Pezeshkian: Iran haitakataa haki ya kulipiza kisasi mauaji ya Haniyeh

 Pezeshkian: Iran haitakataa haki ya kulipiza kisasi mauaji ya Haniyeh

Picha ya mchanganyiko inawaonyesha Rais wa Irani Masoud Pezeshkian (kulia) na mwenzake wa Ufaransa Emmanuel Macron.



Rais wa Iran Masoud Pezeshkian anasema nchi za Magharibi zinapaswa kuacha mara moja kuunga mkono utawala wa Kizayuni ikiwa kweli zinataka kuzuia kuenea kwa ukosefu wa usalama katika eneo hili.

Pezeshkian alisisitiza haki ya Iran kulipiza kisasi kufuatia mauaji ya hivi karibuni ya Israel ya kiongozi wa Hamas Ismail Haniyeh mjini Tehran.

Rais wa Iran ameyasema hayo katika mazungumzo ya simu na Rais Emanuel Macron wa Ufaransa ambaye aliiomba Iran ijizuie kukabiliana na shambulio la kigaidi lililomuua Haniyeh wiki iliyopita.

 “Jamhuri ya Kiislamu ya Iran daima imekuwa na nafasi muhimu katika kuleta amani, utulivu, na usalama katika eneo na dunia na kuzuia mivutano, ukosefu wa usalama na vita,” Pezeshkian alisema.

“Hata hivyo, utawala wa Kizayuni pamoja na vitendo vyake vya jinai na kigaidi dhidi ya watu wanaodhulumiwa na wasio na ulinzi wa Ghaza na mauaji ya shahidi Haniyeh akiwa mgeni rasmi wa Iran, unalenga kulitia moto eneo hili.”

“Kwa bahati mbaya, Marekani na nchi za Magharibi, badala ya kulaani utawala huu, wanauunga mkono katika kufanya uhalifu, mauaji ya halaiki na ugaidi.”

Rais wa Iran alisema Marekani na washirika wake katika nchi za Magharibi wameshindwa kulaani mashambulizi ya Israel dhidi ya ubalozi wa Iran mjini Damascus mwezi Aprili na mauaji ya Haniyeh, akielezea tabia zao kama mfano wa wazi wa undumilakuwili.

Pezeshkian alisikitika kuwa nchi za Magharibi zinaunga mkono utawala usiozingatia sheria na kanuni zozote za kimataifa na haujizui na vitendo vyovyote vya uhalifu katika eneo, na wakati huo huo kuzialika nchi zinazolengwa na vitendo hivyo kuacha kujibu na kujizuia. .

Kamanda Mkuu wa Jeshi la Iran amepongeza kuteuliwa kwa Yahya Sinwar kama kiongozi mpya wa kisiasa wa Hamas, akionya kwamba utawala wa Israel hivi karibuni utakabiliwa na jibu kali kutokana na mauaji ya mkuu wa harakati ya muqawama wa Palestina Ismail Haniyeh.

Pezeshkian amesema, maadamu utawala wa Kizayuni kwa uungaji mkono wa kisiasa, kifedha, kijeshi na vyombo vya habari vya Marekani na nchi za Magharibi unajihusisha na mauaji ya kimbari, jinai na ugaidi, eneo na ulimwengu hautaona utulivu, usalama na amani. .

 “Iwapo Marekani na nchi za Magharibi zinataka kweli kuzuia vita na ukosefu wa usalama katika eneo, lazima ziache mara moja kuuza silaha na kuunga mkono utawala wa Kizayuni na kuulazimisha kusimamisha mauaji ya kimbari na mashambulizi dhidi ya Ghaza na kukubali kusitishwa mapigano.”

Rais wa Iran amesema Tehran haitafuti vita na inajitahidi kuendeleza amani duniani, lakini kamwe haitakaa kimya mbele ya uchokozi dhidi ya maslahi na usalama wake.