Na Nora Damian, Mtanzania Digital
Watoto wenye ulemavu na wanaoishi katika mazingira magumu ambao wanaolelewa katika Kituo cha Nazzar Foundation kilichopo Madale jijini Dar es Salaam wamepatiwa misaada mbalimbali kuwezesha
Misaada hiyo ambayo iajumuisha pampasi, sabuni, vyombo vya kufulia nguo na vifaa vya usafi umetolewa na Kampuni ya Nywele ya Prima Afro.
Akikabidhi msaada huo Aprili 4,2025 Afisa Masoko wa Prima Afro, Jackine Mputa, amesema wameguswa kuwasaidia watoto hao kama sehemu ya kurudisha fadhila zao kwa jamii.

“Watoto wanaolelewa katika kituo hiki wana changamoto nyingi hasa kutokana na walivyozaliwa ndiyo maana kama kampuni tuliguswa kuja kuwaona na kuwaletea misaada mbalimbali kama sehemu ya kurudisha fadhila zetu kwa jamii,” amesema Jackline.
Mkurugenzi wa kituo hicho Zahra Ismail, amesema kinahudumia watoto 38 wenye ulemavu wa aina mbalimbali kama vile viungo, akili na usonji pamoja na watoto yatima.
Hata hivyo amesema kituo kinakabiliwa na changamoto mbalimbali hasa mahitaji muhimu ya kibinadamu ya watoto hao pamoja na kodi kwa kuwa nyumba wanayotumia wamepanga.
“Changamoto ni kubwa kwa sababu mzazi anaweza akamleta mtoto halafu asionekane hata mwaka mzima, kwahiyo inabidi tuhangaike huku na kule kuhakikisha watoto wanapata chakula na mahitaji mengine. Tunaomba wadau wengine waguswe kuwahudumia watoto hawa ambao wanahitaji misaada mbalimbali ya kibinadamu,” amesema Zahra.
Mwalimu katika kituo hicho Abdallah Kilenya, amesema watoto hao wamekuwa wakifundishwa kujitegemea wenyewe na elimu ya awali kuwawezesha kujua kusoma, kuandika na kuhesabu na kuwataka wazazi na walezi kutowaficha majumbani.