
Dar es Salaam. Mchakato wa uchaguzi wa kumpata Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika, unatarajiwa kufanyika kesho Jumapili Mei 18, 2025 jijini Geneva, Uswisi.
Kikao maalumu cha ana kwa ana cha Kamati ya Kanda ya Afrika kimepangwa kufanyika kesho huko Geneva kwa ajili ya kuteua Mkurugenzi wa Kanda ajaye.
Tayari wawakilishi kutoka mataifa mbalimbali ya barani Afrika, wakiwemo mawaziri wa afya ambao watapiga kura, tayari wamewasili kwa ajili ya mkutano huo.
Uchaguzi huo umeitishwa kwa mara nyingine baada ya kifo cha aliyekuwa mteule wa nafasi hiyo Mtanzania, Dk Faustine Ndugulile, aliyechaguliwa kushika nafasi hiyo Agosti mwaka jana.
Dk Ndugulile alifariki dunia Novemba 27, 2025 wakati akipatiwa matibabu nchini India.
Baada ya kifo chake, uchaguzi ulitangazwa kurudiwa tena na Tanzania ilimpendekeza Mwanasayansi na mtafiti Profesa Mohammed Janabi kugombea nafasi hiyo, uteuzi uliotangazwa na Rais Samia Suluhu Hassan, akieleza kuwa uzoefu wake katika sekta ya afya unamfanya kuwa mgombea mwenye sifa stahiki kwa nafasi hiyo muhimu kimataifa.
Baada ya majina ya wagombea wa awamu ya pili kupelekwa WHO, yalichakatwa na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo, Dk Tedros Adhanom Ghebreyesus.
Machi 14, 2025 Profesa Janabi alitangazwa rasmi kuwa mmoja wa wagombea wanne kwa nafasi hiyo kupitia ukurasa wa mtandao wa Shirika la Afya Duniani (WHO).
Janabi ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), anawania nafasi hiyo akiwa sambamba na wagombea kutoka nchi za Magharibi mwa Afrika.
Orodha ya wagombea mbali na Tanzania, nchi nyingine tatu na wagombea watakaochuana ni pamoja na Dk N’da Konan Michel Yao kutoka Ivory Coast, Dk Dramé Mohammed Lamine kutoka Guinea, na Profesa Mijiyawa Moustafa kutoka Togo.
Mkurugenzi wa Kanda huteuliwa na Bodi ya Utendaji ya WHO baada ya kuteuliwa na Kamati ya Kanda ya WHO ya Afrika. Uteuzi wa Mkurugenzi wa Kanda utakuwa kwa kipindi cha miaka mitano, na anaweza kuteuliwa tena mara moja tu.
Nchi yoyote Mwanachama wa Kanda inaweza kupendekeza mgombea wa wadhifa wa Mkurugenzi wa Kanda. Mkurugenzi wa Kanda huchaguliwa kwa kura ya siri katika kikao cha faragha cha Kamati ya Kanda.
Mchakato ulivyokuwa
Baada ya kutangazwa majina ya wagombea, kama sehemu ya mchakato wa uchaguzi wa Mkurugenzi mpya wa Kanda ya Afrika, mdahalo wa wagombea kunadi sera zao kwa njia ya mtandao ulifanyika kwa mara ya kwanza Aprili 2 mwaka huu.
Mdahalo huo wa mtandaoni, uliokubaliwa na nchi wanachama wa WHO katika Kanda hiyo, ni mojawapo ya hatua zilizochukuliwa ili kuimarisha uwazi wa mchakato wa uchaguzi.
Mdahalo huo uliendeshwa chini ya uenyekiti wa Louise Mapleh Kpoto, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii wa Liberia na Makamu wa Kwanza wa Mwenyekiti wa Kamati ya Kikanda ya WHO kwa Afrika.
Jukwaa hilo lilikuwa muhimu na nafasi kwa wagombea kuelezea uzoefu na ujuzi wao, na kuwasilisha maono yao kuhusu kile wanachotumai kufanikisha wakati wa muhula wao ili kutekeleza majukumu muhimu ya WHO katika Kanda ya Afrika.
Utaratibu uliowekwa wagombea walitoa kila mmoja uwasilishaji wa si zaidi ya dakika 20. Kila nchi mwanachama iliyoshiriki katika jukwaa la mtandao iliweza kuuliza maswali.
Wakati wa mdahalo huo, ndipo Profesa Janabi alitaja maono yake iwapo atachaguliwa, kipaumbele chake itakuwa ni afya kwa wote katika kuhakikisha kila nchi inatenga asilimia 15 ya bajeti yake kushughulikia afya.
Alitaja mapendekezo yake ya vyanzo vya fedha kupitia bima ya afya, ubia kati ya sekta ya umma na binafsi, uwekezaji mseto, ubadilishaji wa madeni kwa afya na kufutwa kwa madeni ya kimataifa.
Kipaumbele cha tatu ni maandalizi ya kukabiliana na dharura za kiafya, ambacho kinajumuisha kuimarisha nguvu kazi ya afya, kuboresha ufuatiliaji wa magonjwa, kuimarisha mifumo ya mwitikio wa haraka, na kukuza ushirikiano wa mipakani.
Katika afya ya mama, mtoto na lishe, alisema Afrika inachangia asilimia 70 ya vifo vya wajawazito na asilimia 56 ya vifo vya watoto chini ya miaka mitano duniani.
Hata hivyo, Tanzania ilipunguza vifo vya wajawazito kwa asilimia 80 kati ya 2015 na 2022, mafanikio yaliyotambuliwa wakati Rais Samia Suluhu Hassan akipokea Tuzo ya Global Goalkeeper kutoka Taasisi ya Gates mwaka 2024.
Profesa Janabi pia aliahidi kupambana na magonjwa ya kuambukiza, yasiyoambukiza na magonjwa yaliyopuuzwa kwa kutekeleza mikakati thabiti ya kudhibiti magonjwa, kukuza maisha yenye afya, na kutambua uhusiano kati ya binadamu, wanyama, mimea na mazingira.
Kipaumbele cha sita ni kupambana na usugu wa vimelea vya dawa (AMR), tatizo linalosababisha vifo milioni 1.2 kila mwaka, huku asilimia 40 ya mataifa ya Afrika yakikosa takwimu za ufuatiliaji. Ameahidi kuanzisha hifadhi data za kikanda kukabiliana na tatizo hilo.
Kipaumbele cha saba ni kuimarisha uwezo wa uzalishaji wa ndani wa bidhaa za afya.
Wasifu wake
Profesa Mohamed Yakub Janabi, daktari bingwa wa magonjwa ya moyo na msomi mashuhuri wa Tanzania, anaendelea kuandika historia katika sekta ya afya.
Kwa sasa, anahudumu kama Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) tangu Oktoba 2022 na pia ni Mshauri wa Rais wa Tanzania kuhusu Afya na Matibabu.
Profesa Janabi ana rekodi ya kitaaluma inayovutia, akiwa amepata elimu kutoka taasisi mbalimbali mashuhuri duniani. Alipata Shahada ya Udaktari wa Tiba (MD) kutoka Chuo Kikuu cha Matibabu cha Kharkiv, Ukraine. Aliendelea na Shahada ya Uzamili katika Shule ya Tiba ya Chuo Kikuu cha Queensland, Australia, chini ya Profesa Ian Riley.
Alihitimu Shahada ya Uzamivu (PhD) katika magonjwa ya moyo na baadaye alifanya mafunzo ya juu ya kitabibu katika Chuo Kikuu cha Osaka, Japan, kupitia ufadhili wa Japan Society for Promotion of Science, chini ya Profesa Yuji Matsuzawa.
Uzoefu wa kitaaluma na kiutawala
Katika sekta ya afya, Profesa Janabi ameonesha weledi mkubwa katika nyadhifa mbalimbali:
– Mkurugenzi Mtendaji wa MNH tangu 2022.
– Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) tangu 2015 hadi 2022, ambapo alihusika katika kuifanya JKCI kuwa moja ya vituo bora vya matibabu ya moyo Afrika Mashariki.
– Daktari Binafsi wa Rais Jakaya Mrisho Kikwete tangu mwaka 2005.
– Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) tangu mwaka 2000.
– Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Tiba cha South Carolina, Marekani, tangu mwaka 2003.
Ushiriki katika tafiti na utawala
Mbali na utawala wa hospitali, Profesa Janabi ni mwanataaluma na mtafiti aliyebobea. Ni Mjumbe wa Baraza la MUHAS, Mjumbe wa Bodi ya JKCI, Taasisi ya Saratani ya Ocean Road na Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA).
Amefanya tafiti mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kuwa Mtafiti Mkuu katika utafiti wa chanjo ya Ukimwi wa TaMoVac kati ya 1998 na 2002. Ameshachapisha zaidi ya makala 83 za kisayansi katika sekta ya afya.
Profesa Janabi ana uwezo wa kuwasiliana katika Kiswahili, Kiingereza, Kirusi na Kijapani, jambo linalomwezesha kushirikiana na wataalamu wa afya duniani. Pia, alihudumu kama Mkurugenzi wa Matibabu wa Madaktari Afrika, shirika la Marekani linaloshirikiana na mifumo ya afya ya Tanzania.