
Dodoma. Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) amewataka maofisa manunuzi na wakurugenzi watendaji wa halmashauri nchini kutoa taarifa za kampuni ambazo zimeomba tenda na kushindwa kufanya kazi ndani ya siku 28, kwa ajili ya hatua zaidi.
Kauli hiyo imetolewa leo Ijumaa, Februari 7, 2025 na Mkurugenzi Mkuu wa PPRA, Dennis Simba wakati akizungumza na maofisa ununuzi na wakurugenzi wa halmashauri kwenye kikao kazi kuhusu matumizi ya mfumo wa ununuzi kwa njia ya kielektroniki (Nest) jijini Dodoma.
Simba amesema kumekuwa na tabia za baadhi ya kampuni kuomba tenda zinazotangazwa kwenye halmashauri lakini wakishinda wanaingia mitini, hawaonekani kazini, hawajibu barua pepe wala hawapokei simu na hivyo kuiingiza tena halmashauri gharama ya kutafuta mkandarasi mwingine na wakati muda unakuwa umeisha.
“Mkipata changamoto ya aina hiyo wasilianeni na sisi ndani ya siku 28 ili tuifungie kampuni hiyo kufanya kazi hapa nchini na hata kama wamiliki watataka kufungua kampuni nyingine, hawataweza kwa sababu mfumo wa Nest umeunganishwa na taasisi 20 ikiwemo Nida, TRA na Brela. Hivyo hataweza kufanya kazi tena hapa nchini,” amesema Simba.
Mbali na hilo amesema bado kuna changamoto nyingi ambazo bado zinaikumba mamlaka hiyo ikiwemo baadhi ya taasisi kutotumia mfumo wa Nest kufanya ununuzi wa umma kwa mujibu wa sheria.
“Hata hivyo, tunaendelea kutoa elimu na kuchukua hatua za kisheria dhidi ya taasisi zinazokiuka taratibu hizi,” amesema Simba
Amesema mfumo wa Nest umesaidia kuokoa Sh14.94 bilioni kwenye ukaguzi wa Sh2.7 trilion kupitia ufuatiliaji wa michakato ya ununuzi wa umma nchini.
Sheria ya Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa inatoa mamlaka mbalimbali kuhusu kampuni zinazoshindwa kutekeleza kazi kwa mujibu wa mkataba wa manunuzi ya umma.
Kampuni inayoshindwa kutekeleza kazi ipasavyo au kuvunja masharti ya mkataba inaweza kuwekewa marufuku kushiriki zabuni za umma kwa kipindi fulani, kama inavyotakiwa chini ya kifungu cha 62 cha Sheria ya Ununuzi wa Umma na kanuni zake.
Aidha ofisa sheria mwandamizi wa PPRA, Deusdedith Bishweko amesema mfumo wa Nest hauruhusu mtu kuvunja mkataba kiholela bila kufuata taratibu zilizowekwa.
Amesema mifumo ya zamani ilikuwa inamwezesha mtu kuvunja mkataba wakati wowote lakini kwa sasa mkataba hauwezi kuvunjika bila kufuata taratibu zilizowekwa.
“Hata kama mtu anataka kuvunja mkataba ni lazima afuate taratibu zilizopo na kila mtu ajiridhishe kweli kama kuna sababu za msingi za kuvunja mkataba huo ndipo aruhusiwe kuuvunja hata kama mkataba huo utakuwa na thamani ya Sh50,” amesema Bishweko.
Kadhalika amesema mfumo unatambua mabadiliko ya bei za baadhi ya bidhaa madukani, hivyo mkandarasi ataweza kufidiwa gharama zilizozidi kwenye makubaliano ya utekelezaji wa mkataba baada ya wataalamu kujiridhisha na mabadiliko hayo.
Amesema mfumo huo ni rahisi kutumia kwani hata kama mtu yupo safarini na kompyuta mpakato yake, anaweza kuingia kwenye mfumo na kuthibitisha tenda au malipo bila kuwepo ofisini kwa kuwa kila kitu kinafanyika kwenye mtandao.
Mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo, Zubeda Mbaga ameiomba PPRA kupita kwenye halmashauri ambazo hazifanyi vizuri kwenye matumizi ya mfumo ili watoe elimu kwa wataalamu wa ununuzi kwani wengi hawajui jinsi ya kuutumia mfumo huo.
“Kuna wakati huwa tunatangaza tenda hadi mara saba lakini hakuna mtu hata mmoja anayejitokeza kuomba, tunaomba mtusaidie kwenye hili, kwanza sisi watendaji tuujue huu mfumo vizuri kwa sababu huenda kuna mahali tunakosea na ndiyo maana hakuna anayeomba tenda zetu,” amesema Zubeda.