
Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema mwenyekiti wa chama hicho, Tundu Lissu anayeshikiliwa na polisi mkoani Ruvuma yupo njiani kusafirishwa kwenda jijini Dar es Salaam.
Lissu anayedaiwa kushikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani Ruvuma jana Jumatano Aprili 9, 2025 muda mchache baada ya kumaliza kuhutubia mkutano wa hadhara uliofanyika mjini Mbinga mkoani Ruvuma.
Wakati Lissu akidaiwa kuendelea kushikiliwa na polisi, huku wenzake watatu wakiwemo walinzi wake na kada mmoja wa chama hicho, Shija Shebeshi wameachiwa huru.
Akizungumza na Mwananchi leo Alhamisi Aprili 10, 2025 Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi wa Chadema, Brenda Rupia amesema safari ya Lissu kusafirishwa kupelekwa jijini Dar es Salaam ilianza jana jioni baada ya kukamatwa na kupelekwa kituoni.
“Mwenyekiti (Tundu Lissu) yupo njiani kueleka Dar es Salaam, Songea alishatoka tangu jana jioni, bado sijajua kama amefika au la… sasa hivi tunaelekea Songea mjini kutakuwa na mkutano na wanahabari saa tano asubuhi atazungumza Makamu Mwenyekiti Bara (John Heche.
“Tukimaliza mkutano na wanahabari tutaendelea na ratiba za mkutano wa hadhara wa kuhitimisha siku sita za ziara katika mikao ya Lindi, Mtwara na Ruvuma kunadi No Reforms, No Election,” amesema Rupia.
Hata hivyo, hadi sasa bado haijafahamika chanzo cha Lissu kushikiliwa na Polisi, ingawa jana Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Marco Chilya aliliambia Mwananchi yupo katika ufuatiliaji kuthibitisha kuwepo kwa taarifa hizo.
“Na mimi ndio nafuatilia hiyo taarifa, bado sijaipata rasmi. Kukiwa na taarifa kamili tutaitoa kesho (leo),”amesema Kamanda Chilya alipoulizwa na Mwananchi Digital kwa njia ya simu.
Katika purukushani za kumkata Lissu, polisi walilazimika kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya wananchi waliokuwa wanazuia utekelezaji wa majukumu yao.
Jitihada za Mwananchi kumpata Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Marco Chilya au Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime zinaendelea kwani simu zao za mkononi zinaita pasi na kupokelewa.
Endelea kufuatilia Mwananchi