Profesa Mbarawa: Ufanisi Bandari ya Dar umewaziba midomo

Dar es Salaam. Waziri wa Uchukuzi wa Tanzania, Profesa Makame Mbarawa amesema utendaji wa Kampuni ya DP World katika Bandari ya Dar es Salaam umeleta mabadiliko makubwa hali iliyofanya kupungua kwa maneno yaliyokuwa yakisemwa awali.

Oktoba 22, 2023, Serikali iliingia makubaliano na DP World kupitia mikataba mitatu iliyosainiwa kwa lengo la kuongeza ufanisi katika bandari hiyo kwa miaka 30.

Kabla ya kutia saini mikataba hiyo, Serikali iliingia makubaliano na Serikali ya Dubai kuhusu uwekezaji huo (IGA) ambayo yalikosolewa na wadau mbalimbali. Hata hivyo, Serikali ilisisitiza mkataba huo utakuwa na manufaa makubwa.

Tayari kampuni hiyo iliyoibua mijadala mikali nchini imekwisha kuanza kutoa huduma katika bandari ya Dar es Salaam.

Leo Jumatano, Februari 19, 2025 Waziri Mbarawa ametembelea eneo la ujenzi wa matanki 15 ya kuhifadhia mafuta katika eneo la Kigamboni jijini Dar es Salaam na kugusia ufanisi wa bandarini kwa sasa.

Ujenzi huo umefikia asilimia 14.7 ikiwa ni ongezeko kutoka asilimia 4.5 iliyokuwapo Septemba mwaka jana huku ukigharimu Sh678.76 bilioni.

Profesa Mbarawa amesema takwimu zinaonyesha katika miezi sita ya kwanza ya sekta binafsi ndani ya Bandari mapato yalikusanywa ni takribani Sh440 bilioni ambayo zamani haikuwapo.

Mbali na mapato meli za makasha muda wake wa kusubiri nangani na gatini umepungua na sasa inakaa siku tatu hadi mbili tofauti zamani ilikuwa wiki mbili hadi wiki tatu.

“Kwa upande wa DP World ambao wanafanya kazi katika gati namba 5, 6 na 7 foleni ya meli za kontena kukaa muda mrefu imepungua kwa kiasi kikubwa na imefanya wale waliokuwa wakisema sasa hawasemi tena wamenyamaza, muda utaleta majibu na muda hapa umeleta majibu,” amesema Profesa Mbarawa.

Amesema wanatambua bado kuna changamoto ya kuhudumia mzigo wa kichele huku akisema Serikali inaendelea kuboresha mifumo yake ili hilo liweze kubadilishwa.

Akizungumzia ujenzi wa matanki ya kuhifadhia mafuta unaofanyika amesema kama nchi ilikuwa na changamoto ya eneo la kuhifadhia mafuta awali.

Hali hiyo iliongeza gharama alizokuwa akilipa mtu wakati wa kusubiri kushusha mzigo jambo lililochochea mlaji wa mwisho kuelemewa na bei kubwa ya mafuta.

“Hiyo ilifanya serikali kuja na wazo la kujenga matanki yenye uwezo wa kuhifadhi futi za ujazo 378,000 ambayo sasa yatafanya meli kutumia saa mbili hadi tatu kuoakua mzigo tangu kufika hali itakayofanya mafuta yakiingia sokoni yawe na bei nafuu kutokana na kutokuwapo na tozo za ziada,” amesema Profesa Mbarawa

Akizungumza kwenye hafla hiyo mwaka 2023, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Plasduce Mbossa alibainisha Serikali itatia saini mikataba mitatu na kampuni ya DP World.

Mikataba hiyo ni mkataba wa nchi mwenyeji (HGA), mkataba wa ukodishaji na uendeshaji wa gati 4 – 7, na uendeshaji wa pamoja wa gati 0 – 3 kati ya TPA na DP World kwa shughuli za kibiashara na za kiserikali.

“Mikataba hii haihusishi shughuli zote za uendeshaji wa Bandari ya Dar es Salaam wala bandari nyingine za Tanzania,” amesema Mbossa akiongeza tayari wameanza mchakato wa kumpata mwendeshaji wa gati 8 – 11 ambaye siyo DP World.

Akizungumzia matanki 15 ya kuhifadhia mafuta yanayojengwa, Profesa Mbarawa amesema sita kati yake yatakuwa kwa ajili ya dizeli, matano kwa ajili ya petroli na matatu kwa ajili ya mafuta ya ndege huku moja likiwa kwa ajili ya akiba.

Akielezea asilimia 14 za ujenzi zilizofikiwa sasa, Profesa Mbarawa amesema Kazi iliyofanyika ni kuhakikisha udongo uliokuwapo awali unaondolewa na kuletwa kifusi ambacho kinafanya ardhi kuwa tayari kwa ajili ya kuanza ujenzi wa matanki hayo.

Kufanya hivyo ni kuhakikisha matanki yanakuwa salama hata inapotokea ajali ya aina gani.

“Kwa mtu wa kawaida anaona kazi hii ni rahisi lakini kitaalamu kazi hii ndiyo ya msingi kwa sababu uimara wa matanki yako na kuyafanya yaishi kwa muda mrefu yanategemeana na uimara wa msingi uliokuwapo,” amesema Profesa Mbarawa.

Amesema anaamini hata wakati wa mvua kazi hiyo itaendelea vizuri huku akiwataka TPA kusimamia makubaliano ya mkataba hasa katkka hatua za awali za mkataba.

Amesema kiwango cha ujenzi kilichofikiwa kipo ndani ya kile kilichpo ndani ya mkataba huku akisema anaamini kuwa kazi itaendelea hata mvua inaponyesha.

Alitumia nafasi hiyo kuitaka TPA kusimamia vyema ujenzi huo ili kuhakikisha unafanyika kwa viwango vinavyotakiwa.

Naibu Mkurugenzi wa TPA, amesema maelekezo yaliyotolewa na waziri yamepokelewa na yatasimamiwa.

“Amehimiza tufanye kazi kwa bidii na sisi tutamsimamia mkandarasi kuhakikisha anafanya kazi kwa bidii,” amesema.