
Dar es Salaam. Kama una ratiba za kunywa soda kila siku, hasa aina ya cola upo kwenye hatari zaidi ya kupata ugonjwa wa kisukari, Profesa Kaushik Ramaiya amesema.
Amesema kwa kawaida binadamu anatakiwa kula vijiko vitano vya sukari kwa siku, ila baadhi ya vyakula vina sukari iliyozidi mfano soda yenye ujazo wa mil 350 ina sukari vijiko 10, juisi hali kadhalika.
Kaushik ambaye ni daktari bingwa mbobezi wa magonjwa ya ndani na kisukari, amesema unywaji wa vinywaji vyenye sukari nyingi na mtindo wa maisha ni sababu ya ongezeko la wagonjwa wanaugua kisukari aina ya pili ‘Type 2 diabetes’.
Wagonjwa wanaotibiwa kisukari wameongezeka katika kliniki nchini kutoka 464,110 mwaka 2019 mpaka kufikia watu 674,399 mwaka 2023 kwa mujibu wa takwimu za Mtuha za Wizara ya Afya.
Akizungumza na Mwananchi katika mahojiano maalumu mapema wiki hii, amesema hali ya maisha inaweza kuchangia mtu kupata kisukari kwa zaidi ya asilimia 40 mpaka 50.
“Kinga ni pamoja na kutoa elimu, watu waelewe aina ya chakula kipi ni bora, kinywaji kipi sahihi kwake. Kuna watu wanaamka na kunywa cola asubuhi, wanalala na cola usiku soda yoyote siyo nzuri kiafya, vinywaji vingi vyenye sukari ya kuongeza ni hatari,” amesema Profesa Kaushik.
Amefafanua licha ya mazoea hayo, unapokunywa asubuhi kabla ya kula au usiku wakati wa kulala hatari huongezeka zaidi na kwamba cola ina athari mara mbili kwanza sukari ya kuongezwa na kafein iliyopo.
Amesema sukari siyo katika soda na juisi za viwandani pekee, bali inatengenezwa na ulaji wa vyakula vyenye mafuta mengi, wanga mwingi huleta sukari mwilini na ikiwa mlaji hafanyi mazoezi: “Unakuta mazoezi hakuna, muda wote umekaa kwenye kompyuta, simu ya mkononi, dukani au kwenye runinga, hakuna mazoezi.”
Amesema kutokana na changamoto ya matibabu kuwa ghali, watu wanapaswa kujikinga na ugonjwa wa kisukari.
“Kitendo kinachotakiwa cha kukinga, inatakiwa jamii ielimishwe ni muhimu sana kuepuka sigara, shisha, pombe na tabia zote hatarishi. Ni muhimu sana kuziangalia hiyo itasaidia kupunguza magonjwa ya kisukari na mengine yasiyoambukiza,” amesema.
Profesa Kaushik amesema ili kuidhibiti sukari mwilini, mtu anatakiwa kujua ni kiasi gani cha wanga anakula, “Kama unatumia sukari na wanga na unafanya mazoezi ya kutosha na uzito wako hauongezeki haitaleta shida, kama hufanyi mazoezi huchomi zile ‘calories’ inavyotakiwa lazima ile sukari itaenda kwenye ini na baadaye unapata kisukari.”
Pamoja na hayo, Kaushik ambaye ni Ofisa Mtendaji Mkuu wa Hospitali ya Shree Hindu Mandal anataja hatua madhubuti ambazo zinatakiwa kufanyika ikiwemo elimu kwa jamii.
“Mtu akiona anapata kiu sana au anaanza kukojoa sana, uzito unapungua, anapata kidonda hakiponi anapaswa kwenda hospitali akaangaliwe, kwani yaweza kuwa dalili za kisukari au matatizo mengine pia,” amesema Profesa Kaushik.