Phiri aipeleka Simba nusu fainali

MSHAMBULIAJI wa zamani wa Simba Moses Phiri anayekipiha kwa sasa Power Dynamos ya Zambia amekiangalia kikosi cha sasa wa Wekundu hao chini ya kocha Fadlu Davids na kusema anaiona kabisa ikifika mbali katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, iwapo itaamua kukaza buti.

Raia huyo wa Zambia aliyeichezea Simba kwa misimu miwili kabla ya kuondoka dirisha dogo la msimu uliopita, aliliambia Mwanaspoti kutoka Zambia, endapo wachezaji wakiamua kufanya muendelezo wa kiwango walichokionyesha hadi kutinga robo fainali, inaweza kuwafikisha hata fainali.

Kitu alichokishauri Phiri kwa mastaa wa Simba ni kujenga moyo wa kujitolea kwa ajili ya timu, kuweka dhamira ya pamoja ya kutaka kuandika rekodi mpya CAF, anaamini wakifanya hayo njia ipo wazi kutinga fainali.

“Nimeifuatilia Simba katika mechi zao za CAF, imeonyesha kiwango na ukomavu kwa wachezaji kuamua matokeo, kadri wanavyopiga hatua ndivyo ushindani unavyozidi kuongezeka, hivyo ni kazi kwa wachezaji kuongeza bidii na wawe tayari kujitoa kwa ajili ya timu,” alisema Phiri na kuongeza;

“Simba ni kati ya klabu kubwa Afrika, ndiyo maana kwa sasa inaongoza kundi lake A kwa pointi 13, hilo linaonyesha hakuna kinachoshindika endapo viongozi, makocha na wachezaji wakiamua kuweka mikakati madhubuti ya kufika fainali.”

Alisema ana uzoefu na michuano hiyo akiwa na Simba na nje ya klabu hiyo, hivyo anasisitiza Wanamsimbazi kuongeza nguvu ili kuandika rekodi nyingine katika michuano hiyo, “Simba imekuwa kawaida kwake kutinga robo fainali, ila awamu hii naona kabisa ina wachezaji wazuri ambao wana kila sababu ya kuiwezesha kufika fainali.”

Phiri ambaye msimu wake wa kwanza kucheza Simba (2022/23) alifunga mabao 10 kabla hajaondoka  Januari 2024 kwenda kujiunga na Power Dynamos alifunga mabao matatu.

“Mbali na Simba kiwango inachokionyesha CAF pia inafanya vizuri ligi ya ndani naiona inaongoza katika msimamo, ndiyo maana nasema ina wachezaji wazuri ambao wakitulia na kuweka umakini zaidi katika kazi, msimu huu utakuwa wa manufaa makubwa kwao,” alisema.

Katika Msimamo wa kundi A  Simba inaongoza kwa pointi 13, mechi 13 imeshinda nne, sare moja na imefungwa mmoja, CS Constantine ipo nafasi ya pili kwa pointi 12, nafasi ya tatu ni Bravos do Maquis ina pointi saba na CS Sfaxien ndio inayoburuza mkiani kwa pointi tatu.