Polisi yazuia mazishi wanaodaiwa kunywa pombe yenye sumu

Manyara. Jeshi la Polisi mkoani hapa, limezuia kuzikwa kwa miili ya watu watatu wanaodaiwa kufariki kwa kunywa pombe yenye sumu, hadi uchunguzi wa kitaalamu ukamilike.

Watu hao Madai Amsi ‘Samweli’ (42), Hao Bado (59) na Nada Yaho ‘Paulina’ (43) wakazi wa Kijiji cha Bashnet wilayani Babati mkoani Manyara walifariki dunia Januari 31, 2025 kwa nyakati tofauti huku wakidaiwa vifo vyao kusababishwa na kunywa pombe yenye sumu.

Akizungumzia tukio hilo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara, Ahmed Makarani amesema kuwa bado vifo hivyo vina utata wa chanzo halisi, hivyo wamezuia kwanza isizikwe ili kukamilisha taratibu za kiuchunguzi wa kitaalamu kwa ajili ya hatua za kisheria.

“Watu hao wanadaiwa wamefariki Januari 31, 2025 kwa kunywa pombe yenye sumu, lakini hatuwezi kuwa na uhakika labda walikunywa kuzidisha kiwango chao au kunywa pombe kali bila kula au vyovyote ndio maana tumezuia na imehifadhiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Babati kwa taratibu za uchunguzi wa kitaalamu,” amesema.

Amesema kuwa kwa kushirikiana na madaktari wabobezi watafanya uchunguzi mkubwa hadi kwenye mapafu ili kujiridhisha na taarifa watakazozitoa, hivyo kuwataka wananchi kuwa watulivu wakati kazi inaendelea.

“Uchunguzi huu ni ule mkubwa, maana tunataka kutoa hadi mapafu ambayo huwa yanahifadhi sumu kujua kama sumu ipo au walilewa zaidi,” amesema.

Mkuu wa Wilaya ya Babati, Emmanuela Kaganda amesema kuwa Serikali haitasita kuchukua hatua kali za kisheria kwa watakaobainika kuwa chanzo cha mauaji hayo.

Awali wakizungumza nyumbani kwao, mke wa marehemu Samweli, (Veronika Daniel) amesema siku ya tukio mumewe alitoka kwenda kunywa pombe kabla ya kurudi usiku na kulala.

“Asubuhi mimi niliamka kwenda shambani na niliporudi mchana ndio nikashangaa kumkuta mume wangu amelala akidai anaumwa sana tumbo na kichwa, nilimpa maji nikimtaka apumzike lakini baadaye kidogo alianza kutapika mfululizo kabla ya kulegea.

“Tulipoona hivyo tulimchukua na kumpeleka Hospitali ya Bashnet na kutundikiwa dripu za maji lakini kwa bahati mbaya haikuchukua muda mrefu alifariki dunia.”

Mwenyekiti wa maafa katika kijiji cha Bashnet, Samweli Manda amesema kuwa wamepata taarifa za vifo na kuiomba Serikali kuchukua hatua za haraka kuchunguza tukio hilo.

Amesema kuwa siku ya tukio alipata taarifa za kuzidiwa kwa Paulina (Nada) kwa madai kuwa saa chache zilipopita alikunywa pombe, wakati wanafanya taratibu za kumuwahisha hospitali alifariki.

“Watu walimpeleka mochwari alfajiri hiyo na kufanya taratibu zote za kuhifadhi mwili na kurudi nyumbani lakini wakakutana na taarifa zingine kuwa kuna mzee (Hao) amezidiwa aliyekuwa anakunywa na marehemu jana.

“Naye alipelekwa kituo cha afya Bashnet kwa machela maana hali ilikuwa mbaya na kutundikiwa dripu lakini saa saba mchana alifariki,” amesema Manda.

Amesema kuwa wakati wanawaza vifo hivyo, ndiyo walipata taarifa za Madai (Samweli) naye amefariki akipatiwa matibabu.

“Hapo ndio vichwa vikaanza kuuma watu wakiwaza ni nini, tukapata taarifa wote walikuwa wanakunywa pombe pamoja, tukaanza kutilia shaka pombe hiyo,” amesema.

“Tunaomba Serikali ichunguze kwa kina inawezekana pombe hiyo ilikuwa na sumu iliyosababisha vifo vya wenzetu, maana kila siku wanakunywa iweje leo wafe tena kwa wakati mmoja na dalili moja?” amesema.

Naye mjumbe wa serikali ya kijiji cha Bashnet, Agripina Tango amesema kuwa unywaji wa pombe katika eneo hilo imekuwa kero kubwa, hasa wafanyabiashara kusambaza kileo hicho kwenye majumba ya watu asubuhi na kusababisha baadhi kuwa waraibu.

“Serikali tunaomba iingilie kati swala hili maana si jambo la kwanza watu kuzidiwa na kilevi, wengi wamekuwa waraibu wa pombe zinazotembezwa mitaani asubuhi kila kukicha na kusababisha nguvu kazi ya Taifa kupotea. Wanaotumia pombe hizi wengi ni vijana na wazee wanaotegemewa na familia,” amesema Tango.