Polisi yashutumiwa kushikiliwa Toyota Probox Kagera, RPC ajibu

Bukoba. Wakati Robert Razalo, mkazi wa Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera, akisimulia anayopitia baada ya gari lake aina ya Toyota Probox kushikiliwa kituo cha polisi likidaiwa kuwa la wizi,  jeshi hilo limesema linafanyia kazi malalamiko ya mwananchi huyo na kisha lilitoa taarifa kwa umma.

Razalo, kupitia ujumbe kwenye mitandao ya kijamii na baadaye katika mazungumzo na Mwananchi, amesema gari hilo linashikiliwa na polisi, huku mali nyingine ikiwemo nyumba ziko hatarini kupigwa mnada.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Brasius Chatanda, akizungumza na Mwananchi leo Jumatano, Machi 26, 2025, amesema ujumbe unaoonekana kwenye mitandao ya kijamii ukihusisha gari hilo kung’ang’aniwa kituo cha polisi unafanyiwa kazi na baada ya hapo litatoa taarifa kamili.

“Tunafanyia kazi ujumbe huo, tukikamilisha tutawaita msiwe na wasiwasi,” amesema Kamanda Chatanda.

Gari lake aina ya Toyota Probox linalosambazwa kwenye mitandao ya kijamii likidaiwa kuwa la wizi.

Razalo akizungumza na Mwananchi amesema gari hilo alinunua kwa mtu (jina linahifadhiwa kwa sasa) mkazi wa mkoani Mwanza mwaka 2022.

Amedai mwaka jana aliliuza gari hilo na mnunuzi aliendelea kulitumia wakati akifanya taratibu za kuhamisha umiliki.

Razalo amedai Oktoba 27, 2024 alipigiwa simu na Mkuu wa Upelelezi wa Polisi Mkoa (RCO) wa Kagera akimtaka afike ofisini kwake, alipokwenda kituoni aliambiwa gari alilouza lilikuwa la wizi na akatakiwa aeleze alivyolipata.

Kwa mujibu wa Razalo, alieleza alikolinunua na baada ya uchunguzi ilibainika halikuwa la wizi lakini polisi wameendelea kuling’ang’ania.

“Kinachoniumiza ni kwamba, napitia yote haya wakati RCO alishasema gari kulingana na uchunguzi lilikamatwa kimakosa na aliyedai kuibiwa gari alishafika kituoni akasema gari si hilo, lakini bado wamekataa kuliachia. Matokeo yake gari la jirani yangu limechukuliwa na nyumba ya familia inataka kupigwa mnada, naumia sana,” amedai.

Razalo aliyejitambulisha kuwa ni dereva wa taasisi moja ya umma mkoani Kagera, amesema mpaka sasa hakuna hatua zinazoendelea kuchukuliwa kuhusu suala hilo, isipokuwa jana Machi 25, 2025 alipigiwa simu kutoka kituo cha polisi akitakiwa apeleke kadi ya gari na mkataba wa mauzo.

Nyumba ya Robert Razalo mkazi wa manispaa ya Bukoba ikiwa imechapishwa maandishi mekundu ikisomeka kukamatwa kwa kibali cha Mahakama.

Akizungumzia ujumbe uliosambaa kwenye mitandao ya kijamii amesema:

“Nilisambaza ujumbe baada ya kukosa msaada kwa njia yoyote kutoka Jeshi la Polisi. Niliyemuuzia gari alinishtaki mahakamani akidai nimpatie lingine au nimrudishie pesa na mimi sina uwezo.”

Amesema: “Mali zangu zimezuiwa, kwa mujibu wa machapisho ya ujumbe kwenye ukuta wa nyumba yangu unadai imekamatwa kihalali kwa kibali cha mahakama.”

Amedai ameshawatumia ujumbe kwa njia ya simu viongozi wa mkoa wa Kagera, wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa na Wizara ya Mambo ya Ndani kuhusu suala hilo.

Ujumbe mtandaoni

Katika ujumbe uliosambaa kwenye mitandao ya kijamii, Razalo amedai baada ya gari kushikiliwa kituoni yeye aliachiwa kwa dhamana.

Amedai alipowasiliana na aliyemuuzia gari alimweleza yeye (muuzaji) ndiye mmiliki wa kwanza alilinunua likiwa jipya.

“Nikatarajia kesi itafunguliwa mahakamani ili tutoe ushahidi. Lakini kesi haikufunguliwa. Nikaomba Polisi watuonyeshe mlalamikaji anayedai kuibiwa gari lakini hatukuonyeshwa.

“Nilipofuatilia sana nikaambiwa mtu aliyedai kuibiwa gari alifika akasema gari siyo lenyewe. Basi nikaomba wanirudishie gari langu wakasema upelelezi bado unaendelea,” amedai Razalo.

Amedai aliyemuuzia gari alifungua kesi ya madai, mahakama ikataka amlipe gari lingine au amrudishie fedha yake.

“Sikuwa na uwezo wa kumpa gari lingine wala kumrudishia pesa. Akarudi mahakamani kukazia hukumu na kuomba kukamata mali zangu. Mahakama ikampa kibali.

“Wiki mbili baadaye, akaja na dalali wa mahakama hawakukuta mtu nyumbani. Wakavunja geti na kwenye parking (maegesho) wakakuta gari la jirani yangu. Huwa anapaki kwangu akisafiri. Wakalibeba kwa kreni na kuondoka nayo. Kisha wakachora nyumba kwa maandishi makubwa kwamba inauzwa,” amedai na kuongeza:

“Kwa nini RCO anagang’ania gari ambalo halina kosa? Nawaza nitamlipa nini jirani yangu? Nawaza nyumba ikipigwa mnada familia yangu itaishi wapi? Napitia yote haya bila kosa.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *