Polisi Simiyu wamnasa luteni feki wa JWTZ

Simiyu. Jeshi la Polisi Mkoa wa Simiyu limemkamata mtu mmoja anayejifanya askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), akiwa na sare za jeshi hilo.

Mtu huyo aliyefahamika kwa jina la Emmanuel Mapana (24), mkazi wa Mtaa wa Sima mjini Bariadi, alikutwa na sare zinazofanana na za jeshi hilo, zikiwa na cheo cha luteni.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, Kamishina Msaidizi wa Polisi (ACP), Edith Swebe, mtuhumiwa amekamatwa na kikosi kazi cha kupambana na uhalifu na wahalifu mkoani humo leo, Ijumaa Februari 14, 2025 saa 6:30 mchana.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa mtuhumiwa amekutwa kwenye gari na baada ya upekuzi amekutwakombati hizo, mkanda wa JWTZ na kompyuta mpakato moja.

Polisi wamesema Mapana alikuwa akitafutwa muda mrefu na jeshi hilo kwa kosa la kujifanya mtumishi wa Serikali.

Kufuatia tukio hilo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Simiyu limetoa wito kwa wananchi wote kuendelea kushirikiana nalo kwa kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu.

Matukio ya watu kukamatwa na sare za majeshi mbalimbali yamekuwa yakijiorudia hapa nchini na kuna kipindi JWTZ iliwahi kutoa kipindi cha msamaha kwa watu walio nayo kuyasalimisha.