
Dar es Salaam. Kama sehemu ya mchakato wa uchaguzi wa mkurugenzi mpya wa Shirika la Afya Duniani (WHO) wa Kanda ya Afrika, mdahalo wa wagombea kunadi sera kwa njia ya mtandao utafanyika Aprili 2, 2025.
Mdahalo huo utawahusisha wagombea kutoka mataifa manne, Tanzania ikiwakilishwa na Profesa Mohammed Janabi, mkurugenzi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) ambaye pia ni mtafiti, mkufunzi na daktari bingwa mbobezi wa magonjwa ya moyo.
Wagombea wengine ni Dk N’da Konan Michel Yao kutoka Ivory Coast, Dk Dramé Mohammed Lamine kutoka Guinea na Profesa Mijiyawa Moustafa kutoka Togo.
Mdahalo ulioidhinishwa na nchi wanachama wa WHO Kanda ya Afrika ni miongoni mwa hatua za kuongeza uwazi wa mchakato wa uchaguzi.
Kwa mujibu wa tovuti ya WHO, mwenyekiti wa mdahalo huo ni Louise Mapleh Kpoto, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii wa Liberia na Makamu wa kwanza wa Mwenyekiti wa Kamati ya Kikanda ya WHO Afrika.
Kupitia mdahalo huo, wagombea wataeleza uzoefu na ujuzi wao, watawasilisha maono yao kuhusu kile wanachotumai kufanikisha wakati wa muhula wao ili kutekeleza majukumu muhimu ya WHO Kanda ya Afrika.
Katika mdahalo huo, wagombea watapata takribani dakika 20 za kujieleza.
Wawakilishi wa nchi wanachama wanaweza kuuliza maswali iwapo zitapenda kufanya hivyo, isipokuwa nchi wanachama zilizopendekeza mgombea, hazitarajiwi kuuliza maswali kwa mgombea waliyempendekeza.
Mdahalo huo utarushwa moja kwa moja kwa lugha za Kiingereza, Kifaransa na Kireno kwenye mitandao ya kijamii na tovuti ya WHO Kanda ya Afrika.
Uchaguzi huo umeitishwa kwa mara nyingine baada ya kifo cha aliyekuwa mteule wa nafasi hiyo, Dk Faustine Ndugulile kutoka Tanzania.
Dk Ndugulile aliyekuwa mbunge wa Kigamboni, alifariki dunia usiku wa kuamkia Novemba 27, 2024 nchini India alikokuwa akipatiwa matibabu.
Alitarajiwa kuanza kazi rasmi WHO Machi 2025, baada ya kupewa miezi sita ya kujipanga baada ya kuchaguliwa kushika wadhifa huo Agosti 27, 2024.
Alishinda nafasi ya Mkurugenzi wa WHO, Kanda ya Afrika akiwashinda wagombea wengine ambao ni Dk Boureima Hama Sambo wa Niger, Dk N’da Konan Michel Yao (Ivory Coast), Dk Ibrahima Soc’e Fall (Senegal) na Dk Richard Mihigo (Rwanda).
Baada ya nafasi hiyo kubaki wazi, Tanzania ilimpendekeza Profesa Janabi kuwania nafasi hiyo, uteuzi uliotangazwa na Rais Samia Suluhu Hassan, akisema uzoefu wake katika sekta ya afya unamfanya kuwa mgombea mwenye sifa stahiki kwa nafasi hiyo muhimu kimataifa.