
Dar es Salaam. Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limeonya wananchi kutojitokeza katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Aprili 24,2025 wakati Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu akifikishwa mahakamani hapo, likisisitiza atakayejitokeza atashughulikiwa kwa mujibu wa sheria.
Katazo la Jeshi la Polisi kwa wananchi ni kufuatia wito wa Makamu Mwenyekiti wa Chadema, John Heche kuwataka wanachama wa chama hicho na wananchi kufika kwa wingi Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Aprili 24,2025 wakati Mwenyekiti wao Lissu akifikishwa mahakamani kusikiliza kesi ya uhaini inayomkabili.
Heche ameyasema hayo katika mkutano wa hadhara uliofanyika viwanja vya Mbezi, wilaya ya Ubungo Aprili 16,2025 wakati akihutubia mamia ya wananchi waliofika kumsikiliza, akiwahimiza wananchi hao kufika mahakamani hapo bila kuwa na silaha yeyote wala kufanya fujo bali wabebe vitambaa vyeupe na maji.
Akizungumzia wito huo, leo Aprili 17,2025 jijini Dar es Salaam Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro amesema jeshi hilo limefuatilia mipango ya viongozi wa chama hicho na kubaini siku hiyo kutafanyika vurugu.
Muliro amesema lengo la vurugu hizo ni kushinikiza mamlaka za kisheria kumwachia kiongozi wao ambaye anatuhumiwa.
“Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam linawakumbusha wahusika kuwa Mahakama ni mamlaka za kisheria zilizo huru na hazipaswi kutishwa au kuingiliwa
wakati wa utekelezaji wa majukumu yake.
“Polisi linawatahadharisha watu wote wanaohamasisha kuhusiana na nia hiyo ovu kutoshiriki kwenye mpango huo na linatoa onyo kali kuwa wale wote na wanaopanga ambao watajaribu kutekeleza kinachohamasishwa watashughulikiwa vikali kwa mujibu wa sheria za nchi,”amesema.
Lissu alipandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza na kusomewa shitaka la uhaini baada ya kukamatwa mkoani Ruvuma, alikokuwa kwenye ziara ya kuhamasisha ajenda ya chama hicho ya Hakuna Mageuzi, Hakuna Uchaguzi.
Kabla ya kusomewa shitaka hilo, taarifa ya Jeshi la Polisi iliyosainiwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Marco Chilya, ilieleza kuwa Lissu alikamatwa baada ya kuwepo madai ya kufanya uchochezi na hivyo jeshi hilo linamshikilia kwa mahojiano.
Katika hatua nyingine Kamanda Muliro amesema jeshi hilo limejipanga kuhakikisha waumini wa dini ya Kikristo wanasherekea siku hiyo kwa amani na utulivu.
“Tunatoa wito kwa wazazi na walezi kuwa na uangalizi wa karibu kwa watoto wakati wa matembezi na mikusanyiko mbalimbali, pia nyumba na makazi yasiachwe bila uangalizi wakati wa sherehe hizi.
Suala la usalama barabarani, tunasisitiza madereva wa vyombo vya moto na watumiaji wengine wa barabara kuzingatia sheria ili kuepusha ajali,”amesema.