Dar es Salaam. Shindano la kusaka vipaji vya uimbaji la Bongo Star Search (BSS) limemalizika hivi karibuni na Moses Luka kutokea DR Congo kuibuka mshindi baada ya msimu huu wa 15 kushirikisha washiriki kutoka nje ya nchi ikiwa ni mara ya kwanza.
Mkurugenzi wa WCB Wasafi, Diamond Platnumz ambaye ndiye alikuwa mgeni rasmi katika fainali hiyo alitangaza kusaini washiriki wawili waliofanya vizuri katika lebo yake ambayo imetoa mastaa wakubwa wa muziki Bongo.
Kauli ya Diamond inakuja wakati BSS ikiendelea kunyooshewa vidole na baadhi ya mashabiki kuwa washiriki na hata washindi wake wengi hawafiki mbali katika muziki wa ushindani lakini wao wamekuwa wakieleza kazi yao ni kuibua vibaji na sio kuvisimamia.
Hata hivyo, katika Bongo Fleva kwa sasa kuna mshindi mmoja wa BSS anafanya vizuri, naye ni Phina aliyeibuka mshindi 2018.

Hakuna ubishi huyu anatoa changamoto kwa washindi wengine wa shindano hilo kwa miaka hivi karibuni.
Baada ya Phina kushinda BSS 2018, alijipa muda kidogo huku akifanya cover za nyimbo za wasanii mbalimbali, mwaka 2021 aliingia rasmi katika Bongo Fleva kwa kuachia wimbo wake, In Love, kisha zikafuata nyingine kama Sitaki Tena, Sio Kitoto na Pekecha.
Kufanya vizuri kwa nyimbo hizo kulipelekea Phina kushinda tuzo mbili za muziki Tanzania (TMA) 2021 zilizotolewa Aprili 2022 baada ya kusimama kwa miaka saba tangu mwaka 2015 kutokana na sababu mbalimbali.
Phina alishinda TMA 2021 kama Mtumbuizaji Bora wa Kike na Msanii Bora wa Kike Chupukizi baada ya kuwabwaga washindani wake ambao ni Abigail Chams, Marry G, Lolo Da Prince na Trixy Tonic.

Mwaka 2022 ndipo aliuwasha moto vilivyo kwa kuachia nyimbo tano ambazo ni ‘Wamerudiana’, ‘Number One’ akimshirikisha Ruby, ‘Upo Nyonyo’, ‘Hayaa’ na ‘Super Woman’ akimshirikisha Otile Brown kutokea nchini Kenya.
Na ndiye msanii pekee wa kike aliyeshirikishwa zaidi mwaka huo alifanya kolabo nane ambazo ni Natamani (Christian Bella), Yule (Stamina), Tamu (Kusah), Hata Sielewi (Barnaba), Sinsima (Chege), Tusiachene (Dully Sykes) na Singo (Baddst 47). Kufanya huko vizuri kulipelekea Phina kupata fursa ya kujiunga na kampuni kubwa ya usambazaji muziki barani Afrika na India, Ziiki Media ambayo ina ushirikiano na kampuni kubwa ya muziki duniani, Warner Music Group.
Makubaliano hayo ya miaka minne yaliyoanza Januari mwaka huu, yanalenga zaidi kuendeleza kipaji cha mwimbaji huyo, kukuza soko lake la muziki duniani kupitia usambazaji, pamoja na kukuza fursa mbalimbali za biashara ya muziki.
Basi Phina akarejea tena katika tuzo za TMA 2022 zilizofanyika Mei 2023, akaondoka tena na tuzo mbili na kumfanya kuandika rekodi kama msanii pekee aliyepita BSS kushinda tuzo nyingi zaidi za TMA kwa muda wote.

Utakumbuka alishinda kama Mtumbuizaji Bora wa Kike ikiwa ni tuzo yake ya pili katika kipengele hicho, pia alishinda kipengele cha Wimbo Bora Afrika Mashariki (Super Woman) ft. Otile Brown wa Kenya.
Kufuatia ushindi huo, Phina iliifikia na kuivunja rekodi ya Kala Jeremiah aliyeshinda tuzo tatu za TMA 2013 baada ya kuachia wimbo wake, Dear God akiwa ni msanii wa kwanza Hip Hop Bongo kufanya hivyo.
Hata hivyo, Kala Jeremiah hakuwa mshindi namba moja kama ilivyo kwa Phina, Kala ambaye alishiriki BSS 2006, yeye alishika nafasi ya nne na kupewa zawadi ya kompyuta na meza yake pamoja na deki.
Sasa tangu kurejea kwa tuzo za TMA mwaka 2022, Phina ni msanii wa pili kushinda tuzo nyingi ambazo ni nne sawa na Nandy, wawili hawa wametanguliwa na Zuchu ambaye ameshinda tuzo saba katika misimu miwili pekee ya TMA.
Sio tuzo za TMA tu Phina anaongoza, bali hata kwenye majukwaa ya kidijitali ya kusikiliza muziki namba zake zipo juu kuliko msanii yeyote aliyewahi kupita BSS, mathalani ndani ya miaka miwili tu ana video nne zilizotazamwa YouTube zaidi ya mara milioni 10.

Utakumbuka BSS ni kipindi cha televisheni cha mashindano kinachosaka vipaji vipya vya uimbaji nchini Tanzania, kilianza mwaka 2006 na hadi sasa kimetoa wasanii wengi kama Kala Jeremiah, Peter Msechu, Walter Chilambo, Kayumba, Frida Amani, Phina n.k. Mkurugenzi Mtendaji wa Benchmark 360 ambao ndio waandaaji wa BSS, Madam Rita Paulsen, kazi aliyofanya na kampuni yake kwa Wizara ya Afya ndio iliyompatia fedha zaidi na kuanzisha shindano hilo.
Na AY ndiye alikuwa msanii wa kwanza kufanya tangazo la BSS, shindano ambalo majaji wake wa muda mrefu ni Madam Rita, Master J na Salama Jabir aliyepata nafasi hiyo baada ya kuonyesha uwezo kwa kukosoa video za muziki kupitia kipindi cha Planet Bongo.