
Dar es Salaam. Jumuiya ya wanataaluma wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) imemuaga aliyekuwa profesa wa mshiriki katika kituo cha taaluma za mawasiliano chuoni hapo marehemu Martha Qorro aliyefariki dunia Aprili 30, 2025.
Profesa Qorro alihudumu chuoni hapo kwa miaka 29 kabla kustaafu mwaka 2012 na kuendelea na ajira ya mkataba hadi mwaka 2023.
Akizungumza katika shughuli hiyo Mkurugenzi wa elimu ya juu, Profesa Peter Msofe amesema Profesa Qorro ameacha utajiri mkubwa wa watu watakaotumika badala yake.
“Profesa Martha Qorro ametuachia utajiri mkubwa wa watu watakaotumika badala yake na watu hao walipitia kwenye mikono yake kiufundishaji.” amesema Profesa Msofe.
Rasi wa Ndaki ya Insia, Dk Mpale Silkiluwasha amesama siku zote UDSM itatambua mchango na maono yaliyobebwa na Profesa Qorro hasa katika eneo la ufundishaji na ujifunzaji pamoja na kupigania lugha ya Kiswahili kuwa lugha ya kufundishia katika ngazi zote za elimu.
Amesema kwa Jumuiya ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, atakumbukwa kama shujaa na mtetezi wa haki ya elimu bora kwa wote, mzalendo katika kuhimiza matumizi ya Kiswahili kama lugha ya kufundishia katika taasisi za elimu.
“Alikuwa msomi na mwanataaluma mbobevu aliyetafiti, kuchapisha na kushauri katika ubora wa
ufundishai na ujifunzaji katika shule za sekondari nchini Tanzania, hasa matumizi ya lugha ya Kiswahili kama lugha ya kufundishia.
“Busara na uzalendo wake vimeacha alama isiyofutika katika historia ya chuo kikuu chetu Itifaki ya heshima za mwisho kwa wadau wa elimu, wanataaluma, wadau wa Kiswahili, ndugu, jamaa, na wanafamilia ya Udsm”.
Miongoni mwa waliodhuria shughuli hiyo ni Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la HakiElimu, Dk John Kalage, ambapo amesema Profesa Qorro alikuwa miongoni mwa waanzilishi wa shirika hilo.
Dk Kalage amesema kuwa, Profesa Qorro ana mchango mkubwa katika elimu ya Tanzania kupitia ufundishaji, utafiti, na uchapishaji wa maandiko mbalimbali ya kitaaluma yanayogusa elimu ya Tanzania. Pia katika eneo la lugha ya kufundishia amesema daima alikinadi Kiswahili kuwa lugha ya kufundishia katika ngazi zote za elimu nchini.
Wakati wa utumishi wake UDSM, Profesa Qorro alishika nyadhifa mbalimbali ikiwemo Mkuu wa Idara ya Lugha za Kigeni na Isimu, Mshauri wa Wanafunzi na Mkurugenzi wa Taasisi ya Confucius.
Pia, aliwahi kuwa mjumbe katika kamati nyingi za kitaaluma na ushauri ikwemo Baraza la Chuo Kikuu cha Dar es Saleani, Mwenyekiti wa Bodi za Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijini, Baraza la Kiswahili la Taifa (Bakita), na Shirika la HakiEllmu.