PPP wachakata miradi 84 ikitekeleza sheria ya ubia

Dar es Salaam. Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP) kinatekeleza miradi 84 iliyopo hatua mbalimbali tangu kilipoanza utekelezaji wa sheria namba 103 Aprili, 2024, kwa lengo la kuwa na mikataba yenye thamani kwa miradi husika.

Miongoni mwa miradi hiyo, mradi pekee uliofikia hatua ya uwekezaji ni wa Shirika la Maendeleo la Dar es Salaam (DDC).

Hayo yameelzwa leo Jumatatu Novemba 11, 2024 na kamishna wa kituo hicho, David Kafulila katika mafunzo ya sheria kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala wa Mikoa na Serikali za Mitaa, jijini Dar es Salaam.

Kafulila amesema chini ya mpango wa PPP, wanahitajika kuhamasisha mtaji wa binafsi wa Dola bilioni 9 ili kuwezesha baadhi ya miradi ya ujenzi kuanza.

“Miradi chini ya PPP ipo katika hatua mbalimbali, baadhi ziko kwenye makubaliano, uchunguzi wa kina, tathmini, ununuzi na maelezo ya dhana. Ujenzi wa barabara ya Kibaha hadi Chalinze yenye thamani ya Dola milioni 340 na ujenzi wa barabara za mzunguko zenye thamani ya Dola bilioni moja uko katika hatua nzuri,” amesema.

Kuhusu mradi wa DDC, Kafulila amesema unahusu ujenzi wa jengo la kisasa la kibiashara Kariakoo, moja ya maeneo yenye shughuli nyingi za kibiashara jijini Dar es Salaam.

“Jengo hili litakuwa kitovu cha huduma nyingi kitakachoshughulikia mahitaji mbalimbali ya kibiashara chini ya paa moja, hivyo kuongeza mvuto wa kibiashara wa Kariakoo na kuvutia uwekezaji zaidi,” amesema Kafulila.

Amesema mradi huo unatarajiwa kugharimu Dola milioni 37. Ili miradi ya PPP iwe endelevu, Kafulila amesisitiza kuwa pande zote mbili lazima zizingatie sheria.

Amezungumzia pia mpango wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) kufanya uchunguzi wa kina ili kuwezesha ujenzi wa reli kutoka Kariakoo kupitia Mlimani City hadi Tegeta.

Hata hivyo, amesema tangu sheria ya ubia namba 103 ilipotungwa kumekuwa na changamoto, ikiwemo ya mamlaka za Serikali kutokuwa na utayari wa kuitumia katika kutengeneza mikataba au kufanya uwekezaji.

“Nyingine ni uelewa wa dhana ya ubia kwa mamlaka za Serikali na nyingine ni historia isiyoridhisha kwenye baadhi ya mikataba tuliyopata kuingia na hivyo ikawa inajenga picha hasi kuhusu masuala ya ubia,” amesema.

Pamoja na changamoto hizo, Kafulila amebainisha kuwa mageuzi yaliyofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan tangu alipoingia madarakani, hasa eneo la PPP, yamechangia kuongezeka kwa biashara kutoka Dola bilioni 17 mwaka 2021 hadi Dola bilioni 31 mwaka huu.

“Kiwango cha biashara ya kimataifa ya Tanzania wakati Rais Samia alipochukua madaraka kilikuwa Dola bilioni 17.4, sasa ni Dola bilioni 31, ongezeko la asilimia 84,” amesema.

Akizungumzia mafunzo hayo, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala wa Mikoa na Serikali za Mitaa, Justin Nyamoga amehimiza PPP kuongeza ufanisi ili miradi hiyo iwe na tija zaidi.