
Moshi. Mahakama ya Rufani Tanzania, imemfutia adhabu ya kifo, Frank Ezbon, aliyemuua mpenzi wake, Jesca Lucas baada ya kukuta picha za utupu kwenye WhatsApp akiwa na mwanamume mwingine, badala yake imemuhukumu kifungo cha miaka 15 jela.
Tukio la mauaji ya Jesca, lilitokea Julai 2020 katika nyumba ya kulala wageni ya Paradise Lodge iliyopo Mji wa Mugumu Wilaya ya Serengeti mkoani Mara, huku kiini kikiwa ni picha na video zilizokutwa kwenye WhatsApp.
Katika hukumu yao waliyoitoa Machi 25, 2025, Jopo la majaji watatu wa Mahakama hiyo, Dk Mary Levira, Benhaji Masoud na Deo Nangela, wamesema Jamhuri haikuthibitisha kosa la mauaji ya kukusudia bali ni ya bila kukusudia.
Kwa mujibu wa nyaraka za rufaa iliyowasilishwa mbele ya Mahakama ya rufani, Jesca na Frank Ezbon walikuwa wanatambuliwa kama wapenzi kwa muda mrefu licha ya kuwepo matukio ya misuguano baina ya wawili hao.
Julai 12, 2020 saa 9:00 alasiri, wawili hao walikwenda katika nyumba ya kulala wageni ya Paradise Lodge na kupewa chumba namba tisa, lakini mrufani (Ezbon) aliondoka saa 1:00 usiku na kurejea chumbani muda mfupi baadaye.
Walipofika chumbani, Jesca alimuomba mpenzi wake akamnunulie chips, lakini wakati anaondoka alichukua simu ya Jesca na njiani aliperuzi WhatsApp na kukuta picha za Jesca na mwanamume mwingine wakiwa utupu.
Baadaye mrufani hakuonekana tena akitoka katika nyumba hiyo hadi siku iliyofuata Julai 13, 2020 saa 3:30 asubuhi muhudumu alipokuwa akifanya usafi.
Aligonga katika chumba cha wawili hao akitaka kuwaeleza anataka afanye usafi lakini hakujibiwa.
Muhudumu huyo aliamua kuusukuma mlango ukafunguka kirahisi na alipoingia ndani alikutana na harufu na Jesca akiwa kitandani, jitihada za meneja pamoja na muhudumu huyo kumwamsha hazikuzaa matunda.
Taarifa hizo zilipelekwa polisi ambao walifika na baadaye waliwajulisha kuwa, mteja wao huyo ni mfu.
Julai 15,2020 mwili wa Jesca ulifanyiwa uchunguzi wa kiini cha kifo na kubaini kilitokana na kukosa hewa ya oksijeni.
Baada ya uchunguzi, mrufani alikamatwa mkoani Songwe na katika maelezo yake aliyoyaandika kwa mlinzi wa amani, Leonard Kazinzuri na mengine aliyoyaandika mbele ya polisi, Sajini Saimon Samweli ilidaiwa kuwa alikiri kufanya mauaji hayo.
Alivyojitetea kortini
Baada ya kukamilika kwa uchunguzi, mrufani alifikishwa kortini na kushtakiwa kwa mauaji ya kukusudia ambapo alikanusha mashitaka hayo na baada ya Jamhuri kufunga ushahidi wao, alionekana ana kesi ya kujibu na kutakiwa kujitetea.
Katika utetezi wake, aliegemea ushahidi wa kutokuwepo eneo la tukio siku na saa inayodaiwa na kueleza kuwa aliondoka Mugumu kwenda Mwanza Julai 7, 2020 akiwa amefuatana na babu yake mgonjwa na walipanda basi la Manchester.
Alisisitiza kuwa alikaa Mwanza hadi babu yake huyo alipofariki Julai 30,2020 na baada ya mazishi yake yaliyofanyika Magu Agosti 3,2020 na ndipo aliposafiri kwenda Jijini Dar es Salaam na baadaye alikwenda Tunduka mkoani Mbeya.
Ezbon alikiri kumfahamu marehemu na kueleza kuwa alikuwa mpenzi wake wa muda mrefu kabla uhusiano wao haujavunjika mwaka 2019, na kukiri kuwa aliandika maelezo ya kukiri kutenda kosa hilo, lakini hiyo ni kutokana na kupigwa na kuteswa na polisi.
Baada ya mahakama kusikiliza ushahidi wa Jamhuri na wa utetezi, ilimtia hatiani na kumuhukumu adhabu ya kunyongwa hadi kufa, lakini akakata rufaa kupinga hukumu hiyo akisema Jamhuri hawakuwa wamethibitisha mashtaka dhidi yake.
Picha akaunti ya Whatsapp
Mawakili wawili, Leonard Magweyaga na Juma Mwita ambao walimtetea mrufani katika hatua ya rufaa, walieleza kuwa kutiwa hatiani kwa mteja wao kuliegemea kielelezo P3 na P4 ambavyo viliegemewa kimakosa na Mahakama.
Mawakili hao walieleza kuwa kielelezo P3 ambayo ni maelezo ya mshtakiwa yalichukuliwa Septemba 14,2020 siku tisa tangu tangu alipokamatwa Septemba 5,2020 na hakuna maelezo ya kwa nini ilikuwa hivyo.
Kitendo hicho kilikuwa ni kinyume na mwongozo wa Jaji mkuu ambao unataka maelezo ya mtuhumiwa yachukuliwe mara moja na bila kuchelewa, lakini pia ukurasa wa 53 wa kumbukumbu za rufaa unaonyesha haikusainiwa.
Wakili Magweyaga alienda mbali na kueleza kua kifo cha marehemu kama kilivyoelezewa na mrufani katika kielelezo P4, kilichoegemewa na Mahakama katika kumtia mtuhumiwa hatiani, kilitokana na kuchokozwa na marehemu.
Kulingana na wakili huyo, kiini cha tafrani ilitokana na mrufani kuona katika simu ya marehemu, picha na video fupifupi za marehemu katika akaunti ya Whatsapp akiwa na mwanamume mwingine wakiwa utupu katika tendo la urafiki.
Ni kutokana na picha hizo, mrufani alichokozwa (provoked) kutokana na kile alichokiona, hivyo alirudi chumbani ambako aliishia kusababisha kifo cha marehemu baada ya kumnyonga shingo kwa msaada wa kamba ya jaketi lake.
Mawakili hao waliibua hoja ya kama kweli mteja wao alikiri kumuua marehemu kwa nia ovu na kuna mkanganyiko wa kama alikiri kweli ama la kutenda kosa la mauaji ya kukusudia na hakuna ushahidi wa kosa hilo.
Kwa upande wake, Wakili mwandamizi wa Serikali, Wampumbulya Shani, akisaidiana na mawakili Isihaka Mohamed na Nico Malekela waliunga mkono kutiwa hatiani na adhabu aliyopewa wakisema Jamhuri ilithibitisha shitaka.
Akijenga hoja kwa niaba ya mawakili wenzake, wakili Mohamed alieleza kuwa uwepo wa dhamira ovu ya kuua ilithibitishwa kwani ushahidi unaonyesha namna marehemu alivyouawa kwa kunyongwa shingo kwa kutumia silaha aina ya kamba.
Wakili huyo alisema hata tabia ya mrufani baada ya mauaji hayo inathibitisha uwepo wa dhamira ovu, kwani alikimbia Mwanza na baadaye Songwe na alifanya hivyo kutoroka ili asiweze kukamatwa na Polisi kutokana na mauaji hayo.
Hukumu ya jopo la majaji
Baada ya kusikiliza hoja za pande mbili, majaji walisema mahakama ilimtia hatiani na kumuhukumu mrufani kwa kuegemea muunganiko wa vipande vya ushahidi ukiwamo wa mazingira na maelezo ya mrufani mwenyewe.
Majaji hao walisema ushahidi wa shahidi wa pili wa Jamhuri unaonyesha kuwa mrufani ndiye mtu wa mwisho kuonekana akiwa na marehemu akiwa hai katika nyumba ya kulala wageni ya Paradise Lodge huko katika mji wa Mugumu.
“Vielelezo (maelezo) havikupingwa wakati wa usikilizwaji wa shauri hili. Ni wakati mrufani anajitetea ndio alisema alipigwa na kuteswa na polisi na kulazimishwa kuandika maelezo hayo ingawa hakuwa amepinga wakati vikitolewa,”walisema.
“Alikuwa amechelewa sana kuibua pingamizi hilo katika hatua ya utetezi kwa vile inaonekana kama vile alitaka tu kujinasua. Mahakama ya Rufaa haiwezi kushughulika na mambo mapya ambayo hayakuzungumzwa Mahakama ya chini”
“Hii ina maana kuwa maudhui ya ushahidi uliopo katika vielelezo hivyo yanachukuliwa kama yalithibitisha kesi. Hapakuhitajika uthibitisho mwingine. Maana yake maelezo yalitolewa kwa uhiari na ni ushahidi bora kabisa”
Majaji walisema ushahidi uliopo katika maelezo hayo unaonyesha wawili hao walikuwa katika uhusiano kwa muda mrefu na walikuwa na mzozo kabla ya tukio la mauaji na hii ni kutokana na maudhui ya maelezo hayo.
Kulingana na majaji hao, ushahidi unaonyesha siku ya tukio mrufani alikuta picha za mnato na video katika simu ya mpenzi wake akiwa na mwanamume mwingine, wote wakiwa utupu na wakiwa katika tendo rasmi la kirafiki baina yao.
“Ile mrufani kuona mpenzi wake ana msaliti, ilimfanya awe amechokozwa na kushindwa kujizuia na matokeo yake iliishia kumuua marehemu na mauaji yalikuwa kwa njia ya kumnyonga kwa msaada wa kamba,”wanaeleza majaji.
“Kukutana kule kwenye nyumba ya wageni ilikuwa na lengo la kusuluhishana na kumaliza tofauti zao kwa vile mara kwa mara mrufani alikuwa alimtuhumu marehemu kuwa ana msaliti kwa kuwa na wanaume wengine”
“Wakiwa chumbani, marehemu alimuomba mpenzi wake akamnunulie chips na akakubali na mrufani akaondoka na simu ya marehemu kwenda kutafuta chips”
Kulingana na ushahidi uliochambuliwa na majaji, akiwa njiani alipekua simu ya mpenzi wake na hususan katika akaunti ya Whatsapp na akakutana na picha za mnato na video zikimuonyesha mwanamke huyo akiwa na mwanamume mwingine.
Ni kutokana na kuona picha hizo, kulimfanya akili yake iwe kama imechokozwa na ndipo alipoghairi kwenda kununua chips na kurudi chumbani akaishia kumuua mpenzi wake kwa kumnyonga kwa msaada wa kamba ya jaketi lake.
Majaji walisema wakati Jamhuri iliegemea katika maelezo ya mrufani ya kukiri kufanya mauaji kwa mazingira waliyoyaeleza, hawakuongoza mashahidi kupangua utetezi wa mrufani katika maelezo hayo kuwa ilitokana na kughadhibishwa.
Kulingana na majaji hao, hakuna shahidi hata mmoja wa Jamhuri ambaye alitoa ushahidi kueleza kuwa mrufani alikuwa amepanga kufanya mauaji hayo zaidi ya kwamba hata muhudumu anaeleza alitoka chumbani na kurudi muda mfupi baadaye.
“Kulikuwa hakuna ushahidi wowote wa Jamhuri uliokuwa unaonyesha kuwa mrufani alikuwa na silaha wakati anafika katika nyumba ya wageni na marehemu au hata wakati wa kuondoka. Hakuna aliyesema alikuwa na silaha”
“Vilevile hakuna ushahidi kuwa mrufani alienda kuleta ile kamba ambayo haikuwa sehemu ya jaketi lake ili kutekeleza dhamira yake. Wala hakuna ushahidi wa Jamhuri uliosema simu haikuwa na picha na video zinazoelezwa”
Ni kutokana na mapungufu hayo, Jopo hilo la majaji wamesema wanaona mrufani alisababisha kifo cha mpenzi wake kutokana na kughadhibishwa hivyo hana hatia ya kuua kwa kukusudia, bali bila makusudi hivyo wanamhukumu kifungo cha miaka 15.