Polisi Dodoma watoa wito kwa wananchi kuwafichua wamiliki haramu wa silaha

Polisi Dodoma watoa wito kwa wananchi kuwafichua wamiliki haramu wa silaha

Dodoma. Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma limewataka wananchi kushirikiana na vyombo vya usalama kutoa taarifa kuhusu watu wanaomiliki silaha kinyume cha sheria, likieleza kuwa hatua hiyo ni muhimu katika kulinda amani na usalama wa jamii.

Pia, Jeshi la Polisi limetoa onyo kwa askari wake wote watakaobainika kufichua au kuvujisha taarifa za raia wema wanaotoa kuhusu uhalifu na wahalifu, likisisitiza kuwa kitendo hicho ni uvunjifu wa maadili ya kazi ya polisi na hakitavumiliwa.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, George Katabazi, ametoa kauli hiyo leo, Jumanne Mei 20, 2025, jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kukamatwa kwa watuhumiwa wanne kwa kosa la kumiliki silaha kinyume cha sheria.

Amesema kuwa watuhumiwa hao walikamatwa kufuatia msako maalumu unaoendelea kufanywa na jeshi hilo kwa kushirikiana na raia wema wanaotoa taarifa muhimu kuhusu vitendo vya uhalifu katika maeneo yao.

Katabazi amesema kuwa Mei 17, 2025 saa 11 jioni, katika mtaa wa Kikuyu Mission uliopo jijini Dodoma, Jeshi la Polisi liliwatia mbaroni watuhumiwa wawili waliokutwa na silaha aina ya bastola ikiwa na magazine yenye risasi 13, kinyume na sheria za umiliki wa silaha.

Amesema pia Mei 19, 2025 saa 11 jioni katika mtaa wa Lukole uliopo wilayani Mpwapwa Jeshi la Polisi waliwakamata watumiwa wawili wakiwa na silaha iliyotengenezwa kienyeji inayotumia risasi za ‘shot gun’ na risasi nne kinyume cha sheria.

“Nitoe onyo kwa watu wanaomiliki silaha kinyume na sheria  kufuata utaratibu wa kumiliki silaha hizo kisheria na kwa wale ambao bado wanazo wazisalimishe wenyewe kwenye kituo chochote cha polisi kilichopo jirani, serikali za mitaa au serikali za kijiji kabla mkono wa sheria haujamfikia,” amesema Katabazi

Katika hatua nyingine Katabazi amesema Mei 18, 2025 saa 4 usiku eneo la Kikuyu lililopo kata ya Kizota waliwakamata watumiwa wawili waliotambulika kwa majina ya Thomas Pascal na Nestory Kimario waliokuwa wakisafirisha mafuta aina ya dizeli lita 2,420 kwenye gari aina ya Toyota Hiace yanayodhaniwa kuwa ni ya wizi.

Amesema watuhumiwa wengine  57 wanashikiliwa na jeshi hilo kwa makosa mbalimbali yakiwemo ya  wizi, uvunjaji na kuwa na vifaa vya kuvunjia na kufanyia uhalifu ambapo  watuhumiwa 30 wameshafikishwa mahakamani na wengine 27 bado wanawafanyia uchunguzi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *