Profesa chawa jua huyu ni profedheha

Leo nafyatuka na wasomi, wawe wa kweli au kanjanja. Katika kudurusu maana ya usomi na namna unavyopatikana na kutumika, nimejikuta nikijiuliza maswali lukuki, mojawapo likiwa msomi ni nani, ame, au anafanya nini? Katika darasa la ufyatuaji na ufyatuzi wa leo, nawalenga madaktari, madoktari, maprofesa na maprofedheha. Kwanza, nikiri. Siku hizi kuna madaktari na madoktari wengi tu.

Pia, wapo maprofesa na maprofedheha wengi tu. Hapa madaktari ni wale waliousomea udaktari au kusoma kihalali na kwa kufuata taratibu zote hadi wakafikia kiwango cha shahada ya uzamivu (PhD). Pili, wapo madaktari watabibu ambao huitwa madaktari hata kama hawana PhD. Tatu, wapo madoktari walionunua shahada au kuhonga baadhi ya vyuo uchwara na nyemelezi (Degree or Diploma mills) na kutunukiwa PhD feki nao, kutokana na uzwazwa wakazitumia na kuzitanulia wakati hamna lolote.

Huu kimsingi ni utapeli wa kimaadili wenye madhara kwa jamii. Kwani, unawakatisha tamaa waliosotea au kuwamotisha wanaozitaka kuzinunua bila kutoa jasho kiasi cha kuishi na ujinga wao, lakini mbele ya jamii wakionekana wamebukua wakati siyo. Ni jinai kama nyingine. Tofauti ni kwamba inaviza uwezo wa mafyatu na taasisi zao kupata mafyatu stahiki na wabobezi wakaisaidia kutatua matatizo yao.

Tuje kwenye madoktari. Hawa ni wale wanaojiita au kuitwa daktari bila kusomea, kupewa, au kuipata kwa mchongo. Mfano, ukitaka kujua mhusika ni daktari au doktari, kama anadai amesomea, muulize andiko lake liko wapi. Je, amefanya courseworks kwa muda gani? Kama akishindwa kujibu maswali hayo, hata kama anaitwa au kujiita daktari, jua huyo, kifyatu, ni doktari. Kwa Kimakonde unaweza kusema s/he’s a doctored doctorate au ana udaktari wa mchongo au mizengwe.

Je, utawajuaje? Kama nilivyofyatuka hapo juu, waulize au watake wathibitishe sifa na ubobezi wao. Kama hii ikishindikana kwa kuogopa kugombana au kutoweza kuwafikia, hasa wanene, nenda kwa mheshimika google umuulize.

Leo nitatoa kiungo muhimu cha kuujua ubukuzi na mchango wake katika jamii na taaluma yake. Bonyeza google scholar. Itakupa sehemu ya kuweka jina la mhusika na kila kitu kitafunguka na kufyatuka. Hapa utajiridhisha, in case, unataka kumfyatua.

Haiwezekani fyatu akawa na PhD ya kweli kama yangu, akakosekana kwenye google scholar ambayo ndio uga wa wabukuzi. Ukiona hakuna kitu, jua huyo ni doktari siyo daktari. Kwa maprofesa kadhalika. Kwanza anza na google. Kama hakuna kitu andika jina la chuo anachodai kumtunuku hiyo PhD. Kama ni chuo halali au feki, utajua. Na ukishakipata, angalia kama kimesajiliwa na kina ithibati au ni degree au diploma mills.

Vingi vya vyuo hivi utakuta vinajitambulisha kama vya baadhi ya madhehebu ya dini. Nitonye kuwa wapo maprofesa ambao wamegeuka maprofedheha tokana na kutotumia taaluma zao vizuri. Mfano, profesa anayeomba rushwa iwe ya ngono au njuluku, huyu ni profedheha. Profesa anayedanganywa na kihiyo na kumtii naye ni profedheha. Profesa anayehangaikia tumbo ili aishi ni profedheha. Profesa chawa ni profedheha n.k. Mfano ni daktari mmoja nchini Gambia aliyetuhumiwa na imla wa zamani, Yahya Jammeh kuhadaa dunia kuwa alikuwa amegundua dawa ya kupambana na Ukimwi. Mwingine ni profesa wa kule kwa akina Pedejeee aliyetumiwa na mwizi wa kaya ile Mumbuto Nsesekoko naye kudai alikuwa amegundua dawa kama hiyo.

Mpaka naandika, kuna zaidi ya vyuo uchwara hivi 300 duniani. Vingi vinaweza kukuhadaa kuwa vimesajiliwa ila usajili wake ni feki sawa na leseni za biashara made in Gerezani kwa wale wajanja wa Bongo wanaojua kitu hii.

Je, kwa nini leo nimefyatuka hivi? Msidhani nina wivu na hawa madoktari na maprofedheha. Hapana. Kwanza, nafanya hivi kuwasaidia mafyatu wanaokamia kuitwa madaktari wasifyatuliwe njuluku zao na kujitia aibu bure mbali na kutenda makosa ya jinai. Kimsingi, nafyatua kelele ili mamlaka zetu zianze kufuatilia wahalifu hawa na kuwatia adabu. Wapo makanjanja wengi wanaotumia vyeti feki na kupiga njuluku huku wakizuia mafyatu wenye sifa na uwezo kufanya kazi hizo, hasa za kuajiriwa.

Pili, nafanya hivi ili kuwafumbua maninga muwaenge hawa mawenge lau muwazomee badala ya kuwaabudia. Hawa hawana tofauti na majambazi, matapeli, wala rushwa, hata wezi matajiri ambao ukwasi wao umetokana na jinai. Hata kama wanaishi kwenye mahekalu, wakiendesha ndinga nzito na za bei mbaya au kuwa na vyeo vikubwa, bado ni wahalifu na mafyatu wa kutia aibu unaopaswa kuwadharau kuliko hata manonihino yako.

Huwezi, kwa mfano, kuwa profesa ukakosa kutoa machapisho ya kitaaluma. Huwezi kuwa na PhD wakati huna hata hiyo shahada ya kwanza wala ya pili, vinginevyo utunukiwe ya heshima kama veve iko nene ya kaya fulani.

Marais, kwa mfano, huwa wanatunukiwa kitu hii tokana na nafasi na heshima kwa kaya zao lakini si kwao binafsi. Ndo maana wengi kama vile mzee mchonga alikuwa nazo 23 lakini bado hakujiita wala kukubali kuitwa daktari. Mzee Ruksa, si haba kama jina lake alikuwa nazo, japo hakuwahi kukubali kuitwa daktari. Sana sana alipenda kuitwa shehe kwa vile alikuwa amepiga kitabu kwenye anga hizi mashallah.

Nimalize. Hilo ndilo somo la leo. Tumshukuru Fyatu. Amina.