Pigo lingine Arsenal, ikimkosa Havertz msimu mzima

London. Arsenal itamkosa mshambuliaji wake Kai Havertz katika mechi zote zilizobakia msimu huu baada ya kupata maumivu ya misuli katika kambi ya timu hiyo inayoendelea Dubai.

Hiyo ni habari kwa mbaya kwa Arsenal katika kipindi ambacho inawakosa nyota wengine watatu wa ushambuliaji, Bukayo Saka, Gabriel Jesus na Gabriel Martinelli kutokana na majeraha.

Bukayo Saka atarejea uwanjani hivi karibuni kama ilivyo kwa Martinelli lakini Jesus atakuwa nje ya uwanja kwa msimu mzima ambapo sasa ataungana na Havertz ambaye ndio amekuwa tegemeo la Arsenal msimu huu.

Kumkosa Havertz ni pigo kubwa kwa meneja wa Arsenal Mikel Arteta kwani Mjerumani huyo ndiye amekuwa akitumika kuziba pengo la kukosekana kwa mshambuliaji wa kati hivyo maumivu yake hapana shaka yanaweka shakani ndoto ya timu hiyo kutwaa mataji msimu huu.

Kai ndiye mfungaji bora wa Arsenal msimu huu ambapo hadi sasa ameifungia mabao 15 msimu huu ambayo yamechangia kuifanya iwe katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu England na pia kuiwezesha kutinga hatua ya 16 bora ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Arteta hapana shaka atakuwa kwenye wakati mgumu zaidi kwa vile klabu hiyo ilishindwa kumsajili mshambuliaji katika dirisha dogo la usajili la majira ya baridi mwezi Januari.

Majeraha ya Havertz yametokea katika muda mmoja na yale ya goti ya beki Takehiro Tomiyasu ambaye anatarajaiwa kufanyiwa upasuaji utakaomuweka nje msimu mzima.

Hata hivyo, majeraha ya Tomiyasu huenda yasimvuruge sana kichwa Arteta kutokana na urejeo wa beki Ben White ambaye alikuwa nje ya uwanja kwa muda mrefu.