Mbeya. Wakati Jeshi la Polisi mkoani Mbeya likiendelea na operesheni maalumu kupambana na kudhibiti uhalifu, limekamata shehena ya dawa za kulevya iliyodaiwa kusafirishwa kutoka nchi jirani ya Malawi kuingizwa nchini Tanzania.
Shehena hiyo imekamatwa wilayani Rungwe ikiwa katika gari aina Mitsubish Canter huku mihadarati hiyo ikiwekwa ndani ya magunia ya pumba.
Akizungumza leo Aprili 21, kamanda wa polisi mkoani humo, Benjamin Kuzaga amesema baada ya kupata taarifa kutoka mamlaka ya kudhibiti dawa za kulevya walifika wilayani humo na kulikamata gari hilo.
Amesema hadi sasa inadhaniwa shehena hiyo kuwa na dawa za kulevya aina ya bangi na inasubiriwa uchunguzi wa kitaalamu kwa mkemia kubaini zaidi na ujazo wake.
“Jumla ni vifurushi 67 vilivyokuwa kwenye gari hili, baada ya kupimwa kwa mkemia tutajua kiasi halisi na aina ya dawa zenyewe, niombe wananchi wanaojihusisha na dawa za kulevya waache kazi hii.
“Jeshi la Polisi tutaendelea na operesheni hii, tutaendelea kushirikiana na mamlaka za kupambana na dawa za kulevya ili kunusuru nguvu kazi ya Taifa, hatutakubali kuchafua picha ya nchi,” amesema Kuzaga.

Vifurushi vya madawa ya kulevya aina ya bhangi vilivyokamatwa na Jeshi la Polisi mkoani Mbeya vikisafirishwa kutoka nchini Malawi kuingizwa Tanzania.
Mjumbe wa Serikali ya Mtaa wa Kawetele Chini, Julius Tweve amelipongeza Jeshi la Polisi mkoani humo kwa kazi wanayofanya katika kulinda na kutunza amani na usalama kwa wananchi.
Amewataka wananchi maeneo yote mkoani humo kuacha vitendo vya kujihusisha na dawa ya kulevya akiomba kila mmoja kuwa balozi kufichua vitendo hivyo, akifafanua kuwa yanaharibu vijana na kizazi kijacho.
“Hasa wale wanaoishi mipakani na hata maeneo mengine, tuwe mabalozi kufichua vitendo hivi, vinginevyo tutaharibu na kuua kizazi kijacho, tuache biashara hii kwa masilahi ya Taifa letu,” amesema Tweve.