
Dar es Salaam. Sakata la mabinti wanaodaiwa wanasoma vyuo wanaotuhumiwa kumdhalilisha mwanafunzi mwenzao wa Chuo Kikuu Cha Ardhi, Magnificat Barnabas Kimario bado pasua kichwa, baada ya Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam kusema bado upelelezi wake haujakamilika.
Tukio hilo lililovuta hisia hasi kwa jamii limemaliza wiki mbili sasa, tangu lilipoibuka mtandaoni usiku wa kuamkia Jumapili ya Pasaka, Aprili 20, 2025 akionekana msichana huyo akidhalilishwa, kupigwa na wanafunzi hao huku wakimtaja muhusika mwingine katika mgogoro huo Mwemba Burton Mwemba, maarufu Mwijaku.
Taarifa iliyotolewa Aprili 24, 2025 na Jeshi hilo lilithibitisha kumkamata na kuwahoji Mwijaku na wanafunzi hao wanne kwa kudaiwa kushiriki katika tukio la kumshambulia mwanafunzi mwenzao.
Wanafunzi hao ni Mary Gervas Matogoro, mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Ryner Ponci Mkwawili, mwanafunzi wa Chuo cha Ardhi, Dar es Salaam, Asha Suleiman Juma, mwanafunzi wa Chuo cha Uhasibu, Dar es Salaam.
Washukiwa hao walijulikana baada ya video hizo kuibua mijadala mitandaoni jambo lililomfanya Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk Dorothy Gwajima Aprili 23, 2025, kuingilia kati na kuagiza hatua zichukuliwe dhidi ya wahusika.
Akizungumza leo Jumanne, Aprili 6, 2025 na Mwananchi lililotaka kujua kinachoendelea juu ya suala hilo, Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro amesema upelelezi wake kwa kuwa unahusisha vyombo vingine vya dola bado unaendelea.
“Uchunguzi wa tukio hilo bado unaendelea, na mjue upelelezi wake haufanywi na Polisi pekee isipokuwa tunashirikiana na mamlaka zingine za dola, tukikamilisha tutatoa taarifa zaidi,” amesema.
Kulingana na Muliro amesema kuna watuhumiwa waliokamatwa na kuhojiwa kuhusiana na tukio hilo na walitajwa lakini Jeshi hilo katika kutekeleza wajibu wake kisheria huwa linashirikiana na mamlaka zingine.
“Tukisema kazi fulani imefanyika ambayo ni ya kisheria tunashirikiana na mamlaka zingine na kuona wao pia wanalitazama vipi jambo lile kuhusiana na ushahidi tulioukusanya kwa kile kilichojitokezea,” amesema.
Muliro amesisitiza taarifa aliyoitoa awali inabakia vilevile na hatua nyingine za kisheria kwa mamlaka zingine zinaendelea kuchukuliwa.