MAJUZI ilikuwa ni furaha kwa wachezaji wa Polisi baada ya kuifunga Stein Warriors kwa pointi 64-60 katika fainali ya Ligi ya Kikapu ya Daraja la Kwanza Mkoa wa Dar es Salaam iliyopigwa katika Uwanja wa Donbosco, Oysterbay, Dar es Salaam.
Hata hivyo, licha ya Polisi na Stein Warriors kucheza fainali hiyo tayari zimeshafuzu kucheza Ligi Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam (BDL) mwaka huu kutokana na timu hizo kushika nafasi mbili za juu.
Kabla ya fainali hiyo kufanyika ilitangulia mchezo wa kutafuta mshindi wa tatu kati ya Kurasini Heat na Mlimani B.C ambao Kurasini Heat ilishinda kwa pointi 56-48.
Kwa matokeo hayo Polisi, Stein Warriors na Kurasini Heat zitacheza Ligi ya Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam kuchukua nafasi ya Jogoo, Ukonga Kings na Crows zilizoshuka daraja.
Fainali hiyo ilishuhudiwa na watazamaji wengi iliongozwa na katibu mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Kikapu Tanzania (TBF) Mweze Kabida na mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa KIkapu Dar es Salaam (BDL), Shendu Mwangalla.

POLISI VS STEIN WARRIORS
Pointi 15-6 zilizofungwa na Polisi katika robo ya pili ndizo zilizoibeba kuishinda Stein Warriors katika fainali hiyo.
Pointi nne walizoizidi Stein Warriors zilionekana ni nyingi kutokana na ushindani mkubwa uliokuwepo.
Katika mchezo huo Polisi iliongoza katika robo ya kwanza kwa pointi 20-12, 15-6, 12-10 na ile ya nne Stein Warriors ilipata pointi 25-17.
Mchezaji Lawi Mwambasi wa Polisi aliongoza kwa kufunga pointi 23, akifuatiwa na Fahmi Hamadi aliyefunga 14, huku upande wa Stein Warriors alikuwa Abasi Omary aliyefunga pointi 16 akifuatiwa na Davis Mshamu pointi 15.

KURASINI HEAT VS MLIMANI B.C
Sababu mbili ndizo zilizosababisha Mlimani B.C ipoteze mchezo wake dhidi ya Kurasini Heat kwa pointi 56-48 katika mchezo wa kutafuta mshindi wa tatu.
Mlimani B.C iliyopewa nafasi kubwa kushinda katika mchezo huo ilishindwa kuonyesha makali kama ilivyokuwa katika mchezo wa nusu fainali iliocheza na Polisi.
Sababu ya kwanza ya timu hiyo kufanya vibaya ni kutogudua mapema makosa iliyofanya yakiwemo ya kila mchezaji kutaka kufunga kwa kutumia nguvu kupita mbele ya walinzi wa timu pinzani.
Kufanya hivyo kuliwafanya wachezaji hao wapigiwe filimbi ya madhambi.
John Ally, kocha wa kikapu kutoka Kinondoni alisema mchezaji inampasa kutoa pasi kwa mchezaji wenzake kama amebanwa ili kusaidia timu kupenya na kupata matokeo.
“Nimeshangaa hata benchi la timu hiyo halikungudua kosa hilo. Niliona walikuwa wanawalazimisha waingie tu ndani,” alisema Ally
Sababu nyingine ni kujiamini kupita kiasi. Katika mchezo huo Mlimani B.C iliongoza katika robo ya kwanza kwa pointi 14-13, ya pili Kurasini Heat ikaongoza kwa pointi 12-10, 12-8, 19-16.
Hillary Felix wa Kurasini alifunga pointi 17 akifuatiwa na Dominic Zacharia aliyetupia 11, huku
Martin Rodgers wa Mlimani B.C akiongoza upande wa timu hiyo kwa alama 16 akifuatiwa na Baraka Kweka aliyefunga pointi 9.
Nahodha wa Kurasini Heat Dominic Zacharia aliwapongeza wachezaji wenzake akisema: “Kwa kweli wachezaji wangu walijituma na mipango tuliyoiweka ilikuwa mizuri na hata tungetolewa robo fainali tungeliona ni sawa kutokana na uchanga wa wachezaji,” alisema Zacharia.
Kwa mujibu wa Zacharia, baada ya Mlimani B.C kutamba wachezaji wao walibadilika na kuipa kichapo ambacho haikukitegemea na kwamba kule BDL wataongeza wachezaji pamoja na kutafuta wadhamini ili washiriki vizuri.

WACHEZAJI BORA WALAMBA ZAWADI
Wachezaji bora wa kila nafasi walizawadiwa zawadi za vikombe katika ligi hiyo.
Kwa upande wa mchezaji bora wa ligi hiyo (MVP), alichaguliwa Lawi Mwambasi wa Polisi na mfungaji bora akiwa Davidson Evarist wa Christ The King.
Upande wa ufungaji katika eneo la mitupo mitatu (three points) alichaguliwa Omary Njota wa Yellow Jacket na ule wa asisti aliibuka Davis Mshamu wa Stein Warriors.
Kwa upande wa uporaji mipira (steals) alichaguliwa Robert Mwaipungu wa Christ The King na Lawi Mwambasi alichaguliwa ule wa udakaji ‘rebound’, huku uzuiaji (blocks) akiondoka nayo Mwinyipembe Jumbe wa Stein Warriors na mchezaji chipukizi akiwa ni Kelvin Mushi wa Premier Academy.
Mwambasi alimshukuru mungu kwa kuchaguliwa kuwa mchezaji bora wa mashindano hayo, lakini aliwapongeza wenzake kwa ushirikiano walioonyesha timu hiyo ikapanda daraja.

BDL YATOA ZAWADI ZA VIKOMBE
Katika hatua nyingine, Chama cha Mpira wa Kikapu Dar es Salaam (BD), kimewazawadia washindi wa Ligi ya Kikapu mkoa huo katika tukio lililofanyika kwenye Uwanja wa Donbosco, Oysterbay.
Zawadi za vikombe na medali ilitolewa na katibu mkuu wa TBF, Kabinda kwa timu ya wanaume ya JKT na upande wanawake walipewa Donbosco Lioness.
Kwa upande wa mchezaji bora wa mashindano hayo aliondoka nayo Amin Mkosa wa Mchenga Star ilhali upande wanawake alikuwa ni Taundensia Olouch wa Donbosco Lioness.