
Geita. Jeshi la Polisi mkoani Geita limesema vitendo vya wizi wa ng’ombe vilivyoshamiri kwa sasa katika maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Geita vimetokana na wezi waliokamatwa miaka ya nyuma kumaliza vifungo na kurudi uraiani.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Safia Jongo akizungumza na waandishi wa habari leo Februari 12, 2025 amesema matukio ya wizi yalishamiri mwkaa 2023 na 2024, lakini jeshi hilo lilifanya msako na kuwakamata wanaohusika na matukio hayo ambao walishtakiwa na sasa wamemaliza vifungo vyao na kurudi uraiani na kuanza tena wizi huo.
“Uchunguzi wetu wa awali unaonyesha wanaohusika na matukio hayo ni wale tuliowakamata kwa wizi wa mifugo kwa msako tuiofanya kwa miaka miwili mfululizo na kuwafikisha mahakamani wapo waliopea vifungo vya miezi sita na wengine mwaka sasa wamemaliza vifungo vyao wamerudi mtaani.”
Kamanda Jongo amesema uchunguzi wa awali unaonyesha wezi hao wakishaiba ng’ombe huwachinja na kwenda kuuza kwenye mabucha bubu na kwa mamantilie huku wengine wakiuza kwa wapishi wanaopika kwenye sherehe mbalimbali.
“Mabucha rasmi yanauza nyama iliyopimwa na watu waliopewa hiyo mamlaka, lakini hawa wakiiba wanaenda kuuza kwa mama ntilie na wafanyabiashara wa vyakula tunashirikiana na mamlaka nyingine kuhakikisha mfanyabiashara anayeuza chakula nyama anayotumia imehakikiwa na mamlaka husika,” amesema Kamanda Jongo.
Kamanda Jongo amewataka wananchi kuanzisha vikundi vya ulinzi shirikishi vitakavyosaidiana na Jeshi la Polisi kuimarisha ulinzi na kumaliza vitendo vya uhalifu kwenye jamii.
Februari 8, 2025 kijana anaekadiriwa kuwa na mika 30 au 32 aliuawa kwa kupigwa na wananchi waliokuwa na silaha za jadi kwa tuhuma za kuhusika na wizi wa ng’ombe wawili walioibiwa kitongoji cha Kaseni kata ya Nyakamwaga Wilayani Geita.
Amesema kijana huyo akiwa na wenzake watatu waliingia kwenye zizi la mifugo la Dominiko Peter na kuiba ng’ombe wawili kisha kuwaswaga hadi kitongoji kingine na kwenda kuwachinja karibu na mto.
Kamanda Jongo amesema wananchi walipofika eneno la mto uliopo karibu na kijiji hicho waliwakuta watu wanne wakiwa eneo la maficho kwenye vichaka wakiwa tayari wamechinja ng’ombe mmoja na kupakia nyama kwenye mifuko ya sandarusi.
“Wananchi walipokuwa wakiwahoji watu hao ili kujiridhisha na mifugo waliyokutwa nayo na kwa nini wananchinja usiku kwenye vichaka, watu watatu walifanikiwa kukimbia akabaki mmoja ambaye naye alitaka kuwajeruhi wnanchi na panga katika kujihami walitumia silaha za jadi na kumsababishia majeraha yaliyopelekea kifo chake,” amesema.
Kwa mujibu wa kamanda huyo, mwili wa kijana huyo ambaye hajatambulika umehifadhiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Geita kwa uchunguzi na utambuzi wa ndugu.
Kamanda Jongo amewataka wananchi kuacha kujichukulia sheria kwa kuwa vitendo vya aina hiyo vina madhara kwao na kwa jamii pia.
Wananchi wasimulia
Huruma Mhozya ambaye ni mwenyekiti wa kitongoji cha Kaseni kijijini cha Iponyamakarai wilayani Geita amedai siku ya tukio alipigiwa simu na wananchi kuwa kuna tukio la wizi wa ng’ombe ambapo walipiga kelele ya ishara ya tahadhari ili wananchi waamke na kuanza msako.
Amesema kwa msaada wa nyayo za ng’ombe na nyayo za wezi hao walifanikiwa kuzifuatilia hadi kwenye mto ulioko kitongoji kingine na walipofika walikuta watu wakipakia nyama kwenye mfuko na walipowafikia watatu walikimbia na kumuacha mwenzao ambaye alishambuliwa na wananchi na kufariki dunia.
Mhozya amesema wizi wa mifugo umekuwa mkubwa kwenye kitongoji chao ambapo kuanzia mwaka uanze matukio 12 yameripotiwa kwake na
Mwenyekiti wa Kijiji cha Iponyamakarai, Lukas Buswelu ambaye amesema matukio ya wizi wa mifugo kijiji hapo yameshamiri hadi kufika mahali pa kujuta kugombea nafasi ya uongozi.
“Kwenye kijiji changu wizi wa ng’ombe umeshamiri matukio ni mengi mimi ni kiongozi mpya niliyechaguliwa uchaguzi wa juzi, lakini naona bora ningebaki kulima kuliko kuwa kiongozi, wananchi wangu wazuri sana, lakini haya matukio yanakatisha tamaa ningejua kuna hali hii nisingeomba hii hali inanipa hofu,” amesema Buswelu.
Sikuzani Shija ambaye ni mfugaji amesema kutokana wezi kuwa na tabia ya kurudi mara kwa mara kwa sasa wamelazimika kuuza ng’ombe wakubwa huku ndama anaishi nao ndani ya nyumba ili wawe salama.
“Tulikua hatulali tunakaa kuchunga mifugo ukijiegesha kidogo ukipitiwa na usingizi na wao wanaingia kuiba mwisho mume wangu akaona haya ni mateso akaamua kuuza wote sasa hivi nina ndama wawili na mbuzi na tunaishi nao ndani,” amesema.
Wananchi wameiomba Serikali kuchunguza mtandao huo wa wizi wa ng’ombe na kujua wanakokwenda kuuza nyama ili wizi huo ukomeshwe.
Hivi karibuni akizungumza kwenye Baraza la Madiwani la Manispaa ya Geita, Mwenyekiti wa CCM wa wilaya hiyo, Barnabas Mapande amesema wizi wa mifugo ni mkubwa na kutaka utafutiwe ufumbuzi.
“WIzi wa mifugo wezi wanaingia kwenye zizi na kwenda kuchinja na kuuza maeneo mengine ikiwemo kwenye mabucha ni vizuri mkaangalia ng’ombe ambao hawachinjwi kwenye machinjio rasmi nyama inapelekwa wapi wanao hakiki nyama watueleze,” amehoji Mapande.