Profesa Janabi aeleza shauku, mikakati kutumikia watu bilioni 1.4

Profesa Janabi aeleza shauku, mikakati kutumikia watu bilioni 1.4

Dar es Salaam. Tanzania imeandika historia nyingine katika uongozi wa afya barani Afrika baada ya Profesa Mohamed Janabi kuchaguliwa kuwa Mkurugenzi wa Kanda ya Afrika wa Shirika la Afya Duniani (WHO) akitarajiwa kuongoza na kusimamia shughuli zote za WHO katika nchi 47 wanachama.

Kutoka kuiongoza Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) yenye wafanyakazi 4,000, sasa anakwenda kuhudumia takribani watu bilioni 1.4 wanaoishi barani Afrika, baada ya kuchaguliwa kuwa Mkurugenzi Mteule wa WHO, Kanda ya Afrika.

Janabi ambaye pia ni Mshauri wa Rais wa Tanzania Masuala ya Afya na Tiba, anakabiliwa na jukumu zito, hasa katika wakati huu ambao mataifa makubwa yanajitoa kuweka fedha katika mfuko wa shirika hilo kubwa duniani.

Mkurugenzi wa Kanda ya Afrika wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Profesa Mohamed Janabi akinadi sera zake muda mfupi kabla uchaguzi uliofanyika Jumapili, Mei 18, 2025.

Uchaguzi huo umefanyika jana (juzi) Jumapili, Mei 18, 2025 mbele ya Bodi ya Utendaji ya Shirika la Afya Duniani (WHO) na Kamati ya Kanda ya Afrika katika kikao cha ana kwa ana kilichofanyika jijini Geneva nchini Uswisi.

Uchaguzi huo uliitishwa kwa mara nyingine baada ya kifo cha aliyekuwa mteule wa nafasi hiyo Mtanzania Dk Faustine Ndugulile, aliyechaguliwa kushika nafasi hiyo Agosti 27, 2024, na alifariki dunia Novemba 27, 2024 wakati akipatiwa matibabu nchini India.

Baada ya ushindi huu, jina la Profesa Janabi litathibitishwa na kikao cha 157 cha Bodi ya Utendaji ya WHO, kitakachofanyika kuanzia Mei 28 hadi 29, 2025 huko Geneva.

Kwa mujibu wa utaratibu Janabi atahudumu kwa kipindi cha miaka mitano, lakini anaweza kuteuliwa tena kuhudumu kipindi kingine cha miaka mitano.

Katika mahojiano maalumu aliyoyafanya na Mwananchi leo Mei 19, 2025 Mkurugenzi huyu Mteule wa WHO, amesema atahimiza utafiti na uvumbuzi katika kukamilisha maono yake kufikia mwaka 2030.

Mwandishi: Ulijisikiaje ulipopata taarifa kwamba umeshinda nafasi hii muhimu ya uongozi katika WHO Kanda ya Afrika?

Profesa Janabi: Nilijawa na furaha, heshima na shukurani. Namshukuru sana Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuniamini.  Ushindi huu sio wa kwangu pekee, bali ni wa kila Mtanzania aliyesaidia katika safari hii. Nilihisi pia uzito wa jukumu hili muhimu na umuhimu wa kuwatumikia watu wa Afrika bilioni 1.4 kwa bidii.

Mwandishi: Changamoto kubwa zaidi za kiafya zinazolikumba Bara la Afrika ni zipi, na una mpango gani wa kuzitatua?

Profesa Janabi: Changamoto kubwa ni magonjwa ya kuambukiza, yasiyo ya kuambukiza, ukosefu wa rasilimali za afya, na usawa wa huduma za afya. Mpango wangu ni kuimarisha mifumo ya afya, kuongeza uwekezaji katika huduma za msingi za afya, na kushirikiana na wadau kuhakikisha huduma bora na endelevu.

Mwandishi: Ni funzo gani kuu umejifunza kutokana na janga la Uviko-19 ambalo litakuongoza katika kazi yako?

Profesa Janabi: Funzo kubwa ni umuhimu wa maandalizi na mshikamano wa kimataifa. Tumejifunza kuwa mifumo imara ya afya, uwekezaji katika teknolojia ya afya na mawasiliano mazuri ni muhimu katika kukabiliana na majanga.

Mwandishi: Ni mbinu gani mpya unakusudia kuzileta ili kupambana na magonjwa ya kuambukiza kama malaria, kifua kikuu na Ukimwi?

Profesa Janabi: Nitahimiza utafiti na uvumbuzi, kuboresha upatikanaji wa matibabu, na kuongeza juhudi za kuzuia magonjwa haya kupitia chanjo, elimu, na uimarishaji wa huduma za msingi za afya.

Mwandishi: Ni vipi uzoefu wako kama mtaalamu na kiongozi wa afya nchini utakusaidia katika nafasi hii ya kimataifa?

Profesa Janabi: Uzoefu wangu katika kuboresha huduma za afya nchini Tanzania na ushirikiano wa kimataifa umenipa uelewa wa changamoto na fursa zilizopo barani Afrika. Nitautumia ujuzi huo kuleta suluhisho la vitendo na linaloweza kutekelezeka kwa bara zima.

Mwandishi: Je, kuna mikakati maalumu ya kuhakikisha huduma bora kwa afya ya mama na mtoto?

Profesa Janabi: Nitazingatia kuongeza upatikanaji wa huduma za uzazi, lishe bora, chanjo, na elimu kwa jamii. Pia, nitaleta kampeni za kitaifa na kimataifa kuhakikisha rasilimali zaidi zinaelekezwa kwa makundi haya.

Mwandishi: Kwa Universal Health Coverage (UHC), unaamini WHO inaweza kufanya nini zaidi kusaidia nchi wanachama?

Profesa Janabi: WHO inaweza kusaidia kwa kutoa mwongozo wa sera bora, kuongeza ufadhili wa afya, na kusaidia katika kujenga mifumo endelevu ya afya. Pia, kusaidia nchi wanachama kuongeza uwajibikaji na ufanisi katika usimamizi wa rasilimali.

Mwandishi: Je, Afrika iko tayari kwa mageuzi ya kidijitali katika afya?

Profesa Janabi: Afrika iko tayari lakini inahitaji msaada zaidi. WHO inaweza kusaidia kwa kuwajengea uwezo wataalamu wa afya, kusaidia miundombinu ya kidijitali, na kuhamasisha matumizi ya teknolojia rahisi na salama.

Mwandishi: Una mkakati gani wa kuimarisha ushirikiano na Serikali za nchi wanachama?

Profesa Janabi: Nitahimiza mazungumzo ya wazi na yenye kujenga, kushirikiana katika mipango ya kitaifa, na kuhakikisha kuwa nchi wanachama zinajisikia kuwa sehemu ya maamuzi na utekelezaji wa malengo ya WHO.

Mwandishi: Una ndoto gani kwa sekta ya afya ya Afrika ifikapo mwaka 2030?

Profesa Janabi: Ndoto yangu ni Afrika yenye mifumo imara ya afya, afya bora kwa wote, upatikanaji wa huduma za msingi kwa kila mtu, na jamii zinazostawi bila vizuizi vya magonjwa yanayoweza kuzuilika. Nitahakikisha tunaendelea kuelekea ndoto hii kwa bidii.

Kauli yake ya kwanza baada ya kuchaguliwa, Profesa Janabi alitoa shukurani zake akisema anajivunia na kujisikia mwenye unyenyekevu mkubwa kuchaguliwa kama Mkurugenzi wa Kanda wa Afrika.

Alisema huo ni ushindi wa pamoja kwa jitihada zisizoyumba za bara la Afrika katika kufanikisha afya bora kwa wote.

“Ninazishukuru nchi wanachama kwa kuniamini na kunipa dhamana hii. Afrika ni bara la uvumilivu, ubunifu, na uwezo usio na kikomo. Tunapokabiliana na changamoto zinazoendelea katika sekta ya afya, ahadi yangu ni kushirikiana na wadau wote ili kuimarisha mifumo ya afya, kuendeleza usawa, na kuhakikisha hakuna anayebaki nyuma,” alisema.

Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dk Tedros Adhanom Ghebreyesus alimpongeza akisema, “Hongera zangu za dhati kwa Profesa Janabi. Umeaminika na kupata imani ya nchi wanachama wa kanda hii. Hii ni heshima kubwa, na pia ni wajibu mkubwa sana. Nakuhakikishia msaada wangu pamoja na wa wenzangu walioko Geneva.”

Diplomasia

Sifa ya Tanzania kidiplomasia barani Afrika ni miongoni mwa mambo yaliyochangia ushindi wa Profesa Janabi.

Kipindi cha kampeni iliyochukua takribani miezi mitatu, Mjumbe maalumu wa Rais Samia Suluhu Hassan, Rais mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete alionekana akizunguka katika nchi kadhaa za Afrika kumnadi Profesa Janabi.

Baada ya ushindi, Kikwete alimpongeza kwa ushindi wake wa kishindo kwa kupata kura 32 kati ya 46 zilizopigwa.

Akizungumza leo Jumatatu Mei 19, 2025, wakati wa uzinduzi wa Sera ya Mambo ya Nje ya Mwaka 2001 (Toleo la 2024), Ukumbi wa JNICC Dar es Salaam, Rais Samia Suluhu Hassan amemshukuru Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete kwa kuwa mstari wa mbele na kumpigia kampeni Profesa Mohammed Janabi.

 “Nataka nimshukuru Rais mstaafu (Jakaya Kikwete) nilipomuita kumpa kazi hii ya kuwa meneja wa kampeni kwenye kampeni ya Profesa Janabi angeweza kuniambia nina mambo tele ya kimataifa huko, nina Jakaya Kikwete Foundation, nina hiyo sijui taasisi ya elimu duniani lakini akasema nalibeba na nalifanyia kazi tunashukuru sana.” amesema Rais Samia.

Mhadhiri wa chuo cha diplomasia, Innocent Shoo amesema kwa sababu WHO ni chombo cha UN ambayo ni kubwa kuliko vyote kwenye diplomasia, diplomasia ilitakiwa kuhusika.

Amesema Tanzania ilifanikiwa kushinda kutokana na kampeni iliyofanywa na mwanadiplomasia mkuu ambaye ni Rais Samia Suluhu Hassan.

“Kampeni ile akapewa Rais mstaafu Jakaya Kikwete, akaongoza jopo wakafanya kwenye nchi za Afrika Mashariki EAC walianzia Nairobi, baadaye akaenda nchi zingine kama Burkina Faso kwingineko,” amesema.

Shoo amesema Kikwete alitembea katika balozi zetu zote zilizopo nchi mbalimbali akiwa na Mabalozi wengine kama Hoyce Temu, Balozi Kaganda, na wanadiplomasia wengine na maofisa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje nao walikwenda kufanya kampeni.

Amesema kwa kiasi kikubwa kampeni ilifanywa kuhakikisha Profesa Janabi anashinda na kuipaisha nchi  katika ulimwengu wa diplomasia upande wa afya.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *