Geita. Jeshi la Polisi nchini limewataka askari polisi wote wa ngazi ya kata nchini kutumia sheria, busara pamoja na mbinu ya ulinzi shirikishi katika kubaini na kuzuia vitendo vya uhalifu kabla ya kutokea katika kipindi cha uchaguzi mkuu ujao.
Akizungumza na askari kata wa Wilaya ya Geita, Aprili 3, 2025 katika kikao cha pamoja kilicholenga kuangalia dhana ya ulinzi shirikishi inavyofanya kazi, Kamishna wa Polisi anayesimamia ushirikishwaji wa jamii katika masuala ya usalama, Faustine Shilogile amesema ni muhimu kwa polisi kutumia busara na kufuata sheria katika kipindi chote cha uchaguzi.
“Uchaguzi una hatua tatu; kabla, wakati na baada. Katika hatua zote hizi, usalama ni jambo la msingi mnapaswa kuelewa kuwa hamuwezi kufanya kazi peke yenu, mnahitaji kushirikiana na viongozi wa kata na wananchi ili kudumisha amani,” amesema.
Akizungumzia mpango wa polisi jamii nchini, Shilogile amesema tangu kuanzishwa kwa mpango huo mwaka 2006, uhalifu umepungua kwa kiwango kikubwa nchini.
“Zamani kulikuwa na mauaji hadi 30 kwa siku na matukio ya unyang’anyi wa kutumia silaha kati ya matano hadi saba kwa siku, lakini tuligundua kuwa njia pekee ya kumaliza uhalifu ni kushirikisha jamii kupitia vikundi vya ulinzi shirikishi, na hali ya usalama imeimarika na matukio ya mauaji na ukatili yamepungua kwa kiasi kikubwa,” amesema.

Askari kata kutoka kata mbalimbali za Wilaya ya Geita wakimsikiliza Kamishna wa polisi anaesimamia Ushirikishwaji wa jamii katika masuala ya usalama Faustine Shilogile.
Shilogile atakuwa mkoani Geita kwa wiki mbili akitoa elimu ya ulinzi shirikishi kwa viongozi wa dini, wanasiasa na wananchi na leo Aprili 4, 2025 atazindua programu maalumu ya Polisi Jamii inayoshirikisha Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGML).
Programu hiyo inalenga kuwajengea na kuimarisha uelewa na uwajibikaji katika miradi ya polisi jamii kwa maofisa, wakaguzi na askari wa Jeshi la Polisi, viongozi wa Serikali, taasisi na wananchi kuhakikisha jamii inaendelea kushirikishwa na kushirikiana na jeshi hilo katika kuimarisha ulinzi na usalama.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Safia Jongo amesema uhusiano kati ya jeshi hilo na wananchi umeimarika, hali iliyosaidia kupunguza uhalifu hasa mauaji na matukio ya ukatili.
“Tunajenga uhusiano mzuri kati ya polisi na wananchi, viongozi wa kata, viongozi wa dini na wanasiasa. Ushirikiano huu umeleta matokeo chanya katika kudhibiti uhalifu,” amesema Safia.
Amesema kwa kipindi cha mwaka mmoja, mauaji ya wanawake yamepungua kutoka vifo 37 vilivyotokea mwaka 2023 hadi kufikia vifo saba mwaka 2024, sawa na asilimia 81 ya vifo vilivyoripotiwa kwa mwaka mkoani humo huku matukio ya ukatili wa kijinsia yakipungua kwa asilimia 44 kutoka matukio 95 hadi kufikia matukio 53 katika kipindi kama hicho.

Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita, Mohamed Gombat amesema programu ya Polisi Jamii inalenga kuwapa wananchi elimu ya namna ya kuzuia uhalifu kabla haujatokea.
Mgodi wa dhahabu mkoani Geita umejitolea kusaidia programu ya Polisi Jamii kwa muda wa wiki mbili, ikiwa ni sehemu ya kuhakikisha elimu ya ulinzi shirikishi inawafikia wananchi wengi zaidi.