
Dar es Salaam. Baada ya video iliyosambaa mitandaoni kuonesha mabinti wanaodaiwa kuwa wanafunzi wa vyuo wakimpiga na kumdhalilisha kwa maneno mwenzao, Jeshi la Polisi, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limesema linafuatilia tukio hilo.
Katika video hiyo iliyoanza kusambaa usiku wa kuamkia jana Jumapili ya Pasaka, Aprili 20, 2025 ameonekana msichana ambaye jina lake bado halijatambulika akidhalilishwa, kupigwa na wahusika wanaodaiwa kuwa ni wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
Video hizo zimeibua mijadala mitandaoni jambo lililomfanya Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dk Dorothy Gwajima kuingilia kati suala hilo akitaka hatua zichukuliwe dhidi ya wahusika.
Waziri Gwajima alisema anawasiliana na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda na Waziri wa Mambo ya Ndani, Innocent Bashungwa kwa hatua zaidi.
Tayari UDSM na Chuo Kikuu cha Ardhi (ARU), wametoa taarifa za kulaani tukio hilo huku Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam Jumanne Muliro akizungumza na Mwananchi leo Jumatatu, Aprili 21, 2025, amesema: “Tunafuatilia.”
Jana, katika taarifa aliyoitoa kwa umma, Waziri Gwajima alisema ameshawasiliana na mwathirika na kumuunganisha na huduma za ustawi wa jamii, msaada wa kisaikolojia na huduma za Dawati la Jinsia Polisi ili apate msaada wa kisheria ili haki itendeke.
Alisema anawasiliana na wakuu wa vyuo husika kupitia madawati ya jinsia kwenye vyuo husika ili hatua za nidhamu zichukuliwe.
“Usiku wa kuamkia Jumapili ya Pasaka, Aprili 20, 2025 nilipokea tags nyingi kupitia mtandao wa Instagram wakinitumia video kadhaa zinazoonesha mabinti kadhaa wakishirikiana kumdhalilisha binti mwingine kwa maneno na vipigo na mambo mengine mabaya.
“…ambapo, watoa taarifa walidai kuwa, mabinti hao wote ni wanafunzi wa vyuo vikuu viwili tofauti nchini huku wengine wakidaiwa kuwa, wanasoma darasa moja na huyo binti wanayemdhalilisha na kumrekodi.
“Aidha, kwenye mazungumzo yao kama yanavyosikika, inaonekana ni ugomvi wa kumgombania mwanamume anayetajwa kwa jina moja la Mwijaku,” ameandika kwenye ukurasa wake wa X.
Dk Gwajima amesema udhalilishaji waliofanya haukubaliki na unastahili kukemewa kwa nguvu zote, kwa kuwa ni kinyume na sheria.
UDSM, ARU vyalaani vikali
Kufuatia tukio hilo, UDSM na Chuo Kikuu cha Ardhi (ARU) kwa nyakati tofauti vimelaani tukio hilo huku vikiahidi hatua zaidi kwa watakaobainika.
Taarifa ya Aprili 20, 2025 iliyotolewa na Makamu Mkuu wa UDSM, Profesa William Anangisye inalaani kitendo hicho cha udhalilishaji, shambulizi na kudhuriwa kwa msichana huyo.
“Tayari, chuo kinafuatilia taarifa za tukio hilo kwa kina ili kubaini uhalisia wake na utambulisho wa wahusika. Endapo itabainika wahusika ni wanafunzi wa UDSM, hatua kali za kinidhamu zitachukuliwa kwa mujibu ya sheria, taratibu, kanuni na miongozo ya UDSM.
“Aidha, chuo kitashirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama kuhakikisha sheria za nchi zinazingatiwa,” amesema Profesa Anangisye.
Profesa Anangisye amesema, UDSM inapinga aina yoyote ya ukatili, udhalilishaji au uvunjaji wa haki za kibinadamu ndani na nje ya mazingira ya chuo.
Amesema chuo kinatoa rai kwa wanafunzi na jamii kwa jumla kuzingatia sheria, kanuni, taratibu na miongozo ya chuo na maadili ya Kitanzania.
Makamu Mkuu wa ARU, Profesa Evaristo Liwa katika taarifa yake ya jana Jumapili, amesema chuo kinaendelea kufatilia suala hilo.
“Kufuatia taarifa zinazosambaa katika mitandao ya kijamii zikihusisha mwanafunzi anayedaiwa kuwa ni wa ARU, ambaye amefanyiwa vitendo vya ukatili na udhalilishaji, Uongozi wa Chuo Kikuu Ardhi unalaani vitendo hivyo ambavyo ni kinyume na maadili na utu wa Mtanzania.
“ARU inaendelea kufanya ufuatiliaji wa karibu wa suala hilo kwa kushirikiana na mamlaka husika na endapo itadhihirika waliotenda kosa hilo ni wanafunzi wa Chuo Kikuu Ardhi hatua kali za kinidhamu zitachukuliwa dhidi yao kama sheria, taratibu na miongozo ya chuo inavyoelekeza,” amesema.
Wanasaikolojia wanena
Uongozi wa Maofisa Ustawi wa Jamii Ngazi ya Halmashauri 184, umekemea kudhalilishwa na kurekodiwa kwa mwanafunzi huyo.
“Tunawakumbusha vijana na jamii kwa jumla kuwa, kujichukulia sheria mkononi ni kosa kisheria, Kifungu cha 138C cha Kanuni ya Adhabu (Penal Code): Udhalilishaji wa kingono ni kosa la jinai,” inaeleza taarifa iliyotolewa na uongozi huo.
Akizungumzia matukio ya namna hiyo, mwanasaikolojia Dk Neema Mwankina amesema athari inakuwa pande zote kwa mtendewa na mtendaji.
“Kila kinachoonekana kwenye mitandao ya kijamii kinadumu, hivyo kinamuathiri mhusika, kwa hiyo anahitaji kupata huduma ya saikolojia kutokana na maumivu ya hisia aliyoyapata. Anaweza akapata changamoto ya afya ya akili akajichukia yeye na akachukia wengine,” amesema Dk Neema.
Amesema hata waliofanya hicho, wamechukua uamuzi bila uvumilivu, matokeo yake ni kumuumiza mwingine na wao kuumia kama ilivyo sasa.
“Hata upande wa familia inaathari kubwa, ikiwamo kupasuka kwa familia kutokana na matokeo ya tukio kama hilo. Nashauri tu, kwa wanafunzi wa vyuo kabla hujafanya uamuzi jiulize kutakuwa na matokeo gani, kama kutakuwa na athari hasi basi fuata ushauri wenye busara wa kutofanya,” amesema.
Mwanasaikolojia Modester Kimonga amesema athari wanazoweza kupata ni msongo wa mawazo unaoweza kuwasababishia kujidhuru ikiwamo kujiondoa uhai kwa sababu ya fedheha.
“Kujitenga kutokana na kudhalilika, kutopenda kujichanganya na watu hasa familia na marafiki kama hawatapata wanasihi wazuri wanaoweza kuwavusha katika hiyo hali ya maumivu wanayopitia,” amesema.
Kimonga amesema pande zote zinaweza kushuka kiutendaji na kitaaluma kwa sababu ya kufikiria mambo mengi hasi, hivyo kupungua nguvu na ari ya juhudi katika majukumu yao.
“Wanaweza kupata hali ya mshtuko unaoweza kudumu kwa muda mrefu pindi watakapokumbuka maumivu waliyopitia ya kimwili na kihisia,” amesema Kimonga.