Polisi waweka doria ofisi za Chadema, Muliro atoa sababu

Dar es Salaam. Siku moja baada ya Jeshi la Polisi kuzima maandamano ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) yaliyopangwa kufanyika jijini hapa Septemba 23, 2024, baadhi ya askari wameonekana wakizingira ofisi ya makao makuu ya chama hicho Mikocheni.

Mwandishi wa Mwananchi aliyefika katika ofisi hiyo leo Septemba 24, 2024 ameshuhudia askari hao waliokuwa wamebeba silaha za moto wakichungulia madirisha ya ukuta wa chama hicho, huku wengine wakirandaranda nje ya ofisi.

Katika kudhibiti maandamano hayo makada wa Chadema zaidi ya 50 walikamatwa, akiwamo Mwenyekiti, Freeman Mbowe, Makamu Mwenyekiti (Bara), Tundu Lissu, Mwenyekiti wa Kanda ya Kaskazini, Godbless Leman na makada wengine.

Ofisi ya Makao Makuu ya Chadema iliyopo Mikocheni jijini Dar es Salaam. Picha na Tuzo Mapunda

Alipoulizwa kuhusu uwepo wa askari hao, Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro amesema bado wanaendelea na kuimarisha ulinzi kama walivyofanya jana.

“Tunaimarisha ulinzi tangu jana kwenye zile pointi, muhimu hakuna tukio lolote la kijinai lililotokea wananchi wako salama. Polisi kuzingira ofisi za Chadema na wao tunawalinda kama wananchi wengine wa kawaida maana yake hawakawii kusema wametekwa,” amesema Muliro.

Akizungumzia hali hiyo, mlinzi wa ofisi hiyo, Kopwe Michael amesema hali ya vikosi hivyo kuzingira katika ofisi hiyo ilianza saa 3:00 asubuhi.

“Zilianza kuja Defender tatu zote zilikuwa zimejaza maaskari ndani yake. Baadaye wakashuka na kuanza kuzingira ofisi yetu wengine wakichungulia ndani kupitia madirisha ya ukutani bila kusema jambo gani wanaangalia au wanatafuta,” amesema.

Ndani ya ofisi hiyo makada na maofisa, akiwamo Katibu Mkuu wa chama hicho, John Mnyika na Katibu Mkuu wa Baraza la Wanawake (Bawacha), Catherine Ruge walikuwepo wakiendelea na kazi.

Mbali na hao kulikuwa na makada wengine waliokamatwa jana, akiwamo, Shaban Mabala alisema aliachiwa jana usiku saa nane akiwa na Paulo Shija baada ya kushikiliwa rumande ya Polisi Kati Posta.

“Tulikamatwa jana maeneo ya Mnazi Mmoja mimi na huyu mwenzangu Paulo anayetokea Tabora, tulitaka kuandamana lakini walivyotugundua tukakamatwa walitupeleka Kituo cha Polisi Central na walituachia jana usiku.

“Asubuhi hii tulienda kufuata simu zetu na wametupatia bila masharti ingawa ile jana walitulazimisha kutoa maelezo halafu tusaini tuligoma kufanya hivyo,” amesema Mabala.

Naye, Shida amesema yeye na mwenzake walienda Mnazi Mmoja baada ya kuona Magomeni walikopanga kuanza maandamano hakuna watu.

Spika wa Bunge la Wananchi la chama hicho, Suzan Lyimo akiwa ofisi hapo ameeleza namna alivyonusurika kukamatwa maeneo ya Magomeni.

“Nilikuwa kwenye gari na makada wenzangu tukawa tunasubiri makada wenzetu pale Magomeni lakini baadaye tukaona polisi wanakuja tuliposimana maeneo ya sheli tukaanza kuondoka na polisi wakaanza kutufuatilia hadi maeneo ya Kigogo, tulikojificha,” amesema.