Profesa Sarungi afariki dunia

Dar es Salaam. Waziri wa zamani na mbunge wa Rorya, Profesa Phelemon Sarungi (89) amefariki dunia jijini Dar es Salaam leo Machi 5, 2025.

Kwa mujibu wa msemaji wa familia ya Chifu Sarungi, Martin Sarungi amethibitishia Mwananchi kuwa Profesa Sarungi amefariki dunia nyumbani kwake Oysterbay leo saa kumi jioni.

Sarungi amesema Profesa Sarungi siku chache zilizopita alikuwa akisumbuliwa na malaria lakini alipona.

“Mzee kama unavyojua alikuwa tayari ana umri mkubwa na siku chache zilizopita alisumbuliwa na malaria lakini alipata nafuu,” amesema.

Amesema msiba upo nyumbani kwa marehemu Oysterbay Mtaa wa Msasani, Dar es salaam.

Sarungi amesema shughuli za mazishi zinasubiri watoto na wajukuu zake ambao wengi wanaishi nje ya nchi na mwili umehifadhiwa Hospitali ya Lugalo.

Awali taarifa ya kifo cha Profesa Sarungi ilitangazwa na binti yake Maria Sarungi ambaye kwenye ukurasa wake wa X aliweka picha ya baba yake na kuandika ‘rest with Angels, daddy’.

Kwa mujibu wa Maria baba yake alizaliwa Machi 23, 1936 na amefariki dunia Machi 5, 2025.

Profesa Sarungi ambaye kitaaluma ni daktari bingwa wa mifupa aliyewahi kushika nafasi mbalimbali za uongozi serikalini, baadaye aliingia kwenye siasa na kuwa mbunge wa jimbo la Rorya mkoani Mara.

Safari yake ya kisiasa, Profesa Sarungi amewahi kuwa Waziri wa Elimu, Waziri wa Afya, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Waziri wa Mawasiliano na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro.

Profesa Sarungi mbali na siasa pia alikuwa mwanamichezo na shabiki na mwanachama wa timu ya Simba. Alipenda kucheza Yoga, kukimbia na mazoezi mengine ya viungo.

Historia yake

Profesa Sarungi alikuwa mwalimu, daktari wa upasuaji na mtaalamu wa mifupa, waziri, mbunge na mwanamichezo.

Alizaliwa Machi 23, 1936 huko Tarime, mkoani Mara, wazazi wake ni Sarungi Igogo Yusufu na Amimo (Maria) Sarungi.

Mwaka 1966, Sarungi alipata shahada ya udaktari wa Tiba kutoka Chuo Kikuu cha Tiba, Szeged, Hungary.

Mwaka 1970, alihitimu shahada uzamivu ya upasuaji kutoka Chuo Kikuu cha Tiba, Szeged, Hungary. Sarungi alihitimu Diploma katika Orthopedics/trauma kutoka Chuo Kikuu cha Tiba, Vienna, mwaka 1973.

Pia, mwaka 1975 alihitimu Diploma katika upasuaji wa upandikizaji viungo kutoka Chuo Kikuu cha Shanghai.

Kuanzia mwaka 1971 hadi 1973, Sarungi alifanya kazi kama Mhadhiri wa upasuaji katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Aliwahi kushika nafasi ya Mhadhiri Mkuu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, mwaka 1973-1976.

Pia, Sarungi alifanya kazi kama Profesa Mshiriki katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, mwaka 1977-1979 na kuwa Profesa mwaka 1979, mkuu wa idara mwaka 1977-1984 katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Kuanzia mwaka 1984-1990, Sarungi alifanya kazi kama Mkurugenzi Mkuu katika Kituo cha Tiba cha Muhimbili na katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Alikuwa pia Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu, mwaka 1989-1991.

Pia, kuanzia mwaka 1990-1992, Sarungi alifanya kazi kama Waziri wa Afya, Waziri wa Mawasiliano na Usafirishaji mwaka 1992-1993 na tangu mwaka 1993 amekuwa Waziri wa Elimu na Utamaduni na pia Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.

Pia, Sarungi mwanachama wa CCM tangu mwaka 1971. Pia, ni Mjumbe wa Chama cha Madaktari Tanzania na Chama cha Madaktari wa Upasuaji wa Afrika Mashariki.