Polisi wasimulia utata kifo cha straika wa Vipers

Dar es Salaam. Jana Jumatatu, Februari 24, 2025 soka la Uganda na Afrika Mashariki na Kati lilipata mshtuko kufuatia kifo cha ghafla cha mshambuliaji wa Vipers ya Uganda, Abubakar Lawal (29).

Taarifa za kifo cha mshambuliaji huyo raia wa Nigeria kimeibua utata kutokana na taarifa tofauti ambazo zimekuwa zikitolewa juu ya chanzo chake.

Baadhi ya ripoti zimedai kuwa mchezaji huyo amefariki kutokana na ajali ya gari lakini taarifa ya awali iliyotolewa na Polisi Uganda imeonyesha chanzo tofauti na ajali.

Ripoti ya Polisi Uganda imefichua kuwa mchezaji huyo alijirusha ghorofani muda mfupi baada ya kukutana na rafiki yake mwanamke ambaye anatajwa kuwa ni Mtanzania.

“Kitengo cha Polisi cha Kajansi kinachunguza mazingira ya kifo cha kusikitisha cha raia wa Nigeria Abubakar Lawal, mchezaji wa kandanda katika Klabu ya Vipers Sports, ambaye anadaiwa kuanguka kutoka ghorofa ya tatu ya Voicemall Shopping Arcade asubuhi ya Februari 24, 2025.

“Taarifa za awali zinaeleza kuwa Lawal alifika kwenye jumba hilo la maduka akiwa na gari lake lenye namba za usajili UBQ 695G kukutana na rafiki yake, Naima Omary, anayeishi chumba namba 416 tangu Februari 20, 2025,” inafafanua taarifa hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mchezaji huyo alijirusha muda mfupi baada ya Naima kuondoka.

“Kwa mujibu wa Naima, alimuacha Lawal katika chumba hicho akiandaa chai na kuelekea kituo cha michezo ndani ya jengo hilo. Muda mfupi baadaye, takriban saa 8:00 asubuhi, Lawal aliripotiwa kuanguka kutoka kwenye balkoni. Alikimbizwa katika Hospitali ya Rufaa ya Entebbe, ambapo ilitangazwa kuwa amefariki.

“Vitu vya marehemu, ikiwa ni pamoja na simu mbili za kisasa, jozi ya viatu vya wazi, vifaa vya sauti, vifaa vya kufundishia na chaja, vilipatikana kutoka kwa mkoba wake mweusi. Kama sehemu ya uchunguzi unaoendelea, mamlaka inarejesha picha za CCTV na kufanya mahojiano ya kina ili kubaini mazingira halisi ya tukio hilo.

“Taarifa zaidi zitatolewa kadiri uchunguzi unavyoendelea,” imefafanua taarifa ya kaimu ofisa habari wa Polisi, Luke Owoyesigyre.

Lawal alijiunga na Vipers mwaka 2022 akitokea AS Kigali ya Rwanda ambayo aliitumikia kwa miaka miwili.