na duniani kote inajulikana kwamba ana shule ya sekondari kule kwao, ni rafiki yangu nilishapeleka vitabu kwenye shule yake. Madaktari wa Muhimbili tuwaachie, nyie wote mnataka tumkumbuke, tuwaombe wafanye taratibu, naye ndiye aliyeanzisha MOI, jina lake lisipotee,” amesema.
Profesa Muhongo amesema mara nyingi walikutana kujadili mambo mengi, ikiwemo taaluma, makabila, na aliwahi kumweleza kuwa wao si wajaluo bali ni wasuba.
Baada ya hoja hiyo, Kiongozi mstaafu wa chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe, naye alikazia kwa kutaka muswada upelekwe bungeni kulifanikisha hilo.
Amesema ni muhimu kutekeleza hilo kwa sababu Profesa Sarungi ametoa maisha yake kuhakikisha anamsaidia Watanzania, vema jina lake lienziwe.
Hilo pia, lilipigiwa msumari na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, aliyesema kwa nafasi yake atashinikiza kufanikisha hilo.
Pamoja na kuunga mkono, pia amekosoa utaratibu wa waombolezaji kuja na maoni ya kumuenzi mtu anapofariki, akisema iwapo MOI ingeitwa jina la Profesa Sarungi enzi za uhai wake, angefurahi zaidi.
Alichokisema Jaji Warioba
Waziri Mkuu mstaafu, Joseph Warioba amesema haikuchukua muda kumfahamu Profesa Sarungi muda mchache baada ya kurejea Dar es Salaam akitoka nje kwa masomo.
Katika maisha yake, amesema Profesa Sarungi amekuwa mtaalamu, kiongozi, mwanasiasa, hivyo ni mtu aliyefanya kazi za umma kwa muda mrefu.

Waombolezaji wakiwa wamebeba jeneza lenye mwili wa Profesa Philemon Sarungi katika makaburi ya Kinondoni jijini Dar es Salaam leo. Picha na Sunday George
Amesema Profesa Sarungi ni miongoni mwa viongozi aliofanya nao kazi serikalini na aliendelea kuwa naye hata walipostaafu.
“Unapostaafu, unaacha kutokatoka, labda kutoka ukialikwa mahali, Sarungi hakuwa hivyo, mimi najua kuna wengi ambao Sarungi alikuwa anawatembelea. Mimi ofisi yangu haikuwa mbali na alikokuwa anaishi, haikupita wiki tatu kabla hajapita ofisini tukakaa kuzungumza na wakati wote aliniuliza kuhusu afya yangu,” amesema.
Amesema muda mwingi pia alikuwa akifuatilia maendeleo ya nchi na akiona jambo alimtumia kama kichochoro cha kufika kwa wakubwa.
“Tukizungumza akiona inakwenda hivi ananambia wewe mwenzangu una nafasi kubwa, hebu fanya hivi uwaambie wakubwa,” amesema.
Ingawa walifanya kazi kwa muda mfupi, amesema mara nyingi alimtafuta wakiwa pamoja kwa mazungumzo na hakuona aibu kuomba ushauri akiwa na jambo.
“Nikiwa Waziri Mkuu, Sarungi amekuwa Mkurugenzi wa Muhimbili nadhani kuanzia 1984 hadi 1990 nilipokuwa Waziri Mkuu niliamua kwenda kutembelea Muhimbili, kilikuwa kipindi kigumu sana hatukuwa na rasilimali za kutosha,” amesema.
Licha ya uchache wa rasilimali, amesema kazi zilizofanywa zilikuwa nzuri na hata sehemu za starehe zilijengwa naye akisema wakati mwingine inasaidia mgonjwa atoke nje.
“Unakumbuka mgomo wa wanafunzi wa mwaka 1990, ulikuwa mgomo mgumu sana kushughulikia. Ilibidi tufunge chuo kwa muda lakini kwa shingo upande kwa sababu tulitaka vijana waendelee.
“Nafikiri wakati huo Sarungi ndiye aliyepewa jukumu la kuchunguza mgomo uliotokea na kutoa mapendekezo nini kifanyike na ndio iliyotusaidia kupata uamuzi wa tuendelee namna gani na mafunzo pale chuo kikuu,” amesema.
Amesema Profesa Sarungi alibaki kuwa mwaminifu kwa nchi, mwenye maadili na hakuwa na unafiki, na kwa wengine lugha ya Mara ilikuwa inawababaisha.
“Sisi wa Mara ni watu wa unachokifikiria ndicho unachokisema, alikuwa anaonekana kama mtu mgomvi, lakini hakuwa hivyo,” amesema.
Amesema sifa zake huenda zikasaidia kizazi cha sasa na kinachiokuja, huenda kikawa na juhudi, maarifa, na jitihada kama alizokuwa nazo Profesa Sarungi.
Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku, amesema mara nyingi Profesa Sarungi alimwita faragha kuzungumza masuala kuhusu Taifa na hiyo inaonyesha kuwa alipenda Taifa na Watanzania.
“Humu nadhani wapo watu wa Bukoba, alikuwa akiwaona watu wa Bukoba kwa sababu alipenda sana mila, alikuwa anaangusha utani wa ajabu, aliwatania wanataniana na hakuacha mpaka utakapotoka na utani wake ulikuwa mzuri,” amesema.
Katika familia, amesema alipenda urafiki na muda mrefu alikuwa rafiki wa baba yake na siku moja kulikuwa na ubishi hospitalini kuwa baba huyo akifanyiwa upasuaji angefariki.

Waombolezaji wakiwa katika viwanja vya Karimjee, Dar es Salaam kwa ajili ya kuaga mwili wa Profesa Philemon Sarungi. Picha na Sunday George
“Aliniita pembeni, alinambia Butiku baba tumfanyie upasuaji, wanasema atatoka (atafariki), lakini najua hatafariki, labda kwa mpango wa Mungu, alimfanyia na mtu aliishi,” amesema.
Amesema Profesa Sarungi ndiye aliyekuwa wa kwanza, kuhakikisha Muhimbili inapambwa na maua, wakati huo hayakuwepo hata mawe yanayoonekana sasa.