Polisi walivyojitofautisha, Lissu akiletwa Kisutu

Dar es Salaam.  Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam imeimarisha ulinzi kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na maeneo ya jirani, wakati Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, amefikishwa kuendelea na kesi ya uhaini inayomkabili.

Katika maeneo hayo polisi wameonekana wakilinda usalama huku wakitoa maelekezo kwa wanachama na wananchi waliojitokeza kusikiliza kesi hiyo.

Kesi hiyo inaendelea leo Jumatatu, Mei 19, 2025 huku polisi wakitumia majadiliano zaidi tofauti na matumizi ya nguvu kama ilivyokuwa wakati Lissu alipofikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza ilipokuwa inasikilizwa kwa njia ya mtandao.

Kwenye maeneo jirani na mahakama, polisi wamewataka wafuasi wa Chadema waliovalia sare kukaa umbali wa 100 kutoka geti kuu la kuingilia mahakamani hapo.

Gari aina ya Toyota Land Cruiser Hardtop wakati likiwasili katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam likiwa limembeba Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu leo Jumatatu Mei 19, 2025. Picha na Michael Matemanga

Awali, Polisi waliwataka wafuasi hao kuondoka eneo hilo, lakini waligoma na kutaka waachwe kwa kuwa wameruhusiwa kuingia mahakamani kwa zamu.

“Sisi hapa hatuvunji sheria na hatutoki, tumeruhusiwa kuja mahakamani,” wamesema wafuasi hao.

Wakati hayo yakitendeka, ndani ya Mahakama kesi hiyo ilikuwa ikiendelea huku Polisi 16 wenye silaha wakiwa wamezunguka geti hilo kuimarisha ulinzi, huku wengine kadhaa wakizunguka maeneo tofauti jirani na Mahakama hiyo.

Raia wanaruhusiwa kupita na mara kadhaa Polisi wakiwaelekeza, tofauti na nyakati za nyuma ambapo walitumia mbwa kutawanya raia  na kuzuia watu kusimama pembezoni wakiwatawanya kwa mbwa, jambo ambalo leo halipo.

Itakumbukwa siku za  nyuma kesi hiyo ilipokuwa ikitajwa, jeshi hilo halikuruhusu raia yoyote kusimama jirani na eneo hilo na kuwafukuza kwa mbwa.

Leo imekuwa ni tofauti, achilia mbali raia wapita njia, Polisi wanawasikiliza wafuasi wa Chadema waliopo eneo hilo na kuzungumza nao bila kutumia nguvu, huku mara kwa mara wafuasi wakihoji ubaya wa wao kusimama eneo hilo na Polisi kuwajibu bila kutumia nguvu.

Lissu ambaye yupo rumande Gereza la Ukonga, anakabiliwa mashitaka matatu la kuchapisha taarifa za uongo katika mtandao wa Youtube, akidaiwa kutenda makosa hayo Aprili 3, 2025 jijini Dar es Salaam, kwa nia ya kulaghai umma kinyume cha sheria ya makosa ya kimtandao namba 14 ya mwaka 2015, kifungu cha 16.

Katika shitaka la kwanza, Lissu anadaiwa kuchapisha maneno yanayosomeka: ” Uchaguzi wa serikali za mitaa 2024 wagombea wa Chadema walienguliwa kwa maelekezo ya Raisi, wakati akijua maneno hayo ni ya uongo na ya kupotosha umma.

Shitaka la pili anadaiwa kuwa siku hiyo alichapisha taarifa za uongo na za kupotosha umma kuwa:

“Mapolisi wanatumika kuiba kura wakiwa na vibegi’.

Katika shitaka la tatu anadaiwa kuwa siku hiyohiyo alichapisha taarifa kuwa:

“Majaji ni MA-CCM, hawawezi kutenda haki, wanapenda wapate teuzi na kuchaguliwa kuwa majaji wa Mahakama ya Rufaa.

Kwenye kesi ya uhaini

Lissu anakabiliwa na shitaka hilo, kinyume na kifungu cha  39(2) (d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu.

Anadaiwa kutenda kosa hilo Aprili 3,2025 ndani ya jiji la Dar es Salaam, ambapo kwa nia ya uchochezi alishawishi umma kuzuia kufanyika kwa Uchaguzi  Mkuu wa mwaka 2025 kwa kuandika maeneo yafuatayo.

“Wakisema msimamo huu unaashiria uasi, ni kweli…, kwa sababu tunasema tutazuia uchaguzi, tutahamasisha uasi, hivyo ndivyo namna ya kupata mabadiliko…, kwa hiyo tunaenda kikinukisha…, sana sana huu uchaguzi tutaenda kuuvuruga kwelikweli…, tunaenda kukinukisha vibaya sana…”

Kwa mara ya kwanza, Lissu alifikishwa mahakamani hapo Aprili 10, 2025 na kusomewa kesi hizo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *