Tanga. Jeshi la Polisi Mkoa wa Tanga limeeleza sababu za kuendelea kumshikilia bondia maarufu nchini, Hassan Mwakinyo (29), anayetuhumiwa kumshambulia mkazi wa jijini humo, Mussa Ally akimtuhumu kuwa ni mwizi.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake leo Jumatatu Machi 10, 2025, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Almachius Mchunguzi amesema Mwakinyo anatuhumiwa kumshambulia na kumjeruhi Mussa, ambaye anajishughulisha na uvuvi kwa madai kuwa alipopita kwenye makazi yake.
Kamanda Mchunguzi amesema kuwa uchunguzi wa tuhuma hizo unaendelea na kwamba, watatoa taarifa rasmi na hatua zinazofuata pindi utakapokamilika.

“Tunamshikilia mkazi wa Sahare jijini Tanga, Hassan Mwakinyo kwa kumshambulia na kumjeruhi Mussa Ally. Uchunguzi wa tukio hili unaendelea na ukikamilika mtuhumiwa atapelekwa mahakamani,” amesema Mchunguzi na kuongeza: “Tunatoa wito wito kwa wananchi kuendelea kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu na kuacha kujihusisha na vitendo viovu hasa matukio ya kujichukulia sheria mikononi kwani, kwa kufanya hivyo ni kosa la jinai.’
Kwa mujibu wa Kamanda Muchunguzi amesema Mwakinyo baada ya kuhojiwa, amedai kuwa alimchukulia mtu huyo kama mwizi.
Tukio hilo lilitokea Machi 4, 2025 katika eneo la Sahare ambako ndiko makazi ya Mwakinyo.