Polisi waanza uchunguzi vitisho dhidi ya Askofu Bagonza, bado Mwabukusi

Dar es Salaam. Nani waliowatishia hawa? Ni swali linalosubiri majibu baada ya Askofu wa Dayosisi ya Karagwe ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) na Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Boniface Mwabukusi kusema wametishi na Jeshi la Polisi likianza kuchunguza mojawapo.

Wawili hao kwa nyakati tofauti wameeleza kuwa tayari wamewasilisha taarifa kwa vyombo vya uchunguzi, lakini Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Brasius Chatanda ndiye pekee amethibitisha kupokea malalamiko ya Askofu Bagonza na kuwa uchunguzi unaendelea.

Kuhusu Mwabukusi, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga amekana kupokea taarifa za wakili huyo, akisema kama yuko nje ya mkoa huo, anatakiwa kwenda kuripoti Kituo cha Polisi kilicho karibu yake.

Hofu ya vitisho hivyo juu ya maisha ya wawili hao, inaongezwa nguvu na tukio la kuvamiwa, kupigwa, kuteswa kisha kutekwa kwa mwanaharakati Mdude Nyagali wa jijini Mbeya, ikiwa ni saa chache tangu atoe taarifa ya kutafutwa.

Aprili 30, 2025 saa 8:14, Mdude aliandika katika ukurasa wake wa X kuwa kuna watu waliojitambulisha ni Polisi wa Mkoa wa Mbeya, walikuwa wakitafuta mahali anapoishi, bila kueleza kosa wanalomtafutia.

“Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya wanatafuta nyumba ninayoishi sijui wanataka kuja kutambika au kuniteka. Wamemwambia mmoja wa wanachama wetu kwamba tunaomba utuonyeshe nyumba tu anayoishi Mdude tutakupa pesa,” alieleza.

“…namba zangu za simu ziko ofisi ya RPC na RCO (mkuu wa upelelezi) Mbeya, wao kama wanaona kuna tuhuma dhidi yangu si wanipigie niende? Kwa nini wananiwinda na kunizivizia? Kama lengo ni kuniteka nawaapia watatangulia wao,” aaliandika.

Saa machache baada ya kuandika ujumbe huo, watu wasiojulikana walimvamia nyumbani usiku wa kuamkia Mei 2, 2025 na kumshambulia kisha kuondoka naye.

Baadaye ilisambaa video ya mtu aliyedai ndiye aliyeulizwa na askari wawili ambao aliwataja kwa majina.

Hata hivyo, Jeshi la Polisi mkoa wa Mbeya lilikanusha kuwafahamu askari waliotajwa kutoka ofisi ya RCO kuwa ndio waliokuwa wakimtafuta Mdude, na wakaomba wapelekewe taarifa sahihi za tukio hilo na washukiwa halisi.

Baadaye Jeshi hilo makao makuu lilieleza limetuma timu ya wapelelezi kuchunguza madai ya askari kutajwa, na hadi sasa hakuna taarifa iliyotolewa.

Vitisho kwa Askofu Bagonza, Mwabukusi

Askofu Bagonza aliripoti kutishiwa maisha Mei 7, 2025 huku Rais wa TLS naye akieleza kupata vitisho hivyo Mei 10, 2025.

Mei 8, 2025 Askofu Bagonza aliandika kupitia mtandao wa Facebook, kuwa:-

“Nimepokea taarifa ya tahadhari kuwa wasiojulikana watakuja kunimaliza sishangai, maana ukimfunga mbwa ukamwachia aonje damu za watu huwezi kumdhibiti tena na hawezi kuacha mwenyewe,” aliandika Askofu Bagonza.

Mei 10, 2025, KKKT Dayosisi ya Karagwe kupitia kwa Katibu Mkuu wake, Jeremiah Rugimbana ilitoa tamko la kulaani vitisho vinavyotolewa kwa askofu huyo.

“Tunalaani vikali vitendo hivyo vya vitisho kwa Mkuu wetu na kwa watu wengine vinavyokwenda kinyume na maadili, utu, na haki za binadamu. Tunaendelea kushirikiana na vyombo vya dola kuhakikisha usalama wake na wa wafanyakazi wote unalindwa ipasavyo,” lilieleza tamko hilo.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumatano, Mei, 14, 2025, Dk Bagonza amesema amekuwa akipokea vitisho vya kutishiwa maisha mara nyingi na mwisho ilikuwa Mei 7, 2025.

“Baada ya hapo niliripoti na Polisi Mkoa wa Kagera walikuja nikawapa taarifa zote wakaondoka na wanaendelea na uchunguzi,” amesema.

Dk Bagonza amesema hawezi kuzungumzia zaidi kwani baada ya Polisi kwenda kwake walimweleza jambo hilo akilizungumza anaweza kuharibu uchunguzi.

“Vitisho vya kutishiwa kwangu kilele ilikuwa ni Mei 7,2025 lakini huko nyuma vilikuwa vinaendelea taratibu taratibu,” amesema Dk Bagonza.

Kuhusu Mwabukusi, Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) nacho kilitoa tamko likilaani na kusema kila raia wa Tanzania ana haki ya kuishi na kufanya kazi zake halali bila vitisho, woga wala hofu.

“Rais wetu amepokea ujumbe kwenye simu yake kutoka kwenye namba ya simu ya mkononi (wanaitaja) ukiwa unaonyesha kuna mipango ovu ya kuondoa uhai wake,” ilisema taarifa hiyo kwa umma na kuongeza kuwa:-

“TLS inakemea na kulaani kitendo hicho kwani ni kinyume na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977 na Sheria za nchi yetu.”

Akizungumzia hilo, Mwabukusi amesema alitumiwa vitisho hivyo kupitia namba ya simu akielezwa hatakiwi kuonekana mkoani Mbeya na akikaidi basi atakutana nao (waliomtishia).

“Niko mbali lakini nimeshawasilisha ripoti kwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya (RCO) nimemtumia namba husika na aina ya mesaji nilizotumiwa. Aliyenitumia anataka nisirudi Mbeya, manake yupo Mbeya,” amesema.

Kwa mujibu wa Mwabukusi, baada ya kuwasilisha taarifa hiyo alijibiwa anasubiriwa akirudi akaandikishe maelezo ili uchunguze uweze kufanyika.

“Vitisho hivi nilivipokea siku ya Ijumaa na Jumamosi, baada ya kelele za watu imekuwa kimya (havikuendelea),” amesema.

Alipoulizwa anahisi kwa nini atumiwe vitisho sasa, amesema:-

 “Ni kwa sababu nilisema lazima masuala ya utekaji yafikie ukomo na hatuwezi kuvumilia, lazima tuchore mstari na kupitia hili suala la Mdude Nyagali, tuwajue ni kina nani wanaoteka watu,” amesema Wakili Mwabukusi na kuongeza:

“Nilisema Lazima tusimamie na hatutakubali tena,” amesema.

Mwabukusi amesema suala la utekaji nchini kwa sasa limekuwa changamoto, kila baada ya muda watu wanapotea na wanaosikika na kujulikana ni wale tu wenye majina.

“Hali si salama, hakuna aliye salama, changamoto imekuwa kubwa lazima tuungane kulikabili jambo hili kwa kuchukua hatua za kisheria na kushinikiza mambo haya yaishe. Haiwezekani watu wanatajwa lakini hawaguswi,”amesema.

Wakili Mwabukusi amesema jamii nzima lazima ipige kelele, viongozi wadini wawe mstari wa mbele ili watu waambiwe ni kina nani wanatenda uhalifu huo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *