Polisi yatoa angalizo Idd, hakikisho la usalama

Dar/mikoani. Wakati waumini wa Kiislamu wakitarajia kusherehekea sikukuu ya Idd el Fitr, Jeshi la Polisi limetoa hakikisho la usalama huku likiwaonya madereva na watumiaji wengine wa vyombo vya moto wasiozingatia sheria za usalama barabarani kuwa litawachukua hatua kali.

Waumini wa Kiislamu nchini na duniani kila mwaka husherehekea sikukuu ya Idd el Fitr baada ya mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani ambapo hutekeleza ibada hiyo kufunga takriban siku 30 au 29 kulingana na mwandamo wa mwezi.

Makamanda wa Polisi katika mikoa mbalimbali pamoja na Msemaji wa Jeshi hilo, David Misime wametoa taarifa za kiusalama kuelekea sikukuu hiyo ya Idd ambayo inaweza kuadhimishwa kesho Jumatatu au keshokutwa Jumanne.

Taarifa ya Misime imesema Jeshi la Polisi katika mikoa yote litaendelea kuimarisha usalama katika nyumba za ibada na maeneo yote ambayo yatakuwa na mikusanyiko mikubwa ya watu, na wamiliki wa kumbi za starehe wanakumbushwa kuzingatia maelekezo ya kiusalama na taratibu walizopewa wakati walipopatiwa vibali vya kuendesha kumbi hizo.

Aidha, kila mmoja ajiepushe na vitendo vinavyoweza kuhatarisha usalama wa maisha na mali kama vile kuacha nyumba bila waangalizi, kunywa pombe kupita kiasi, kuruhusu vijana na watoto walio chini ya uangalizi wa wazazi kwenda katika nyumba za starehe au maeneo yanayoweza kuhatarisha usalama na utu wao.

Misime amesema vilevile madereva wajiepusha kuendesha vyombo vya moto bila kufuata sheria za usalama barabarani ikiwa kuendesha huku wamelewa, mwendo kasi na kujaza abiria kupita kiasi.

“Jeshi la Polisi linatoa wito kwa wananchi wote pale watakapoona viashiria au kumtilia mtu mashaka kuwa ni mhalifu wasisite kutoa taarifa mapema katika vyombo vya ulinzi na usalama, pamoja na viongozi wa Serikali waliopo karibu ili hatua ziweze kuchukuliwa mapema,” amesema Misime.

Naye Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro amesema: “Polisi Dar es Salaam imeimarisha usalama maeneo mbalimbali ikiwepo fukwe za bahari.”

Amesema jeshi halitasita kuchukua hatua za kisheria iwe kwa dalili au vitendo vitakavyoashiria uvunjifu wa amani au makosa ya usalama barabarani.

Muliro amesema hawatasita kuwachukulia hatua madereva wanaotumia vyombo vya moto kwa kupuuza sheria za usalama barabarani na kuwa chanzo cha ajali na kusababisha vifo au majeruhi kwa watu mbalimbali.

Pia, ametoa wito kwa wazazi na walezi kutowaacha watoto wadogo kwenda kwenye kumbi za starehe na maeneo mbalimbali peke yao, kwani kufanya hivyo kunaweza kusababisha kupotea, kupata ajali au kufanyiwa vitendo visivyofaa na kudhurika kiafya.

Kuhusu usalama kwa kipindi cha mfungo amesema hali imekuwa salama kwa kipindi cha Ramadhan ambacho kinamalizika pamoja na Kwaresma ambayo inaendelea.

“Kipindi cha mfungo hali imekuwa shwari kabisa na hii kwa sababu ya watu kuwa kwenye mfungo wa Ramadhani na Kwaresma tunatamani kungekuwa na vipindi hivi kwa miezi mitatu,” amesema Muliro.

Naye Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Almachius Mchunguzi amesema hatua mbalimbali zimewekwa ili kubaini, kuthibiti na kutanzua matukio ya uhalifu katika kipindi hiki cha sikukuu.

Amesema jeshi hilo litaimarisha ulinzi katika maeneo yote ya Mkoa wa Tanga, ili kuhakikisha wananchi wanasherehekea Idd kwa usalama na amani, bila kuhofia usalama wao.

Imeandikwa na Devotha Kihwelo (Dar), Rajabu Athumani (Tanga)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *