
Morogoro. Profesa mbobevu wa kemia kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Ndaki ya Sayansi Asili na Tumizi, Faith Mabiki amesema ipo haja ya kuwashirikisha watoto kwenye matukio ya kisayansi ili kukuza udadisi wao.
Amesema hilo litasaidia kuongeza idadi ya wanafunzi wanaosoma masomo ya sayansi, ambayo watu huamini kuwa ni magumu.
Profesa Mabiki amesema hayo wakati akizungumza na wanafunzi wa kidato cha tano na sita katika Shule ya Sekondari ya Alfagems iliyopo Manispaa ya Morogoro, wakati wa mafunzo maalumu yaliyoandaliwa na wanachama wa Pan African Chemistry Network kwa lengo la kuwahamasisha kupenda masomo ya sayansi, hususan kemia.
Amesema wataalamu wamefanya utafiti, imebainika kuwa kitendo cha kuwahusisha wanafunzi kwenye shughuli mbalimbali na matukio ya kisayansi kunasaidia kuongeza idadi ya wanafunzi wanaopenda kusoma masomo hayo ya sayansi.
“Tupo kwenye shule hii leo kwa kuwa tunaamini kupitia mafunzo ya aina hii kwa vitendo tunayoyafanya mara kwa mara, watoto wetu wataanza kuipenda kemia na wanaweza kuona kuwa masomo ya sayansi si magumu kama inavyodhaniwa,” ameeleza Profesa Mabiki.
Amesema kuwa nchi inahitaji wakemia wengi ili kusaidia kufanya kazi kwenye viwanda mbalimbali ambavyo Serikali inahamasisha wawekezaji kuja kujenga, kwa kuwa bila kufanya hivyo nafasi hizo zitachukuliwa na wageni.
Amewataka wanafunzi hao na wengine nchini kuona nafasi ya kemia kwenye maisha ya kila siku, kwenye kila eneo la maisha, akitolea mfano wingi wa bidhaa zinazoongoza kwa kutumiwa madukani zinazotengenezwa kupitia uchanganyaji wa kemikali mbalimbali na kupata bidhaa pendwa kwa jamii, ikiwemo vinywaji.
Hivyo, amesema mafunzo ya aina hiyo yatasaidia kuzalisha idadi ya wanakemia wengi na kuchangia maendeleo ya taifa.
Kwa upande wake, mratibu wa mafunzo hayo, Mkemia Dk Frank Rwegoshora amesema kuwa mafunzo ya aina hiyo ni muhimu kwa wanafunzi hao ambao wana mapenzi na masomo ya kemia.
“Kwa kweli tumefurahi sisi kama waandaaji lakini pia walimu na zaidi wanafunzi 150 ambao wamejitokeza kwa wingi na kufurahia mafunzo hayo yaliyofanyika kwa nadharia na vitendo, yaliyotolewa na walimu na wabobevu wa kemia kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine, na tunaamini tumezalisha jeshi la wataalamu wa kemia kupitia mafunzo haya,” ameeleza Dk Rwegoshora.
Amesema wamefanikiwa kufikia wanafunzi wa shule hiyo, lakini zipo shule nyingi nchini ambazo zina wanafunzi wenye uwezo mkubwa na mapenzi ya kusoma kemia na kuwa wakemia, lakini wana woga na maneno ya baadhi ya watu kuwa kemia ni ngumu, hivyo wanahitaji kufikiwa na kupewa moyo na kuoneshwa fursa zilizopo ikilinganishwa na masomo mengine.
“Tunatoa shukrani nyingi kwa wafadhili wa mafunzo haya, Pan African Chemistry Network na Royal Society of Chemistry, kwa msaada wao mkubwa katika kufanikisha hamasa hii muhimu kwa wanafunzi wetu na wanasayansi wachanga, ambao wameonesha kufurahi na kuahidi kuchagua masomo ya kemia kwenye masomo yao ya ngazi za juu,” ameeleza Dk Rwegoshora.
Wakieleza furaha yao baada ya mafunzo hayo, baadhi ya wanafunzi hao, akiwemo Maganja Jeremiah, amesema wamefurahi kupewa mafunzo hayo na wataalamu hao, lakini kubwa zaidi, mafunzo hayo yamewaonesha fursa kubwa zilizopo kwenye fani ya kemia pamoja na mchango wa wataalamu wa kemia kwenye maendeleo ya viwanda na uchumi wa taifa.
“Binafsi ninasoma mchepuo wa sayansi, lakini nilikuwa na woga kuhusu suala la maisha baada ya kuhitimu, lakini kwa maelezo na ushahidi uliotolewa na wataalamu hawa kutoka SUA, sina woga tena, na nitachagua kusoma SUA fani hii ili niisaidie nchi yangu,” amesema Maganja.
Mwanafunzi Prosper Rey amesema kupitia mafunzo kwa vitendo wamejifunza vitu vingi walivyokuwa hawavifahamu, na ameahidi kuendelea kuvitumia kwenye maisha yao ya kila siku nyumbani, lakini pia kwenye masomo yao hasa wakati wa mitihani yao ya mwisho.
“Elimu hii itatuwezesha na sisi kuwa mabalozi wazuri wa masomo ya kemia kwa wanafunzi wenzetu ambao wamekuwa na woga wa kusoma kemia kutokana na uvumi uliosambaa miongoni mwa watu kuhusu ugumu wa masomo ya sayansi, hasa kemia,” amesema Rey.